Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Majina ya maeneo Zanzibar yanavyoacha watu midomo wazi

Mwonekano wa maghorofa katika eneo maarufu la Michenzani. Maghorofa hayo ni sehemu ya urithi wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume. Picha na Jesse Mikofu

Zanzibar ina simulizi na historia inayoweza kumvuta yeyote anayeisikia. Sio simulizi za masaibu ya historia ya siasa kwa wakazi wa kisiwa hicho kikubwa zaidi katika Bahari ya Hindi, lakini hata katika nyanja nyingine ikiwamo ya maendeleo ya makazi.

Kwa pamoja, visiwa vya Unguja na Pemba vinavyounda Zanzibar, vina utamaduni wa kipekee wa utoaji majina kwa maeneo yake. Kwa anayesikia   majina hayo kwa mara ya kwanza, ni rahisi kupatwa na mshangao na pengine kujiuliza maana ya majina hayo. 

Hebu pata picha unaposikia kwa mara ya kwanza ufundi uliotumika wa kupata  majina ya maeneo kama Mchambawima,  Mfereji Maringo, Jambiani, Kibanda maiti, Kaburi Kikombe, Chokocho, Mangapwani, Makunduchi,Saateni,  Kijito upele, Bububu, Mlandege na mengineyo.

Ni majina yanayomvutia msikilizaji kutaka kujua maana yake. Huu ndio utamu wa utamaduni wa majina ya maeneo katika visiwa vingi ambavyo pia vina sifa ya kutumia miti kuyapa majina maeneo yake.

Zanzibar imejaa majina kama Mfenesini, Mkunguni, Miembeni, Kikwajuni, Mtundani,  Michenzani, Migombani, Mtendeni, Misufini, Mkunazini na mengineyo.

Hata hivyo, mti uliotia fora zaidi kutumika ni mwembe, kwani umekuwa ukitumika sambamba na majina mbalimbali kama vile Mwembeshauri, Mwembatanga, Mwembenjugu, Mwembebeni, Mwembeladu, Mwembe kisonge, Mwembe mchomeke, Mwembemimba, Mwembe makumbi, Mwembe matarumbeta.

Lakini pia upo mti wa mbuyu wenye maeneo kama Mbuyu kidambwita, Mbuyu pacha na Mbuyu  taifa.

Zanzibar pia tajiri wa maeneo yanayotokana na watu. Mifano ya maeneo hayo na watu husika kwenye mabano ni Kwahani (Ali Hani), Kwaalimsha (Ali Mcha), Kwasharifmsa (Sharifu Musa), Kwaalinatoo (Ali Natoo)

Makala haya  kwa kurejea vyanzo mbalimbali, yanaangazia asili na   historia ya baadhi ya majina ya maeneo maarufu kisiwani humo.


Bububu

Wengi hawajui kama Zanzibara hasa Unguja iliwahi kuwa na usafiri wa reli iliyojengwa mwaka 1905. Sauti na mlio wa   treni hiyo ilipokuwa  ikipita ikazaa jina bububu. 

Barabara katika eneo la Bububu.

Hivyo bububu ni tanakali sauti yaani jina linalotokana na sauti ya kitu. Kama ilivyo sauti nyau kupewa paka/ nyau, ndivyo sauti ile ya treni ikipita relini bu-bu-bu ilivyozaa jina la eneo Bububu.


Mangapwani

Ni jina linalomaanisha pwani/ ufukwe wa mmanga au mwarabu. Eneo hilo kwa kuwa  ni la pwani na lilikuwa likikaliwa na Wamanga yaani Waarabu, wazazi wa Kiafrika walikuwa wakiwakataza watoto wao kwenda kucheza maeneo ya pwan,  wakiwaambia kuna Wamanga pwani, hivyo neno Mangapwani likazaliwa kumaanisha pwani ya Wamanga/ Waarabu.


Uzini

Inasemekana kuwa huko zamani wakazi wa hapo walitaka kulinda eneo lao, wakachimba mtaro kuzunguka eneo zima na kuweka uzi ndani ya mtaro huo  kama ishara ya dawa ya  kutambika.

Ikawa watu wakitaka kwenda hapo wanasema wanakwenda Uzini, huo ukawa mwanzo wa jina Uzini.


Mwembemchomeke

Nilisema awali kuwa wakazi wa Zanzibar walitumia utundi na ustadi wa hali ya juu kuyapa majina maeneo hayo. Moja ya jina ni mwembemchomeke lililotumiwa kama tafsida ya kuficha hali matendo ya utusitusi yaliyokuwa yakifanyika eneo hilo.

Mwonekano wa sasa wa eneo la Michenzani.

Simulizi zinaonyesha kuwa eneo hilo lilikuwa na matukio mengi ya ubakaji na kwa kupunguza ukali wa lugha, wenyeji wakapaita hapo Mwembe mchomeke.


Kibanda maiti

Ni eneo lililopo Unguja shehia ya Nyerere. Jina hilo limetokana na awali eneo hilo kuwa na kibanda kilichokuwa kikitumika kuoshea maiti.


Kisiwa Ndui

Ni mahala ambapo simulizi zinaeleza kuwa watu waliokuwa na ugonjwa wa ndui walihifadhiwa.


Mchambawima

Ustadi mwingine wa lugha kwa Wazanzibari unajionyesha katika jina la Mchamba wima. Kilugha kuchamba ni kujisafisha hasa kwa kutumia maji,  pindi mtu anapotoka kujisaidia tena akiwa amechuchumaa.

Sasa simulizi zinaonyesha kuwa eneo hili lilikuwa na maji mengi hivyo kuwalazimu wapita njia kukunja nguo zao wanapopita

Kitendo cha kukunja nguo hali ya kuwa wamesimama kikafananishwa na mtu aliyevua nguo na kuchamba akiwa amesimama.


Chuini

Inaelezwa kuwa eneo hilo zamani kulikuwa na bustani na jengo lililokuwa likifuga wanyama wakiwamo chui.

Unadhani ni majina haya tu yanayowacha watu midomo wazi? La hasha! Yako mengi sana. Mwananchi tumeanza, wengine wanaweza kuchimba zaidi kuhusu utamaduni huu wa utoaji majina katika visiwa hivi vya karafuu.