Utapiamlo unavyoathiri watoto Zanzibar

Muktasari:

  • Ripoti ya Afya na Lishe Shuleni yaonyesha watoto watatu kati ya watano wana utapiamlo Zanzibar.

Dar es Salaam. Ripoti ya Afya na Lishe Shuleni mjini Zanzibar ya mwaka 2022 inaonyesha asilimia 58.4 ya watoto wenye umri wa kuanza shule na waliopo shuleni kuanzia miaka 5-19 wana utapiamlo.

Takwimu hizo zina maana kwamba, katika kila watoto wenye umri wa miaka mitano hadi 19 watatu kati ya watano wanakabiliwa na utapiamlo.

Utapiamlo kwa maana ya udumavu, upungufu wa damu, uzito pungufu, uzito kupita kiasi na ukondefu ni hali ya afya duni itokanayo na ulaji usiokidhi mahitaji ya mwili au uliopitiliza.

Ripoti hiyo inaonyesha asilimia 41.6 ya watoto waliopo shule wa umri kati ya miaka 5-19 wana aina moja ya utapiamlo.

Mgawanyo wa takwimu hizo unaonyesha asilimia 45.7 ya watoto wa shule za sekondari na msingi wana upungufu wa damu (anemia), asilimia 15.6 wamedumaa, asilimia 13.9 wana uzito pungufu, na asilimia 8.4 wana uzito kupita kiasi.

Hali si nzuri kwa siku saba ambazo utafiti ulifanyika, ukibaini asilimia 50.4 ya watoto na vijana wa umri wa miaka mitano hadi 19 waliripoti kutopata kifungua kinywa asubuhi, asilimia mbili pekee wakikiri kula nje ya nyumbani mara tatu zaidi kwa wiki na asilimia 56.6 wanakula vitafunwa kila siku.

Licha ya watoto hao kuondoka nyumbani bila kula, utafiti unaonyesha asilimia 40 ya shule ndiyo hutoa chakula kwa wanafunzi.

Hiyo ni sawa na wilaya mbili kati ya 11 ambazo ni za Kaskazini A na Kusini, huku Wilaya ya Kati ikikosa ripoti ya chakula shuleni kwa wanafunzi.

Inaonyeshwa katika ripoti hiyo kuwa, asilimia 76 ya maduka yanayozunguka mazingira ya shule, vyakula vinavyopatikana ni chipsi, soda, juisi za viwandani, keki, biskuti, piza, mihogo ya kukaanga, maembe mabichi, aiskrimu, ubuyu, koni, bazoka, karanga na vitu vingine vingi ambavyo hujulikana kama vyakula vya haraka.

Sera kuhusu lishe

Sera ya kilimo ya mwaka 2002 dhamira yake ni kuchochea maendeleo ya sekta hiyo kiuchumi na kijamii kwa mustakabali wa maendeleo ya watu na kufikia uhakika wa chakula kwa kaya na kitaifa, na kuboresha hali ya lishe ya watu, hususan kina mama wanaonyonyesha na watoto.

Pia, malengo ya Sera ya Usalama wa Chakula na  Lishe Zanzibar ya mwaka 2018 iliweka malengo matano kwenye sera ambayo ni kuimarisha upatikanaji wa chakula na kuinua uzalishaji wa ndani, na kuongeza uwezo wa kununua na upatikanaji wa chakula kwa kaya zote masikini.

Kitu kingine ni kuboresha matumizi ya chakula cha kutosha, chenye lishe bora, salama kwa wanakaya wote,

Pia, kupunguza uwezekano wa kuathiriwa na uhaba wa chakula na utapiamlo kwa makundi ya watu masikini kupitia hatua zinazowekwa za ulinzi wa kijamii, na maandalizi madhubuti ya dharura ya chakula kitaifa.


Ilani ya CCM

Sura ya nane ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 kifungu cha 182 inayozungumzia elimu ya msingi kifungu (C), chama hicho kiliahidi kuimarisha programu ya lishe katika shule za msingi zilizo katika mazingira magumu kutoka 27 mwaka 2019 hadi 50 mwaka 2025. 


Kauli ya Serikali

Akizungumzia hali hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Lishe Zanzibar, Asha Hassan Salmini anasema hatua ambazo wizara imechukua ni kuanza kukabiliana na upungufu wa damu na kuhamasisha ulaji unaostahili.

“Kwenye huo utafiti tumeona ulaji haupo vizuri, watoto wengi vyakula vyao ni vile vya wanga. Vyakula vya protini, vitamini na mbogamboga vinaliwa kwa kiwango kidogo jambo lililosababisha upungufu wa damu na ukuaji usio sahihi,” anasema.

Anaeleza Wizara ya Afya imeanzisha programu ya kuwafundisha wanafunzi shuleni jinsi ya kupika mboga za majani kwa namna isiyopoteza virutubisho na aina ya vyakula wanavyopaswa kula.

Anasema wanashirikiana na Wizara ya Kilimo kuwafundisha wanafunzi namna ya kulima bustani za mboga za majani.

“Hatua za haraka tulizochukua tumeshirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia

Watoto (Unicef) kuanzisha wiki ya madini chuma ambayo tunatoa kwa wiki mara moja,” anasema.

Anasema tayari Wizara ya Elimu imetengeneza mwongozo wa lishe shuleni, pia wanasambaza vipeperushi vinavyohusu afya.

Asha anaeleza tayari walimu wameshaelezwa hali hiyo inatokana na nini; wazazi waliitwa na kamati za shule wakapewa taarifa hiyo na hatua za kuchukua.


Wilaya zenye utapiamlo

Hali ya udumavu kwa watoto na vijana wa miaka mitano hadi 10 Mjini Kati ni asilimia 19.9, Wete asilimia 22.7, Mkoani asilimia 17.4.

Kwa watoto wenye uzito pungufu Kaskazini A ni asilimia 21.7, Kusini (15.9), Mkoani (18.5), Wete (16.9) na Chake Chake (17.2).

Kwa hali ya ukondefu, Magharibi B ni asilimia 17.8, Kusini (10.7), Wete (11.6), Mkoani (12.8) na Micheweni (10.7).

Uzito kupita kiasi, Wilaya ya Kati ni asilimia 18.8, na Magharibi B (10.8); huku upungufu wa damu, Kaskazini A ikiwa ni asilimia 53.3, Kusini (48), Kati (43.9), Mkoani (57.3), Chake Chake (48.4), na Wete (48.6).


Wilaya zinazotoa chakula

Hali ya utoaji wa chakula shuleni utafiti huo unaonyesha Wilaya ya Mkoani inatekeleza hilo kwa asilimia 25, Chake Chake (12.5), Micheweni (14.29), Wete (33.33), Magharibi B (16.67), Magharibi A (27.27).

Wilaya zingine ni Mjini kwa asilimia 10, Kusini (42.86), Kati (0), Kaskazini B (14.29), Kaskazini A na (42.86)


Wazazi na wanafunzi

Akizungumzia utaratibu wa kupata lishe, mwanafunzi wa Shule ya Firdous iliyopo kwa Kisasi, Abdul Nassor anasema wana ratiba maalumu iliyowekwa kwa ajili ya chakula kuanzia asubuhi hadi muda wa kuondoka.


Anasema asubuhi kwa kawaida hupikiwa uji na maandazi na mchana wanakula kulingana na chakula kilichopo katika ratiba.

"Ikifika mchana tunakula chakula kilichopo katika ratiba kama ni wali wa maharage, wali kunde na wali na dagaa. Samaki na nyama havipo katika ratiba yetu," anasema Abdul.

Anasema mlo ambao anautumia anapokuwa nyumbani ni wali, ugali na pilau.

Hilo ni tofauti na mwanafunzi wa Shule ya Msingi Bububu, Ali Othman ambaye anasema wao wanakula vyakula vinavyouzwa na watu nje ya shule vikiwamo bagia, kachori, mihogo na juisi.

“Siku ambayo sina pesa ya kununulia vitu hivyo inanibidi nikae na njaa hadi nirudi nyumbani ndipo nile chakula," anasema.

Kwa mujibu wa Ali, chakula anachopenda ni wali kwa sababu ndicho kinachopikwa nyumbani kwao na mara chache hula ugali.

Fatma Massoud, mkazi wa Bububu ambaye ni mzazi anasema kutokana na hali yake, hana chakula maalumu anachowaandalia watoto wake, hivyo wanachokikuta ndicho wanachokula.

“Sijaweka ratiba inategemea nimepika nini ndicho watakachokula, wakija sijapika basi watasubiri nipike,” amesema.

Mulhima Zahor, anasema kwa kawaida watoto wake hunywa chai wakiwa shuleni. Kwa upande wake, huwaandalia wali mchana na usiku huwapa matunda baada ya mlo.


Wanachosema wadau

Akizungumza na Mwananchi Digital, mtaalamu wa masuala ya afya, Dk Zakayo Mmbaga amesema utafiti huo si ishara nzuri kwa watoto na vijana wa umri wa miaka mitano hadi 19 visiwani Zanzibar.

Amesema vijana wa umri huo ndiyo kipindi ambacho lishe bora inahitajika kwa ajili ya ukuaji wa mwili na akili.

“Kinachohitajika ni kufanya utafiti mwingine kuangalia upya wale watoto waliokutwa na tatizo la upungufu wa damu wote wangefanyiwa kipimo cha selimundu kwani tatizo hili ni kubwa. Hivyo inawezekana ukawa na wenyewe unachangia kiasi kikubwa cha upungufu wa damu,” amesema.

Dk Mbaga amesema badala ya virutubishi vya madini chuma na foliki asidi kutolewa kwa wanawake pekee, itapaswa kutolewa kwa wale wa kiume pia watakaogundulika kuwa na tatizo na selimundu.

Mtaalamu na mshauri wa masuala ya afya, Festo Ngadaya amesema changamoto ya upatikanaji chakula shuleni ni la Tanzania Bara na Zanzibar ambako kwa takwimu zilizotolewa hauridhishi.

“Upatikanaji wa chakula shuleni umekuwa changamoto, hata wanavyopata haviwasaidii kwenye ukuaji wao,” amesema.

Amesema kinachoathiri utoaji wa chakula kwa wanafunzi shuleni ni dhana ya elimu bure inavyotumika, baadhi ya wazazi hujiondoa kwenye jukumu la kuchangia lishe ya watoto wao.

Ngadaya amesema watoto wengi wanashinda shule hivyo ni muhimu kuanzishwa programu maalumu za lishe shuleni.

Ameshauri shule ziwe na mradi wa shamba kwa ajili ya mahindi na bustani za mboga za majani, lakini wazazi wapewe elimu ya lishe kwa watoto haina uhusiano na ada bure.

“Watoto wakianza kulima mbogamboga wakiwa shuleni na wazazi wachangie fedha za lishe shuleni, watoto wakifika nyumbani wapate chakula na ikiwezekana Serikali ianzishe kampeni ya lishe,” amesema.

Mdau wa maendeleo, Dk Aidan Msafiri amesema akili ya mtoto inafanya kazi pale ainapopata lishe bora, hivyo kuikosa kunamdumaza kitaaluma.

“Akili haiwezi kufanya kazi kwa mtoto asiye na lishe bora, kwa hiyo hapa tunatengeneza kizazi cha watu tegemezi baadaye, hii hali si nzuri ukiona shule nyingi hazitoi chakula kwa wanafunzi maana yake kuna siasa imeingia hapo,” amesema.

“Ni muhimu wazazi waambiwe ukweli kuhusu kuchangia elimu ili waondokane na mfumo wa kukataa kuchangia eneo la chakula, kama hakutakuwa na mabadiliko tatizo la ukiukwaji wa maadili litakuwa kubwa kwa sababu watato wataingia kwenye makundi yasiyofaa kusaka mlo,” amesema.

Nyongeza na Zulekha Fatawi Zanzibar