Othman: Wanawake nguvu yenu kubwa, ongozeni vuguvugu la mabadiliko
Muktasari:
- Othman Masoud, makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema kama wanawake wanataka machozi yao yafutwe na yasitokee tena ili heshima yao ilindwe na ya nchi, lazima wasimame kama raia huru kulinda heshima hizo kwa kupambania mabadiliko.
Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud amesema wanawake wanapaswa kuwa mstari wa mbele kupigania mabadiliko, kwani wao ndio waathirika wakuu wa mifumo na madhila yanapokuwapo mfumo mbovu wa kutoa haki.
Ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Novemba 10, 2024 wakati akifungua kongamano la wanawake wa chama hicho mjini Unguja, lenye kauli mbiu ‘wanawake na ushindi mwaka 2025’
Othman ambaye pia ni makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema kama wanawake wanataka machozi yao yafutwe yasitokee tena na heshima yao ilindwe na ya nchi, lazima wasimame kama raia huru kulinda heshima hizo kupambania mabadiliko.
“Mwanamke ana kila sababu kudai mabadiliko, kwani ndio yatamfanya aache kulia na kumtua mzigo alioubeba, kama hamkufanya hivyo wenzenu hawana muda na mambo haya yataendelea,” amesema Othman.
Amesema kila yanapotokea madhila mwathirika wa kwanza ni mwanamke, “mabadiliko ni haki yenu, tusikubali nchi hii ikaendelea kuendeshwa kama sisi tupo karne ya 12, tumeshatoka huko karne ya sasa ya 21 hatuwezi kukubali kuendelea hivyo.”
Othman amesema mwaka 1961 watu 68 waliuawa baada ya kutokea machafuko, lakini Serikali ilifanya jitihada na kuchukua hatua kwa kuzingatia misingi ya sheria na wapo waliofungwa na wengine kupigwa faini.
Pamoja na watu kufungwa, pia Serikali ilichukua hatua za kubadilisha sheria ya jinai ili yasitokee tena, lakini kwa kipindi cha miaka ya karibuni mambo hayo yameendelea kutokea na hakuna hatua zinazochukuliwa.
“Dunia nzima ilijua kupitia ripoti hiyo nani alikosa, nani alifanya kwa sababu gani, leo tunasema tupo nchi huru, lakini madhila yanayotokea hakuna hatua tunaona zinachukuliwa, wenye kupaza sauti ni nyie wanawake,” amesema Othman.
Amesema ikiwa hali duni za kiuchumi kwenye nchi si kwa sababu ni mipango ya Mungu, bali ni kwa sababu ya ufisadi uliokithiri ya kutojali maslahi ya wengine.
“Mimi niwaombe sana tuwe pamoja kwa kauli moja, sote tulaani kilichotokea mwaka 2020 na kwamba hakuna hatua iliyochukuliwa, tutake hatua zichukuliwe kupitia sauti zetu,” amesema.
Amesema mambo yanayoendelea katika Taifa hilo yanapaswa kulaaniwa, kwani si mambo yanayopaswa kutokea kwenye nchi yenye katiba, sheria na mifumo ya utoaji haki na kwamba watu wanapotea wanakutwa wameuawa, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa. Amerejea tukio la hivi karibuni la Ramadhan Iddi, aliyechukuliwa na watu saa 12 jioni, kisha siku iliyofuaya akakutwa ameuawa.
“Uchunguzi ufanyike wa wazi na waliohusika wote wachukuliwe hatua, tusirudi tulipokuwa tuchukue hatua kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria, tusizidishe machozi ya mwanamke, bali tuchukue hatua kuyasitisha,” amesema.
Makamu mwenyekiti ngome ya ACT Wazalendo-wanawake Taifa, Mkunga Sadala amesema kongamano hilo litakuwa na mada mbili ambazo ni mwanamke jasiri na mwanamke na uongozi.
Amesema lengo ni kuhamasisha wanawake kushiriki katika harakati za siasa kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2025.
“Ni kuongeza ujasiri kwa wanawake kujitoa kwenye siasa na kujitoa kugombea nafasi mbalimbali wakati tunaelekea katika uchaguzi mkuu mwakani,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mkunga amesema ngome hiyo ya wanawake imesikitishwa na mchakato wa kuwaengua wagombea katika uchaguzi wa serikali za mtaa, akidai lengo ni kuwakatisha wanawake tamaa lakini wasiogope waendelee kupambania haki zao.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Omar Ali Shehe amesema “wanawake ni jeshi kubwa, imara na makini hivyo kupitia kongamano hili mtachora ramani na kujenga barabara kwa kupitia vijiji, mitaa na milango kuhakikisha mnampeleka Othman Masoud Ikulu 2025.”
Awali akitoa salamu, mwenyekiti mstaafu, Duni Haji (Babu Duni) amesema ushindi unapopatikana wanawake wanakuwa mstari wa mbele kuliko wanaume.
“Wanawake ndio waathirika wakuu wa madhila yanayotokea kwa hiyo niwasihi muendelee kupambana zaidi,” amesema.