Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wizara ya Mawasiliano yawekeza katika usalama wa mtandao kuziba mianya ya wahalifu

Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Fatma Mabrouk Khamis (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Serensic Afrika, Esther Mengi (kushoto) wakisaini hati ya makubaliano ya ushirikiano. Picha na Zuleikha Fatawi

Muktasari:

  • Hati hiyo ya makubaliano inalenga kuimarisha uwezo wa wataalamu wa usalama wa mtandao, kuongeza uelewa wa watumishi na viongozi, kukuza matumizi salama ya teknolojia na kuimarisha ushirikiano wa kukabiliana na uhalifu wa kidijitali.

Unguja. Licha ya dunia kushuhudia mageuzi makubwa ya kidijitali, bado kuna changamoto zinazoongezeka za kiusalama zinazotokana na matumizi ya mifumo ya kidijitali.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi, Juni 11, 2026 na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mohamed Sijamini, kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo, Mudrick Ramadhan Soraga, katika hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano kati ya Wizara hiyo na Kampuni ya Serensic Afrika.

Sijamini amesema changamoto nyingi za kiusalama zinatokana na ukosefu wa uelewa wa watumiaji, ikiwemo kupokea barua pepe za ulaghai, kufungua viunganishi hatarishi, matumizi ya nywila dhaifu na kutofuata taratibu za usalama wa mtandao.

Amesema mianya hiyo ndiyo inayotumiwa na wahalifu wa mtandao kufanya mashambulizi dhidi ya wananchi, ambao mara nyingi huwa waathirika wakuu wa uhalifu huo.

Kwa mujibu wa Soraga, mashambulizi ya mtandao yakiwemo wizi wa taarifa, udanganyifu wa kidijitali, uharibifu wa mifumo na vitendo vingine vya uhalifu wa kimtandao vinaendelea kuongezeka, hivyo vinapaswa kudhibitiwa kwa kiwango kikubwa iwezekanavyo.

"Maendeleo ya teknolojia lazima yaende sambamba na uwekezaji katika usalama wa mtandao," amesema Soraga.

Amesema hati hiyo ya makubaliano inalenga kuongeza uwezo wa kitaalamu kwa watendaji wa wizara na taasisi zake katika masuala ya usalama wa mtandao.

Pia, itasaidia kuimarisha uelewa wa viongozi na watumishi kuhusu hatari zinazoweza kuathiri mifumo ya kidijitali na namna ya kuzidhibiti, pamoja na kukuza matumizi ya teknolojia salama katika utoaji wa huduma za Serikali na shughuli za maendeleo.

Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Fatma Mabrouk Khamis (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Serensic Afrika, Esther Mengi (kushoto) wakipeana mikono baada ya kumaliza kusaini hati ya makubaliano ya ushirikiano. Picha na Zuleikha Fatawi

Aidha, amesema makubaliano hayo yataimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika kukabiliana na changamoto za kiusalama zinazojitokeza katika ulimwengu wa kidijitali, pamoja na kujenga utamaduni wa usalama wa taarifa ili kuhakikisha taarifa za serikali na za wananchi zinalindwa ipasavyo.

Vilevile, amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya sekta ya Tehama kupitia sera, sheria na mikakati inayolenga kuharakisha mageuzi ya kidijitali nchini.

Amesema katika kufanikisha hilo, wizara inaendelea kuimarisha usalama wa mtandao na ulinzi wa taarifa kwa kuchukua hatua mbalimbali za kimkakati, ikiwemo kuimarisha mfumo wa kisheria na kiutawala unaosimamia matumizi salama ya teknolojia za habari na mawasiliano.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Serensic, Esther Mengi, ameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuandaa mfumo mmoja wa kitaifa utakaotoa mwongozo kwa watumiaji wa teknolojia kutokana na ongezeko la matumizi ya mifumo ya kidijitali.

Amesema Serikali nyingi barani Afrika zinatumia teknolojia kukuza uchumi, kuboresha miundombinu ya umma na kuongeza ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli za maendeleo.

Naye, Mkurugenzi wa Usalama wa Mtandao na Ulinzi wa Taarifa Zanzibar, Khalfan Mohamed Othman, amesema bado wizara hiyo inahitaji wataalamu zaidi wa masuala ya usalama wa mtandao ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi salama ya teknolojia na kujikinga dhidi ya uhalifu wa kimtandao.