Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zanzibar ilivyopanga kukuza uwezo wa watu, kuimarisha uchumi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya

Muktasari:

  • Mpango huo umetaja maneno matano ya kimkakati na miradi ya maendeleo ambayo itagharimu Sh3.2 trilioni.

Unguja. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya ametaja maeneo matano ya kimkakati kwa mwaka wa fedha 2025/26 yakigusia kukuza uwezo wa watu, kuimarisha mageuzi ya kiuchumi na mazingira wezeshi.

Maeneo mengine ni kutumia fursa za uchumi wa buluu, kukuza rasilimali watu na huduma za kijamii nakuimarisha utawala na uhimili.

Akisoma hotuba ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2025/26 Waziri Saada amesema jumla ya Sh3.292 trilioni zinatarajiwa kutumika kugharamia programu na miradi ya maendeleo ya kimkakati sawa na ongezeko la asilimia 57.77 ikilinganishwa na Sh2.086 trilioni za bajeti ya maendeleo ya mwaka 2024/25.


Kukuza uwezo wa watu na maendeleo ya jamii

Waziri Dk Saada amesema katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma za kijamii Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu na rasilimali watu sambamba na utoaji wa huduma zenye viwango.

“Katika kufanikisha hilo, Serikali inakusudia kuanza ujenzi na ukarabati mkubwa wa hospitali ya rufaa ya Mnazi Mmoja, ujenzi wa hospitali ya Binguni ambayo itakua ni Taasisi ya tiba, tafiti na kufundishia na Ujenzi wa nyumba za bei nafuu katika maeneo ya Chumbuni, Kisakasaka, Nyamanzi, Kwahani, Mfikiwa, Mkungu Malofa na Saateni,” amesema.

Kwa upande wa sekta ya elimu, Serikali inaendelea na ujenzi wa madarasa 1,000, utanuzi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) pamoja ujenzi wa mabweni ambapo jumla ya Sh1.260 trilioni zinatarajiwa kutekelezwa. Pia inakusudia kujenga kiwanja kipya cha michezo, Fumba na viwanja vya michezo vya wilaya.


Kuimarisha mageuzi ya kiuchumi

Waziri Saada amesema Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu katika maeneo tengefu ya viwanda, biashara ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Vilevile, kuendeleza shughuli za uzalishaji wa mazao ya kilimo kupitia uendelezaji wa miundombinu ya uzalishaji na uhifadhi wa chakula, kushajiisha kilimo cha mazao mbadala ikiwemo viungo kwa ajili ya usafirishaji na kuanza utekelezaji wa mageuzi ya kilimo ili kukuza uzalishaji huku ikidhamiria kuendelea kuimarisha miundombinu ya uchumi wa kidijitali kwa kulaza mkonga wa Kimataifa wa Baharini Zanzibar na ujenzi wa Kituo cha kuhifadhia taarifa. Ambapo eneo hili limetengewa Sh148.91 bilioni.


Mazingira wezeshi na kuimarisha miundombinu

Amesema Serikali itaendelea na uimarishaji wa miundombinu ya usafiri wa anga ikiwemo ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Pemba, ujenzi wa jengo la abiria la Pili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amaan Karume pamoja na kuanza ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Nungwi.

Vilevile, kuendelea na ujenzi wa barabara kuu Unguja na Pemba zenye urefu wa kilomita 782.9 zikiwemo za mjini, vijijini za ndani na zile zinazounganisha hoteli pamoja na ujenzi wa mitaro na matengenezo ya maziwa katika maeneo ya miji.

Waziri amesema kupitia programu hiyo kutakuwa na uendelezaji wa kazi za ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji, na umeme na upatikanaji wa umeme wa jua ambapo zitatumika Sh1.201 trilioni katika kutekeleza miradi hiyo.


Kutumia fursa za uchumi wa buluu

Amesema Serikali itaendelea na utekelezaji wa sera na mikakati ya kuendeleza sekta ya uchumi wabuluu kwa ujenzi wa miundombinu ya viwanda vya usarifu wa mazao ya baharini pamoja na utalii wa bahari na visiwa.

Kwa mwaka 2025/2026, kiasi cha Sh428.09 bilioni zinatarajiwa kutumika kwa kugharamia ujenzi wa miundombinu ya uvuvi na ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani, Mpigaduri na bandari ya uvuvi Shumba.


Kuimarisha utawala bora na uhimilivu

Akiendelea na hotuba yake Waziri amesema Serikali itaimarisha ulinzi na usalama pamoja na kuimarisha upatikanaji wa haki ili kuhakikisha nchi inaendelea kubaki katika hali ya utulivu na amani sambamba na uhifadhi wa Zanzibar kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Katika eneo hili miradi itakayotekelezwa ni kuimarisha ulinzi na usalama, Ujenzi wa Mahakama za Wilaya na Mikoa na uhifadhi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi ambapo itatumika Sh253.65 bilioni.

“Kwa mwaka wa fedha 2025/26 Serikali inatarajia kutekeleza miradi mengine ambayo itagharimu Sh1.247 trilioni. Miradi hii inajumuisha  inayoendelea, yenye dhima ya fedha za Serikali kwa washirika wa maendeleo na upelekaji wa miundombinu katika maeneo yanayotarajiwa kutekelezwa miradi ya kimkakati,” amesema

Akitaja mwelekeo wa hali ya uchumi kwa mwaka 2025 malengo na shabaha za uchumi jumuishi kwa mwaka 2025, Dk Saada amesema;

“Uchumi wa Zanzibar unakadiriwa kukua kwa wastani wa asilimia 7.3 kutoka wastani wa asilimia 7.1 mwaka 2024 kwa kufikia malengo yafuatayo,  kuongezeka kwa uingiaji wa watalii watakaotembelea Zanzibar kwa asilimia 12.6 kutoka watalii 736,755 kwa mwaka 2024 hadi 829,929 mwaka 2025.

Amesema wataendelea na hatua za kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei ili kubakia katika tarakimu moja, kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuongeza thamani na miradi ya uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi

Ameitaja sekta binafsi kuongeza mchango wake kutokana na juhudi za Serikali za kukuza uwekezaji, uwezeshaji wananchi kiuchumi na kuongeza ajira.

“Kuongezeka kwa uzalishaji katika sekta ya uchumi wa buluu na kuimarisha matumizi endelevu ya bahari baada ya kukamilika kwa ujenzi wa viwanda vya uchakataji na usarifu wa mazao ya baharini.”

Pia Waziri Saada amesema wamedhibiti mfumuko wa bei kubaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya kiwango cha asilimia tano kama ilivyo shabaha iliyowekwa kwa nchi za Afrika Mashariki.