Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utaratibu mpya ukataji leseni usafirishaji watalii, kuleta ahueni

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga akizungumza na waandishi wa habari ofisi za wizara hiyo Unguja Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Badala ya kukata leseni hiyo kila siku, kwa sasa itakatwa kuanzia miezi sita hadi mwaka mmoja huku gharama zake zikipungua kwa wastani wa Sh1.3 milioni

Unguja. Ili kupunguza gharama na kuondoa mianya ya udanganyifu katika huduma za ukodishaji wa magari ya watalii, Serikali kupitia Kamisheni ya Utalii Zanzibar imeboresha mfumo wa utoaji wa leseni, hatua ambayo imewezesha kupungua gharama kwa takriban Sh1.3 milioni kwa mwaka.

Utaratibu uliopo kwa sasa unamtaka mtu anayefanya biashara ya kusafirisha watalii kwa gari kulipia leseni ya Sh5,000 kwa siku, hali inayofanya gharama ya mwaka kufikia Sh1.8 milioni.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai mosi,2025 Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramadhan Soraga amesema utaratibu huo sio tu unaongeza wigo wa wazawa kupata fursa bali pia unasaidia kuondoa mamluki katika sekta hiyo kwani wengi walikuwa wakijificha kwenye kichaka hicho,  na kuhatarisha sekta hiyo.

Katika utaratibu huo mpya, utakaoanza Novemba mwaka huu, mtu anayetakiwa kufanya biashara ya kubeba watalii atatakiwa kukata leseni hiyo ama kwa mwezi mmoja kwa Sh100,000, miezi mitatu Sh300,000 au mwaka mmoja Sh500,000.

“Haya mabadiliko yataanza kufanya kazi Novemba mosi mwaka huu, ukiangalia gharama zimepunguzwa kwa kiasi kikubwa kwani awali ilikuwa mtu anakata leseni kwa mwaka Sh1.8 milioni,” amesema.

Pia, amesema utaratibu huo hakuwa rafiki na umelalamikiwa kwa sababu ililazimika kusimamishwa kila wakati kukagua leseni hizo, lakini baada ya kuanza kutumia leseni za miezi na mwaka watatumia mfumo maalumu.

Akizungumza hatua hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (Zati), Suleiman Ali Mohammed amesema utaratibu huo utawanufaisha wazawa zaidi, lakini utaondoa usumbufu wa kila siku kukata leseni.

“Ukiangalia gharama zimepungua kwa kiasi kikubwa, huu ni wakati sasa wazalendo kuchangamkia fursa maana zaidi ya asilimia 70 imepungua,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Soraga amezungumzia kuhusu ushindi wa Zanzibar kwenye tuzo za dunia za usafiri utalii na ukarimu (WTA) mwaka 2025, kwamba ni matokeo ya juhudi kubwa za Serikali kupitia kamisheni ya utalii na ushirikiano wa wadau wa sekta hiyo.

Hivi karibuni zilitolewa tuzo hizo jijini Dar es Salaam na Zanzibar kuibuka mshindi wa tuzo mbili kati ya tatu zilizokuwa zikishindaniwa.

 “Mara hii Zanzibar imefanikiwa kushinda maeneo yenye hadhi kama Bazaruto  Msumbiji, Cape Maclear Malawi, Cape Town Afrika Kusini, na Diana Beach Kenya, ushindi huu umeonesha wazi kwamba Zanzibar ni kisiwa kinachoongoza kwa vivutio vya fukwe barani Afrika,” amesema

Amesema tuzo hizo sio tu sifa bali ni nyenzo ya kuimarisha jina la Zanzibar kimataifa kama kivutio kinachoheshimika.

Tuzo hizi zimeanzishwa mwaka 1993 na hufanyika kila mwaka kwa ngazi ya bara na baadaye kimataifa kupitia hafla kuu ya Word Travel Award Global Ceremony.

Soraga amesema ushindi huo haujaja bure bali umetokana na jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa kuhakikisha Zanzibar inaongeza vivutio na kuongeza mikutano ya utalii.

Soraga amesema kwa mwaka 2026 tuzo hizo zinatarajiwa kufanyika Tanzania na Zanzibar kwa kushirikiana na wadau wa utalii wanaendelea kufanya jitihada kuhakikisha hafla hiyo ya heshima ya kimataifa inakwenda Zanzibar.

“Hili litakuwa jambo la kihistoria litakaloongeza thamani kubwa ya kiuchumi na kimataifa kwa visiwa vyetu,” amesema.

Meneja Mkuu wa hoteli ya Zanzibar White Sand, Valerie Mansis amesema wanajisikia faraja kubwa kuwa miongoni mwa washiriki katika tuzo hizo na zimeongeza chachu na ari ya kuendelea kuhamasisha utalii endelevu.