Nchimbi: SUK imezuia damu Zanzibar
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi.
Unguja. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema kama kuna watu wanaona Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) haina maana, ni dhahiri wanataka kuendelea kuona damu za watu zikimwagika.
Amesema CCM kina msimamo usioyumba kuhusu umoja, utulivu wa Taifa, hivyo wataendelea kuunga mkono SUK ili kuimarisha utulivu huo.
Dk Nchimbi alieleza hayo jana alipozungumza na mamia ya wanachama wa CCM waliojitokeza kumpokea katika viwanja vya Ofisi Kuu za chama hicho Zanzibar, ikiwa ni siku chache baada ya kutangazwa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.
Dk Nchimbi aliteuliwa kushika wadhifa huo Januari 15, mwaka huu katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM uliofanyika Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan.
“Wale ambao wamezaliwa juzi wanaweza wasijue maana ya neno siasa za kihasama. Miaka ya 2000, tumeshuhudia siasa za kihasama zilizokuwepo Unguja na Pemba. Watu wa familia moja wamenuniana hawazungumzi mwaka mzima, halafu kuna watu wanaona hakuna umuhimu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema.
Aliongeza: "Wewe ukiona mtu ana hamuhamu hivi ya kuona Serikali ya Umoja wa Kitaifa imevunjika basi ujue muda wote anapotembea pua zake zinatamani kunusa damu za watu."
Katika kusisitiza hilo Dk Nchimbi alisema: “Kwa hiyo lazima tuungane tushirikiane wana-CCM wote, msimamo wetu usiyumbe kwamba tunaunga mkono SUK na tunawapa shime wenzetu wa ACT- Wazalendo kwamba nao wana wajibu wa kuunga mkono Serikali ya Umoja wa Kitaifa.”
Kwa mujibu wa katibu mkuu huyo, kama kuna mambo madogomadogo ambayo hayaendi sawa, yanapaswa kuzungumzwa na ndiyo maana ya maendeleo na maana halisi ya ushirikiano.
“Ni lazima tujue wote ni Wazanzibari, sote ni Watanzania suala la kupendana sisi kama Watanzania ni wajibu wa kiraia," alisema.
Alisema wanaposema Serikali ya Umoja wa Kitaifa iendelee kuwapo wanayasema kwa dhati, huku wakijua wanataka kuendelea kushirikiana na ndugu wote, huku na wakiwa na imani ya dhati kwamba, wanafanya hivyo kwa nia njema na ni sehemu ya kuenzi Mapinduzi.
Alisema waasisi wa Mapinduzi hawakukusudia kuwa na nchi iliyojaa uhasama, chuki na isiyo na umoja.
“Haya hayakuwa matarajio ya waasisi wa nchi yetu, waasisi wa chama chetu wala matarajio ya waasisi wa Mapinduzi,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kueleza alivyofurahishwa na maono ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ya kuendeleza SUK kwa masilahi mapana ya nchi.
Mtendaji mkuu huyo wa CCM, alisema amekutana na Dk Mwinyi akamuuliza anachofikiri kuhusu SUK na yeye (Dk Mwinyi) akamjibu ni muhimu kwa Zanzibar na Tanzania, kwa hiyo amefurahishwa kusikia kauli hiyo kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM.
Kauli ya ACT
Akizungumza na Mwananchi kwa simu kuhusu kauli hiyo, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT-Wazalendo, Salim Bimani alisema wanachotaka ni utekelezaji wa vitendo wa yote yaliyokubaliwa kuwamo katika SUK na si maneno.
“Msimamo wa chama ni mfupi tu, kuna masuala ya msingi ya makubaliano yanahitaji kutekelezwa kivitendo na si maneno, yakitekelezwa yale yote tuliyokubaliana sisi hatuna zaidi ya hapo,” alisema.
Alisema wa kuamua kutekeleza ni CCM, hivyo kama Dk Nchimbi kasema hivyo pengine anataka kuona mambo yakienda.
Mbali na kauli ya Bimani, hivi karibuni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT- Wazalendo ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud akiwa katika mkutano wa hadhara Mtonikidatu, alisema kama mambo hayaendi hawana sababu ya kuendelea kuwa na SUK.
Kauli hiyo ilirudiwa na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Juma Duni Haji alipozungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu nyumbani kwake Kisauni. Alisema wala hawatanii kuhusu kujiondoa katika SUK
Miongoni mwa sababu zinazotajwa na chama hicho kikuu cha upinzani Zanzibar, ni kutotekelezwa kwa matakwa waliyokubaliana kuingia kwenye SUK, ikiwa ni pamoja na kutoshughulikiwa hoja zao 26 mbali na zile tatu za Maalim Seif Sharif Hamad alizokubalina na Dk Mwinyi.
Aidha, alisema kamati ya maridhiano ambayo iliundwa haifanyi kazi.
Duni katika mazungumzo na gazeti hili alifafanua kuwa, Desemba 2020 aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, hayati Maalim Seif Sharif Hamad, akiongoza ujumbe wa ACT-Wazalendo, walifanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, pamoja na mambo mengine yakilenga kuleta utulivu baada ya uchaguzi.
Katika mazungumzo hayo, alisema walipendekeza kufanyika mabadiliko katika taasisi mbalimbali, ikiwemo Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuwezesha kuwapo uchaguzi huru na wa haki ifikapo mwaka 2025, pendekezo analodai halijatekelezwa.
“Tulipendekeza kufumuliwa kwa sheria ya uchaguzi ya Zanzibar na kufanyiwa maboresho. Mfano, sheria inasema kupiga kura siku mbili, hivi kweli watu 500,000 wanaweza kupiga kura kwa siku mbili?” alihoji Duni.
Alisema licha ya Rais Mwinyi kuwaachia huru wanachama wa ACT-Wazalendo walioathiriwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, hawajapelekwa hospitali wala kufidiwa.
“Hawa walitakiwa kufidiwa, bado hakuna kilichofanyika hadi sasa, waliokuwa wagonjwa hawajapelekwa hospitali,” alisema.
Alisema baadhi ya mambo yaliyolalamikiwa katika uchaguzi wa mwaka 2020 ni uwepo wa Mkurugenzi wa ZEC, Thabit Idarous Faina ambaye bado anaendelea na majukumu yake.
Duni maarufu ‘Babu Duni’ alidai baadhi ya watendaji wa Serikali wanadharau makubaliano waliyoingia na Dk Mwinyi, akitoa mfano mmoja wa mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), aliwahi kutamka kuwa hamtambui Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman.
“Hii ina maana gani? Yaani anamtambua Dk Mwinyi na Hemed Suleiman Abdulla (Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar). Sasa tuamini vipi katika kauli ya waziri anayesema hivi na Rais yupo? Hakuna mtu yeyote aliyesema hayo ni maneno yake (waziri)” alisema.
Duni alisema lugha zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali zinaidhalilisha ACT-Wazalendo, ndiyo maana Othman alisema itafika mahali chama hicho, kitajitoa ndani ya SUK.
Usimamizi wa Serikali
Wakati huohuo, Dk Nchimbi alisema katika kipindi ambacho atakuwa katibu mkuu, chama kitaimarisha usimamizi wa Serikali zake kuhakikisha zinatimiza wajibu wake kwa kutekeleza ilani ya CCM na kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.
Alisema kazi anayoifanya Rais Samia na Dk Mwinyi ni kubwa, inahitaji kuimarishwa kwa usimamizi wa Serikali hizo, huku akiwahakikishia wanachama kwamba watauimarisha.
Kuvunja makundi
Alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wanachama kuvunja makundi akisema pindi uchaguzi unapomalizika nayo lazima yafe.
Dk Nchimbi alisema baada ya uchaguzi walioshinda lazima wawe wanyeyekevu na walioshindwa wajue kwamba kushinda au kushindwa kupo katika mapenzi ya Mwenyezi Mungu.
Alisema kama hukushinda leo utashinda kesho, huku akitoa mfano wake kwamba aligombea mara 27 lakini sita alishindwa.
“Unapotaka kupika, ndiyo unawasha moto, ukimaliza kupika unazima moto wako. Ni mjinga peke yake anayeendelea kukoleza moto wakati ameshapakua, nawasihi wana-CCM.”
"Utashindwa leo lakini utashinda kesho, mimi nimegombea nadhani mara 27, nimeshindwa mara sita wala haikuwa shida na ukiwa kama mwanasiasa kushindwa nayo ni raha, na kama hujawahi kushindwa wewe si mwanasiasa bwana," alisema.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohammed Said Mohammed (Dimwa), alisema kwa mujibu wa Katiba ya CCM ibara ya 15, wajibu wa wanachama ni kujua kwamba chama ndiyo chenye uwezo na nguvu zinatokana na umoja wa wanachama.
Alisema wana imani kwa uwezo wa Dk Nchimbi na ushirikiano wa wanachama, atakivusha chama hicho katika uchaguzi mkuu mwaka 2025.