Nafasi ya Mama Fatma Karume katika kufanikisha Mapinduzi ya Zanzibar

Muktasari:

Mbali na kumsaidia mumewe, Fatma alikuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya mumewe hadi kuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar

Watetezi wa masuala ya jinsia wana msemo wao kuwa kila mwanaume mwenye mafanikio nyuma yake kuna mwanamke. Hii ni dhana halisi ambayo na si rahisi kuiona isipokua wenye uelewa na kuona mbali. Dhana hii inatukumbusha tusiwadharau wanawake pale inapotokea tumepata mafanikio na tunapaswa kutambua kuwa mwanamke ni sehemu ya ushujaa wetu.

Leo tukiwa tunaadhimisha miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoasisiwa na Mzee Abeid Amani Karume ipo haja pia kukumbuka na kutambua mchango wa mama aliy-emtunza na kumtia moyo, kabla na baada ya mapinduzi hayo. Mama huyo ni Fatma Gulam Hussein, wengi kwa sasa humuita Fatma Karume ambaye alianzisha uhusiano wa ndoa na Mzee Karume Novemba 1944.

Fatma alizaliwa Bumbwini Mkoa wa Kaskazini Unguja mwaka 1929 akiwa ni mtoto wa Gulam Hussein na Mwanasha Mbwana Ramadhani. Alipata elimu yake ya msingi katika shule ya kijijini kwao Bumbwini na mara baada ya kumaliza elimu yake ya msingi ndipo alipofunga ndoa na Karume. Mara baada ya ndoa ya wawili hao kufungwa walihamia mtaa wa Kisima Majongoo katika nyumba iliyokuwa na namba 18/22.

Fatma alipata mtoto wa kwanza na waliyedhamiria kupewa jina la Asha katika mwaka 1946 lakini kwa bahati mbaya mtoto huyo alifariki siku ya pili yake mara tu baada ya kuzaliwa. Mtoto wa pili alikuwa ni Amani Abeid Karume (Rais mstaafu wa Zanzibar) aliyezaliwa Novemba 1, 1948 na mtoto wake watatu alikuwa ni Ali Abeid Karume (Waziri wa vijana, utamaduni, sanaa na michezo ) aliyezaliwa mwaka 1950.

Mbali na kumsaidia mumewe, Fatma alikuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya mumewe hadi kuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar. Katika mahojiano aliyofanya na gazeti hili mwaka jana, Mama Karume anasema mume wake alinuia kuona Wazanzibari wanapata haki yao ya kujitawala wenyewe. Anasema kuna wakati hakuwa akiamini kwamba ndoto hizo zinaweza kutimia na aliwahi hadi kukata tamaa, lakini aliamini inaweza kuwa kweli, ndio maana hakutaka kumvunja moyo mumewe.

“Hatimaye Mwenyezi Mungu alimpa nguvu zaidi Mzee Karume na wenzake wakaamua kufanya mapin-duzi ambayo yamewafanya Wazanzibar leo hii kuwa huru lakini pia kuwaunganisha Watanzania wote kuwa kitu kimoja,” anas-ema. Anasema muda wote marehemu mume wake alikuwa anawaza jinsi ya Wazanzibari wangepataje haki ya kujiongoza na kujiamulia wenyewe mambo yao.

Anasema si kwamba Mzee Karume alipenda sana uongozi bali alikuwa na mapenzi ya kuona wananchi wa visiwa hivi wanabaki kuwa huru bila ya utumwa ambao ulitawala kwa kiasi kikubwa na kuwafanya wazawa wa visiwa hivi kubaki watumwa ndani ya nchi yao. Fatma anasimulia hata hapo awali, Mzee Karume aliwahi kukataa wadhifa wa Mwenyekiti wa Chama cha Afro-Shirazi lakini kutokana na kulazimishwa na wajumbe wa mkutano huo na kushauriwa pia na Mwalimu Julius Nyerere ilimlazimu kukubali kwa sababu wote walikuwa na dhamira ya kusaka uhuru.

“Hatukulala usiku mzima mpaka alfajiri Mzee alipokuja kunisimulia kuwa ametakiwa kuwa mwenyekiti wa Afro-Shiraz, sote wawili tuliona amepewa mzigo mkubwa ambao asingeuweza,” aliongezea Fatma. Fatma anasema waliona wadhifa huo ni mkubwa kwao kwa sababu ya kipindi wenyewe tayari walishakuwa na watoto wawili ambao nao walikuwa wadogo sana huku akifahamu kuwa mume wake anakwenda kubeba jukumu kubwa zaidi la mapambano ya kusaka uhuru.

Anasema mumewe aliwaza sana watoto wake na mke wake zaidi katika kipindi hicho, ukizingatiwa kuwa walikuwapo baadhi ya watu ambao hawakutamani kufanyika kwa mapinduzi. Hata hivyo anasema alilazimika kumpa moyo muda wote huku akiamini kwamba siku moja itakuwa kweli na Wazanzibari wan-getoka kwenye makucha ya wakoloni na kubaki kuwa watu huru kwenye nchi huru.

Anasema bila kumtia moyo Karume, haamini kama mapinduzi yangekuja kwa haraka kiasi kile. Fatma anasema hata baada ya kufanikiwa kwa mapinduzi hayo, Mzee Karume hakuwa kuwa na amani kwa sababu wapo baadhi ya watu ambao hawakuyataka wala kuyapenda. Alisema kutokana na hofu hiyo Mzee Karume aliamua kuiunganisha Zanzibar na Tanganyika hatimaye kuzaliwa kwa Tanzania kupitia muungano ambao hadi leo hii walio wengi wanajivunia. Alisema bila shaka ipo haja ya kutunzwa na kuen-ziwa kwa Mapinduzi lakini pia watu wanapaswa kufahamu kuwa kufanyika kwa mapinduzi ya Zanzibar ni sababu pia iliyopelekea kuzaliwa kwa Taifa jipya la Tanzania ambalo leo hii kila mmoja anajivunia.