Zanzibar yaahidi kuendeleza ushirikiano na China

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na idara maalumu za (SMZ) Masoud Mohamed Akizungumza na ugeni kutoka China waliomtembelea ofisini kwake Vuga mjini Unguja. Picha na Muhammed Khamis

Muktasari:

  • Amesema ushirikiano kati ya China na Zanzibar utaendelea kuimarishwa kwa maslahi ya nchi zote mbili.

Unguja. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Mohamed ameahidi kudumisha ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kukuza uchumi wa nchi.

Ameyasema hayo leo Novemba 17 wakati Akizungumza na Naibu eya wa manispaa ya Jiji la Chong Qing kutoka China aliefika huko Ofisini kwake Vuga mjini Unguja.

Amesema ugeni huo una lengo la kuzisaidia manispaa katika kubadilishana uzoefu wa kiutendaji kazi ili kuhakikisha jiji la Zanzibar kuwa na mazingira mazuri.  

Aidha ameleza kufurahishwa kwake na ujio huo pamoja na kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Zanzibar katika kuleta maendeleo nchini.


Naibu Meya wa Manispaa ya Jiji la Chong Qing Hon. Shang Kiu ameahidi kuwa ushirikiano huo utakuwa endelevu ili kuleta manufaa katika nchi zote mbili.

Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar, Mahmoud Mohamed Mussa amesema ugeni huo una nia dhabiti ya kushirikiana na kusaidiana kwa pamoja ili kupendezesha Mji wa Zanzibar.

Aidha, amesema katika kupendezesha Mji wa Zanzibar kuwa safi kunahitajika kupata Miundombinu itakayoweza kusaidia kuimarisha Nchi.

Ugeni huo ulikuwa nchini kwa siku mbili na ulitembelea maeneo mbali mbali kwa ajili ya kuangalia mazingira ya Mji na Utalii uliopo Zanzibar.