Ripoti yaanika chanzo kifo cha Mmarekani Ashlee Jenae hotelini Zanzibar
Mwanaharakati wa mitandao ya kijamii kutoka nchini Marekani, Ashlee Jenae Robinson enzi za uhai wake.
Muktasari:
- Takribani miezi miwili imepita sasa tangu kitokee kifo cha Mmarekani huyo katika Hospitali ya Ampolla aliwahishwa kwa ajili ya matibabu baada ya kukutwa akining’inia kwenye chuma cha kabati ndani ya Hoteli ya Zuri alipokuwa na mchumba wake.
Unguja. Jeshi la Polisi Kamisheni ya Zanzibar kupitia Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar limetoa taarifa ya uchunguzi wa kifo cha mwanaharakati wa mitandao ya kijamii kutoka nchini Marekani, Ashlee Jenae Robinson (31), kwamba alijinyonga kutokana na msongo wa mawazo.
Tukio la kujinyonga lilitokea Aprili 8, 2026 saa 2:55 usiku katika Hoteli ya Zuri Mkoa wa Kaskazini Unguja ambako alikuwa na mchumba wake Joseph McCann, kisha alifariki dunia Aprili 9, wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Ampolla Mkoa wa Mjini Magharibi.
Katika taarifa za awali zilizotolewa na polisi, zilieleza kwamba binti huyo alijinyonga baada ya kutofautiana na mchumba wake licha ya wakati huo pia kuwapo kwa baadhi ya taarifa kwenye mitandao ya kijamii zikieleza kwamba aliuawa na mchumba wake.
Kutokana na sintofahamu hizo, Jeshi la Polisi lilianza uchunguzi wa tukio hilo ikiwa ni pamoja na kumshikilia mchumba wa Ashlee kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari leo Juni 4, 2026, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Zuberi Chembera, amesema imethibitika bila shaka kwamba mwanaharakati huyo alijinyonga kwa sababu ya msongo wa mawazo.
“Kupitia maelezo ya mashahidi na vifaa vya mawasiliano vya marehemu na mchumba wake, tumegundua marehemu alikuwa na tatizo la msongo wa mawazo kwani kupitia ujumbe mfupi (SMS) za marehemu na mchumba wake zimeonesha mara kwa mara alikuwa akilalamika kuhusiana na mwenendo wa maisha yake,” amesema.
“Baada ya upelelezi huo kwa kushirikiana na taasisi zingine, upelelezi umethibitisha bila shaka yoyote tukio la marehemu alilolifanya tarehe hiyo la kujaribu kujinyonga ndiyo lililosababisha kifo chake baadaye, hivyo hakuna mtu yeyote anayeweza kuhusishwa kwa namna yoyote ile kwenye kifo hicho,” amesema.
Ilivyokuwa
Kwa mujibu wa polisi, Ashlee aliingia Hoteli ya Zuri Aprili 6 akiwa na mchumba wake McCann na kupangishwa nyumba namba 25.
Siku ya tukio, Aprili 8, saa 12 jioni kulitokea hali ya kutokuelewana baina ya marehemu na mchumba wake, ambapo walikuwa na mizozo isiyoeleweka ilikuwa na muktadha gani.
Taarifa za polisi zinaeleza kwamba taarifa ya kutokuelewana kwao ilifika kwa uongozi wa hoteli, hivyo uongozi wa hoteli uliamua kumuhamisha mchumba wake na kumpangia nyumba namba 65 kwa muda wakati suala lao la kutokuelewana likiendelea kushughulikiwa na uongozi wa hoteli hiyo.
Kwa mujibu wa Chembera, majira ya saa 2:55 usiku mmoja kati ya wahudumu wa hoteli hiyo akiwa katika shughuli zake za kawaida za kutoa huduma za jioni ikiwemo kupuliza dawa za wadudu, kuteremsha neti na kufanya usafi kwenye villa hizo, alipofika namba 25, akakuta kuna giza na mlango umefungwa.
“Aligonga ili kupata kufunguliwa lakini hakupata majibu, hakuna mtu aliyeitikia, hivyo akaamua kutumia ufunguo wa akiba aliokuwa nao. Alifungua na kuwasha taa na ghafla upande wa kushoto wa mlango akasikia kishindo cha mtu kama anajigonga, ndipo alipogeuka akamkuta Ashlee ananing’inia kwenye kabati,” amesema.
Alikuwa kwenye chuma cha kuweka hanger za nguo akitumia mkanda wa nguo ambazo wateja huzitumia wakiwa vyumbani.
Jeshi la Polisi Tanzania Kamisheni ya Zanzibar linatoa wito kwa wazazi na walezi kuendelea kuwa karibu na watoto na vijana ili kujua mienendo ya maisha yao ya kila siku na kuelewa pindi wanapokuwa na changamoto zozote za kimaisha pamoja na kuwashauri ili kuepusha watoto na vijana kuchukua maamuzi magumu.
Mazishi ya Ashlee Jenae yalifanyika Mei 5, 2026 katika Jimbo la New Jersey, Marekani, ambapo ibada ya mazishi ilifanyika kwenye kanisa la Second Baptist.