Zanzibar kuwakutanisha wadau kujadili Kiswahili

Katibu Mkuu Wizara, Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fatma Hamad Rajab akizungumza na waandishi wa habari kuhusu siku ya kiswahili wizarani hapo Junguja. Picha na Jesse Mikofu
Muktasari:
- Novemba 23, 2021, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) lilitangaza na kukiwekea Kiswahili siku yake maalumu ya maadhimisho ambayo ni Julai 7 kila mwaka.
Unguja. Wakati Julai saba ikitarajiwa kufanyika maadhimisho ya Kiswahili duniani, Zanzibar imejipanga kuadhimisha siku hiyo kuanzia Julai 5, kwa kufanya shughuli mbalimbali zinazohusiana na Kiswahili ambapo wadau na wananchi wameitwa kushiriki, ili kupata taaluma ya lugha hiyo.
Novemba 23, 2021, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) lilitangaza na kukiwekea Kiswahili siku yake maalumu ya maadhimisho ambayo ni Julai 7 ya kila mwaka.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 2, 2025 Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Fatma Hamad Rajab amesema watafanya shughuli zinazohusiana na lugha na utamaduni wa Mswahili katika maeneo mbalimbali.
“Siku zote nne kutakuwa na shughuli za sanaa, utamaduni, taaluma na matembezi ya kiafya ambapo watajumuika pamoja na watoto wetu ili kukuza utamaduni na mshikamano katika jamii zetu,” amesema
Amesema Julai 5 itakuwa jukwaa la mwanamke hazina ambapo kutakuwa na uwasilishaji wa makala inayohusu mwanamke na utawala bora.
Amesema Julai 6 kutakuwa na matembezi ya wanafunzi na wadau wa Kiswahili kisha uwasilishaji wa makala inayohusu umuhimu wa usomaji wa vitabu.
Katika shughuli hiyo pia kutatolewa tuzo kwa washindi wa mashindano ya insha kwa shule za sekondari mwaka 2025 na wanafunzi bora wa Kiswahili mwaka 2024.
Katika siku ya kilele ya Julai 7, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi itawakutanisha watu mbalimbali kujadili Kiswahili.
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (Bakiza), Dk Mwanahija Ali Juma amesema mpaka sasa watu 430 tayari wameshajisajili kushirikia maadhimisho hayo kutoka ndani na nje ya nchi.
“Pia, ubalozi wa Urusi wamethibitisha kushiriki kwenye siku ya kilele, tunategemea watu wataongezeka zaidi kwani, bado wanaendelea kujisajili.”