Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mikakati kufungua wigo wa utalii Pemba

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mudrik Ramadhani Soraga (katikati) akizungumza wakati wa  kuzindua bonanza la michezo na utamaduni Pemba (PTCB) kulia ni Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Aboud Suleiman Jumbe na Katibu Mtendaji Kamisheni ya utalii Zanzibar, Arafat Abbas Manji. Picha na Zuleikha Fatawi

Muktasari:

  • Bonanza la utamaduni na michezo Pemba (PTCB) laandaliwa kukifungua kisiwa hicho.

Unguja. Ili kukifanya Kisiwa cha Pemba kuwa kitovu cha utalii wa kijani, Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar kwa kushirikiana na Kamisheni ya Utalii imezindua bonanza la utamaduni na michezo Pemba (PTCB).

Bonanza hilo linatarajiwa kuanza Novemba 27 hadi 30, mwaka huu katika uwanja utalii Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba. Litakuwa na fursa mbalimbali, ikiwemo kutembelea maeneo ya historia, michezo na burudani.

Akizungumzia bonanza hilo leo Novemba 8, 2024, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Ramadhan Mudrik Soraga amesema linaenda kuboresha taswira ya Pemba kimataifa kuwa kituo cha utalii wa urithi na michezo. 

Amesema utalii wa michezo una nafasi kubwa katika kuongeza hamasa, kushawishi vijana na kushirikisha jamii kuwavutia watalii wa ndani na nje ya nchi.

"Tunatarajia kuifungua Pemba kuwa kitovu cha utalii wa kijani unaohamasisha michezo, urithi na utamaduni wetu, hivyo bonanza hili litasaidia kuongeza idadi ya watalii, kukuza uchumi na kuwavutia wawekezaji," amesema.

Sekta ya utalii ndiyo mama kisiwani humo na huchangia pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 30.

Pia utalii unachangia zaidi ya asilimia 30 ya fedha zote za kigeni na inatoa ajira zaidi ya 200,000 sawa na zaidi ya asilimia 60 ya ajira zote katika mnyororo wa thamani unaotokana na sekta ya utalii.

Sekta ya utalii kwa muda mrefu imekuwa na maeneo makuu mawili ya fukwe na mambo ya kale, hivyo kwa kipindi cha hivi karibuni Serikali kupitia wizara na Kamisheni ya Utalii imeanza mpango kuhakikisha inaongeza watalii na kupanua wigo wa soko hilo.

Waziri Soraga amesema mipango hiyo ni pamoja na kuanza utalii wa mikutano, maadili, halal na wa michezo ili kuendelea kushika soko kubwa la utalii na kuwavutia wageni wengi kufika katika kisiwa hicho.

Kwa sasa Zanzibar ina rekodi ya watalii zaidi ya 600,000 kwa mwaka, huku ikiwa na mpango wa kufikia watalii zaidi ya 800,000 kwa mwaka.

Pia kuongeza miundombinu, ikiwemo ujenzi wa viwanja vya ndege na kuongeza hoteli zenye hadhi ya kimataifa. Kwa sasa ina vyumba 20,000 vyenye hadhi ya kulaza watalii.

Zanzibar ina mashirika zaidi ya 80 yanayoleta ndege kutoka mataifa mbalimbali, wasafiri wakifika kwa ajili ya kutalii na shughuli nyingine zikiwamo za kibiashara.

Soraga ametoa wito kwa wadau wote kushirikiana kuchangia bonanza hilo ili kujenga na kuifungua Pemba.

Pia amewataka wanawake kisiwani humo  kujitokeza kwa wingi kushiriki katika bonanza hilo, kwani hakuna mtu ambaye atawatoa kwao bila ya kujitoa wenyewe.

Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii, Arafat Abbas Manji amesema jukwaa hilo ni mkakati unaolenga kuziwezesha jamii za ndani na kuonyesha fursa za vivutio vya kipekee kisiwani humo.

Amesema utalii wa kijani ndiyo kiini cha mkakati wa utalii wao kwani unasaidia kukuza uchumi.

"Kamisheni imeanzisha ushirikiano na taasisi mbalimbali kuwawezesha wajasiriamali wa ndani kutoa uzoefu wao halisi ikiwemo maandalizi na shughuli mbalimbali za nyumbani, ziara za vijijini na maonyesho ya kiutamaduni," amesema.

Amewahimiza wageni watakaohudhuria katika bonanza hilo kuheshimu mazingira, utamaduni na watu waliopo kwa lengo la kunufaisha jamii zao.

Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo, Rahim Bhaloo amesema ni wakati sahihi kwa wananchi wa Pemba kuitumia fursa hiyo kuzalisha mazao mapya ya utalii.

Bhaloo amesema ili kuwavutia watalii kisiwani humo lazima wananchi wa Pemba wawe tayari kukubali mabadiliko.

“Fursa hii ni muhimu tusiiache maana itasaidia kutengeneza ajira na kuwakwamua kimaisha, huu ni mkakati maalumu wa kuwapeleka watalii Pemba kukuza utalii na vipato vya wananchi,” amesema.