Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau waichambua bajeti kuu wakionesha mbivu, mbichi


Muktasari:

  • Katika uchambuzi wa wataalamu wa uchumi, fedha, biashara na kijamii, wameonesha maeneo ambayo yataimarisha uchumi na yale ambayo yangezingatiwa zaidi yangeleta tija.

Unguja. Siku moja baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kusoma bajeti kuu ya Serikali, wataalamu wa uchumi, fedha, biashara, kijamii na wananchi wa kawaida wametoa mitazamo yao kuhusu ubora na udhaifu wa bajeti hiyo.

Bajeti hiyo iliyosomwa na Waziri wa Fedha na Mipango jana Barazani, Dk Juma Malik Akil, kwa mwaka 2026/27, Serikali inatarajia kutumia Sh8.5 trilioni. Kati ya fedha hizo, Sh5.7 trilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Katika bajeti hiyo, Serikali imeonesha maeneo ya kimkakati na jinsi ambavyo bajeti hiyo inapunguza utegemezi, badala yake kuongeza mipango ya kukusanya kodi za ndani.

Katika mpango huo, Serikali inapendekeza kuongeza kodi katika nywele bandia, wigi, kucha bandia, pombe, soseji, tozo ya bandari na kuondoa tozo katika vifaa vya watu wenye ulemavu, viwanda vidogo na mafunzo ya amali.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili leo Juni 12, 2026, baadhi ya wachambuzi wa uchumi wamesema bajeti hiyo ni ya wananchi huku wengine wakionesha maeneo ambayo yalitakiwa kuwekewa mkazo zaidi.

Mtaalamu wa Uchumi na Fedha, Dk Twahir Mohamed Khalfan amesema ni mwendelezo wa bajeti ambapo kuna sekta za kipaumbele ambazo zimezingatiwa ikiwemo ujenzi, miundombinu ya barabara, masoko na bandari.

“Bajeti ukiiangalia kwa ujumla kuna maendeleo yake, licha ya upungufu unaoonekana lakini kwa uhakika imeongeza mahitaji kulingana na mazingira ya Zanzibar tuliyonayo,” amesema.

Hata hivyo, Dk Twahir ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kijamii, Kiuchumi na Uchambuzi wa Sera Zanzibar (ZRCP), amesema katika bajeti hiyo Serikali imetenga fungu la zaidi ya Sh200 bilioni ambazo zitakwenda kusaidia mashirika ya Serikali kupata mitaji.

Hata hivyo, amesema licha ya mpango huo mzuri bado kuna hatari iwapo kampuni hizo hazitazalisha na kufikia malengo ya Serikali; itakuwa ni hasara. Badala yake, fedha hizo zingetumika katika kuimarisha mazingira ya biashara na kukuza sekta binafsi.

“Hii ni nzuri, lakini iwapo hazitazalisha itakuwa ni hasara, kwa hiyo ingetumia fedha hizi katika kuimarisha mazingira ya biashara na kukuza sekta binafsi ambazo zina mchango wa moja kwa moja katika uchumi wa taifa badala ya kupeleka fedha hizi katika kampuni ambazo pengine hazitaleta faida,” amesema.

Kadhalika, mtaalamu huyo wa uchumi amesema licha ya kujipambanua katika maendeleo ya uchumi wa kidijitali, lakini katika bajeti hiyo haijaonesha kwa namna gani inaweza kushughulikia eneo hilo, hivyo bado kuna haja ya kuhakikisha linapata nguvu kubwa.

Pia, amesema bado kuna gharama kubwa katika malipo ya kidijitali jambo ambalo nalo linatakiwa kushughulikiwa.

“Kuna jambo pia limezungumzwa kwenye mijadala kwa wawakilishi kuhusu gharama za intaneti kuwa juu, bado hatukuona mkakati mahususi wa kuhakikisha gharama za intaneti zinapungua, kwa hiyo tunapotaka kukuza uchumi wa kidijitali haya yote yanatakiwa kuangaliwa,” amesema.

Amesema kwa mwananchi wa kawaida ni ngumu kumudu gharama ya Sh120,000 kuunganishiwa intaneti nyumbani.

Hata hivyo, amesema juhudi kubwa zimefanyika kwani kwa miaka minne bajeti inaongezeka, jambo ambalo ni la kupongeza.

“Ukiiangalia imetoka asilimia 20 katika bajeti kwenda miradi ya maendeleo mpaka asilimia 70, hii ni hatua kubwa kwa kipindi cha miaka minne, ila ipo haja sasa katika uhalisia wa utekelezaji unakuta inakuwa asilimia 50 kwa 50, kwa hiyo tunataka kuona angalau katika utekelezaji inafikiwa kweli asilimia hiyo 70,” amesema mtaalamu huyo.

Kwa hiyo, mtaalamu huyo wa fedha na uchumi amependekeza kupunguza matumizi makubwa ya Serikali ili kuhakikisha fedha zinazopatikana zinajikita kwenye miradi badala ya kufanya kazi ambazo wakati mwingine zinaongeza gharama kubwa serikalini.

Mtaalamu mwingine wa uchumi na fedha, Dk Khalfan Suleiman amesema ni bajeti ya wananchi kwani Serikali kuchukua hatua ya kuongeza gharama kwenye vifaa ambavyo si muhimu kwa wananchi wa kawaida ni jambo la kimkakati.

Amesema Serikali imekuja na ubunifu mzuri kwa kuangalia maeneo ambayo ni ya kistarehe zaidi na si kwa mwananchi wa kawaida.

“Kwa hiyo mimi ningeshangaa sana kama wangeongeza bei kwa vifaa vya kilimo na elimu, lakini nywele bandia, kucha na vitu vingine kama hivyo, athari yake haipo kabisa kwa mwananchi wa kawaida,” amesema.

Dk Khalfan amesema kwa jinsi ilivyo, umefanyika utafiti wa kutosha na kuangalia maeneo ambayo hayaumizi wananchi wengi.

Hata hivyo, mtaalamu huyo amesema kuandaa bajeti ni jambo moja na utekelezaji wake ni suala lingine, kwa hiyo amependekeza itekelezwe kikamilifu ili kuhakikisha malengo yote yaliyokusudiwa yanafikiwa.

Amesema bajeti hiyo imejikita katika miradi ya kimkakati ambayo ikitekelezwa italeta tija kwa kuongeza ajira na mapato ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Naona tunaelekea pazuri; ni bajeti endelevu na haitegemei watu wengine, badala yake imejikita katika vyanzo vya ndani,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Zanlink, Sanjay Raja amesema kuweka kodi ya matumizi maalumu ya asilimia 17 ya intaneti ni kuifanya ionekane haramu ilhali kila kitu kwa sasa kinahitaji huduma hiyo.

Amesema Serikali imetunga sera mbili zinazokinzana; sera ya kusambaza mabadiliko ya kidijitali na sera inayoweka kodi ya matumizi maalumu ya intaneti.

“Hizi ni sera mbili zinapingana, wakati wanataka kusambaza mabadiliko ya kidijitali. Hiyo ni sera. Na kisha kuna sera inayosema tunaweka kodi ya matumizi maalumu ya asilimia 17. Haziwezi kwenda pamoja,” amesema Sanjay.

Amesema katika dunia ya sasa hakuna sekta isiyohitaji intaneti; iwe sekta binafsi, ya umma au mtu mmoja mmoja.

Nao baadhi ya wananchi, licha ya kupongeza bajeti hiyo kwa kugusa kodi ambazo haziwalengi wananchi wa hali ya chini, wamesema bado kuna changamoto ya kupanda gharama za maisha hivyo wakaitaka Serikali kupunguza gharama hizo.

Mkazi wa Magomeni, Ashura Haji Musa amesema mara nyingi wamezoea kuona kodi zinaongezwa kwenye bidhaa zinazowagusa moja kwa moja wananchi, lakini safari hii maeneo mengi yaliyoongezwa kodi si muhimu kwa kila mwananchi.

“Hizo nywele bandia, kucha na kope si watu wote wanaotumia urembo huo, kwa hiyo wengi wanatumia kwa ajili ya urembo na si kwa matumizi muhimu,” amesema.

Hata hivyo, amesema licha ya kuona mwanga katika bajeti hiyo, Serikali inatakiwa kuongeza jitihada kwenye makusanyo kwani kuna fedha nyingi zinapotea mikononi mwa watu, kwa hiyo wanatakiwa kuweka mifumo imara ya kuimarisha makusanyo.

Mwananchi mwingine, Haji Ali Ali amesema pamoja na mambo mengi yaliyomo ndani ya bajeti, lakini suala la kupanda gharama za maisha bado linawatesa wananchi wengi.

“Kwa hiyo tulitegemea kuona namna gani Serikali inashughulikia changamoto hii hususan kupanda bei za vyakula, mafuta na bidhaa zingine, kwa hiyo tulitaka kuona mkakati maalumu wa kumpunguzia mwananchi asiye na uwezo gharama hizi za maisha ambazo zinawatesa wengi,” amesema.