ZRA yaanza hamasa ulipaji kodi kwa hiari kukusanya Sh845 bilioni
Muktasari:
- Kaimu Kamishna Mkuu wa ZRA, Said Ali Mohamed amefanya ziara kwa walipakodi kwa nyakati tofauti katika mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja
Unguja. Wakati Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) ikipanga kukusanya Sh845 bilioni mwaka wa fedha 2024/25, imeanza kuwatembelea walipakodi, kusikiliza changamoto zao na kuwakumbusha kuendelea kulipa kodi kwa hiari ili kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora.
Kaimu Kamishna Mkuu wa ZRA, Said Ali Mohamed amefanya ziara katika maeneo mbalimbali ya walipakodi kwa nyakati tofauti katika mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja.
“Tumekutana na walipakodi mbalimbali na kuwataka watimize wajibu wao, kuona kwamba Serikali inapata haki yake na iweze kutoa huduma bora kwao na wananchi kwa jumla,” amesema Said.
Akiambatana na viongozi mbalimbali wa ZRA, Said amefafanua lengo la ziara yake kwa kundi hilo ni kuwasikiliza na kubaini changamoto zinazowakabili walipakodi ili wazipatie ufumbuzi.
Amewahakikishia walipakodi hao changamoto walizozitoa, ZRA imezipokea na iko tayari kuzifanyia kazi kwa lengo la kuimarisha huduma bora.
Sambamba na hayo amesema ZRA haitasita kuwachukulia hatua wale wote watakaokwenda kinyume na sheria na kuikosesha Serikali mapato ambayo ni nyenzo muhimu katika ujenzi wa Zanzibar yenye kupiga hatua za kimaendeleo katika sekta mbalimbali.
Kwa upande wao walipakodi, licha ya kupongeza hatua hiyo ya kutembelewa katika maeneo ya kazi kujua wanavyofanya biashara zao, wamesema zile changamoto zinazojitokeza ZRA iendelee kuzifanyia kazi na kuleta ufanisi zaidi.
“Tumefurahi sana kutembelewa, tunaipongeza ZRA kwa namna inavyotuhudumia vizuri walipakodi,” amesema Meneja wa Hoteli ya Essque Zalu Zanzibar, Fatma Al Sinawi.
Mdhibiti wa Fedha kutoka Hoteli ya The Residence, Jimmy Mbute amesema wataendelea kuwa walipakodi wazuri kwa maendeleo ya Zanzibar.
Mdhibiti wa Fedha kutoka Z Hotel Zanzibar, Raju Poudel amesema mfumo wa Zidras umerahisisha kazi ya ulipaji kodi hasa katika ujazaji na kuwasilisha ritani kwa njia ya kidijitali.
Jumla ya hoteli 11 kutoka Mkoa wa Kaskazini na Kusini Unguja zilitembelewa na mamlaka hiyo.