Wawili wafariki kwa kufukiwa na kifusi wakichimba mawe Pemba

Muktasari:
- Hili ni tukio la pili kutokea kwa mwaka huu katika machimbo hayo.
Pemba. Huzuni na majonzi vimetawala kwa familia ya Mzee Ali Shoka na wakaazi wa Mjini Wingwi Wilaya ya Micheweni baada watu wawili wa familia moja kufariki dunia kwa kufunikwa na kifusi.
Katika tukio hilo lililotokea jioni ya Juni 29, 2025 waliopoteza maisha ni Hamad Juma Makame (64) na Shaame Hamad Shoka (34) na wengine wawili kuokolewa wakiwa salama.
Wakizungumza na Mwananchi baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamesema walikuwa wanne ila wawili wameokolewa wakiwa salama.
Simai Khamis Sharifu amesema baada ya kupata taarifa ya wananchi kuangukiwa na mawe na kufunikwa na kifusi waliamua kufika kwenye eneo hilo kuwaokoa.
Amesema wananchi walijitokeza kuwaokoa ambapo wawili walitoka wakiwa salama, ila wengine wawili waliwahishwa Hospitali ya Wilaya ya Micheweni kwa uchunguzi lakini, walikuwa wameshafariki dunia.
“Tulipopata taarifa hiyo tulikuja eneo la tukio tulikuta tayari watu wengine wameanza harakati za uokoaji tukajiunga nao,”amesema.
Shoka Salim Hassan Mkaazi wa Maziwang’ombe alitoa wito kwa wachimbaji wa mawe kuchukua tahadhari kwani yanaweza kukatika na kuleta athari kwao.
Hata hivyo, ameomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuhamasisha upandaji miti kwa zile sehemu ambazo zimeshakuwa na mashimo kutokana na uchimbaji wa mawe.
“Niwaombe wananchi wenzangu tuwe na tahadhari katika uchimbaji mawe mengine yanakuwa yamejiegesha tu ukiyagusa yanameguka na kuanguka na kuleta athari kama hizi,” amesema Shoka.
Daktari wa zamu wa Hospitali ya Wilaya ya Micheweni, Hamad Abdalla Rashid alisema alipokea wawili kutoka katika tukio hilo, lakini baada ya kuwafanyia uchunguzi wa awali walibaini kuwa wameshaaga dunia.
Amesema walipowafanyia uchunguzi walibaini kuwa walipata majeraha katika sehemu za kifua na ndio sababu ya kifo chao. “Tumeshaikabidhi miili hiyo kwa familia zao kwa ajili ya taratibu za mazishi.”
Mmoja wa wanafamilia ya marehemu hao, Mzee Ali Shoka amesema waliofariki ni mtu na shemeji yake waliondoka mapema asubuhi kwa ajili ya kwenda kazini lakini ghafla waliletewa taarifa kuwa wamefariki kwa kuangukiwa na mawe na kifusi.
Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Khatib Juma Mjaja amesema Serikali inaangalia njia sahihi ya kufanya kazi katika maeneo hayo bila kuleta madhara.
Amesema hilo ni tukio la pili kutokea katika mwaka huu ambapo la kwanza lilitokea Januari 25, 2025 kwenye machimbo hayo kwa kumpoteza msichana akiwa kwenye harakati hizo.
“Kama Serikali tunaangalia njia sahihi ikiwezekana kubadilisha matumizi kuona matukio kama hayo hayajirejei maana Januari 25 mwaka huu alifariki msichana wakati akiwa katika harakati za uchimbaji wa mawe kwenye maeneo hayo,” amesema Mjaja.