Mwinyi ataka utafiti elimu ya juu uisaidie Serikali

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewataka wahadhiri na wanataaluma kufanya utafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Serikali ili iweze kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zilizopo.
Dk Mwinyi alieleza hayo jana, katika mahafali ya 21 ya Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) yaliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Tunguu, Unguja.

"Vyuo vikuu vya umma na binafsi vina mchango muhimu katika kuhakikisha nchi yetu inatoa elimu iliyobora na kuchochea maendeleo katika nyanja zote, ushirikiano wa pamoja unahifajika kufanya tafiti zenye tija kwa maendeleo ya Taifa letu," alisema.

Dk Mwinyi alibainisha kuwa ni matumaini yake wasomi hao watatekeleza wajibu huo ili kuisaidia Serikali kupata ufumbuzi wa changamoto, kwa kuwa lengo ni kuona wataalamu wa ndani nao wanatoa mchango ipasavyo katika tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu.

Alisema tangu alipoingia madarakani mwaka 2020, Serikali yake imeweka kipaumbele katika sekta ya elimu na kuzifanyia kazi changamoto zinazoikabili sekta hiyo, ili iweze kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya Zanzibar kwa ujumla.

Alisema nguvu kazi yenye elimu bora na maarifa ndiyo itakayoweza kutoa mchango mkubwa wa maendeleo kwa kila sekta.
Rais Mwinyi alisema pamoja na sekta ya elimu, Serikali imeweka mkazo katika kuimarisha afya kwa kufanya mageuzi, ikiwemo kuangalia upya sera na mifumo ya utoaji wa huduma.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, Zanzibar kwa sasa ina wataalamu wengi wa fani mbalimbali za afya tofauti na miaka ya nyuma.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Mohamed Mussa, alisema chuo hicho kimekuwa kikitoa kozi mbalimbali zinazotoa wahitimu wenye taaluma nzuri ambao wanasaidia serikalini.

Alisema vyuo vikuu vina dhamana kubwa ya kuongeza wigo wa miundombinu, wataalamu katika fani ya sayansi kwani kuna changamoto ya wahitimu kwenye eneo hilo kama madaktari na wafamasia.

“Uongozi wa vyuo vikuu ulichukuehilo na kuliundia mkakati kuhakikisha vijana wetu katika ngazi ya maandalizi, msingi na sekondari wanafaulu vizuri ili wapate fursa ya kusoma fani za sayansi,” alisema Waziri Lela.

Naibu Makamu mkuu wa Chuo, Dk Rashid Juma Rashid alisema chuo hicho kimekuwa kikiongeza idadi ya wahitimu kila mwaka ambao wana ubora na viwango katika nyanja mbalimbali za kitaaluma.

Alisema hiyo ni hatua nzuri kwa chuo hicho kuongeza idadi ya masomo kila mwaka na kuongeza wigo wa wataalamu wenye viwango bora.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha ZU, Juma Burhan Mohammed, aliwataka wahitimu hao kutumia wakala wa Uwezeshaji Kiuchumi kwa ajili ya kupatiwa mafunzo ambayo yatawasaidia kujiajiri bila ya kutegemea ajira kutoka serikalini.