Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sekta tano zinazoubeba uchumi wa buluu

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Finland nchini, Theresa Zitting, leo Oktoba 11, 2023 Ikulu, Zanzibar

Muktasari:

  • Dk Mwinyi anadi fursa za uwekezaji katika uchumi wa buluu, akiialika Finland kuwekeza Zanzibar

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali imeimarisha sera ya uchumi wa buluu inayobeba sekta tano; huku akiikaribisha Finland kuangalia fursa za uwekezaji katika maeneo hayo.

Sekta hizo ni utalii, uvuvi, usafiri wa vyombo vya baharini, bandari, mafuta na gesi.

Dk Mwinyi amesema hayo leo Oktoba 11, 2023 Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Balozi wa Finland nchini, Theresa Zitting.

Amesema sekta ya utalii inajumuisha fukwe zenye mvuto kwa wageni na urithi wa kale, maeneo yenye fursa nyingi za uwekezaji.

“Tumeimarisha sera ya uchumi wa buluu, zipo fursa nyingi kwa hiyo Finland inakaribishwa kuziangalia na kuweka Zanzibar,” amesema

Kuhusu uvuvi, Rais Mwinyi amesema Zanzibar imejikita kwenye viumbe wa baharini, ikiwamo ufugaji wa samaki na vifaranga; pia kilimo cha matango bahari na mwani.

Kilimo hicho kwa kiasi kikubwa kimewajumuisha wanawake na vijana, hivyo kupunguza changamoto za ajira.

Akizungumzia usafiri baharini, Dk Mwinyi amesema unajumuisha bandari za Zanzibar, Dar es Salaam, Pemba na Tanga kwa kusafirisha abiria na mizigo.

Pia, amezungumzia ushirikiano katika miundombinu ya elimu, afya na nishati, hasa kwenye mifumo na vitendea kazi.

Ameipongeza Finland kwa kuisaidia Zanzibar katika sekta za elimu, kilimo, afya na masuala ya wanawake, hususani mapambano dhidi ya udhalilishaji wa kijinsia kwa kushirikiana na taasisi na wanaharakati mbalimbali.

“Naipongeza Finland kwa mchango wake wa kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, haya ni maeneo machache kati ya mengi ambayo tumepata msaada mkubwa,” amesema Dk Mwinyi.

Balozi Theresa kwa upande wake amesema Serikali ya Finland inafanya kazi kwa karibu na Serikali ya Zanzibar, wakishirikiana kwenye sekta za maendeleo.

Amesema Finland imeshirikiana na Tanzania hasa katika sekta ya elimu na kuimarisha miradi ikiwamo ya uhifadhi wa mazingira, ardhi, misitu na masuala mengine ya maendeleo.

Amesema Taifa hilo linathamini uhusiano na ushirikiano uliopo baina ya Finland, Tanzania (Zanzibar ikiwamo) na nchi zote zilizopo Afrika Mashariki.