TCRA: Huduma za posta zikitumika vizuri ni sehemu ya maisha ya mwananchi


TCRA: Huduma za posta zikitumika vizuri ni sehemu ya maisha ya mwananchi

Umoja wa Posta wa Afrika (Pan African Postal Union, PAPU) ulianzishwa mwaka 1980 ikiwa ni chombo au taasisi maalumu ‘Specialized Agency’ ya Umoja wa Afrika (AU) yenye jukumu la kuendeleza sekta ya huduma za Posta barani Afrika na Makao yake Makuu yakawa Jijini Arusha.

 Licha ya sekta ya Posta kuwa ni moja ya sekta yenye mtandao mkubwa ulimwenguni ambao ni muhimu kwa maisha ya jamii, kwa miaka ya karibuni sekta hiyo imepata changamoto kutokana na mabadiliko ya teknolojia.

Umoja wa Posta wa Afrika (PAPU) ni miongoni mwa vyombo muhimu katika kusimamia sekta ya posta barani Afrika. PAPU imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha huduma za posta zinaendelea kuwa mhimili mkubwa katika jamii.

Wakati inapotimiza miaka 40 tangu kuanzishwa kwake, sekta ya posta katika nchi mbalimbali barani Afrika ikiwemo Tanzania hazina budi kutambua mchango uliotukuka wa Umoja huo katika kukuza sekta ya Posta Afrika.

Ikumbukwe kuwa Tanzania imechangia kwa kiasi kikubwa kwa kuanzishwa kwa PAPU kupitia kwa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alijitolea kwa moyo mmoja kwa mkutano wa posta kufanyika katika ardhi ya Tanzania ikiwa ni sehemu ya kuthamini maendeleo ya pamoja ya Afrika.

Pia, Serikali ya awamu ya tano kupitia kwa Rais, Dk. John Pombe Joseph Magufuli imeendelea pale alipoishia mwasisi wetu na kutoa eneo la kujenga makao makuu ya Umoja wa Posta wa Afrika (PAPU) nchini.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ikiwa ni mdau wa sekta ya posta hapa nchini, inatambua umuhimu wa PAPU katika kukuza na kuendeleza sekta ya huduma za Posta barani Afrika na kwenye mahojiano haya wanaeleza mambo mbalimbali kuhusu umoja huo wenye makao yake makuu jijini Arusha nchini.

TCRA inazungumziaje miaka 40 ya kuanzishwa PAPU?

Umoja wa Posta wa Afrika (Pan African Postal Union, PAPU) ulianzishwa mwaka 1980 ikiwa ni chombo au taasisi maalumu ‘Specialized Agency’ ya Umoja wa Afrika (AU) yenye jukumu la kuendeleza sekta ya huduma za Posta barani Afrika na Makao yake Makuu yakawa Jijini Arusha.

Serikali yetu ya awamu ya kwanza chini ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilitoa kiwanja kwa ajili ya kujengwa Makao Makuu ya PAPU.

Majukumu makuu ya PAPU

  1. Kuwezesha Sekta ya Posta iwe yenye umuhimu katika kujenga uchumi wa kidijitali,
  2. (ii) Kuhamasisha viongozi wa nchi za Afrika kuipa kipaumbele sekta ya posta katika mipango yao ya maendeleo,
  3. (iii) Kuunga mkono maendeleo ya utoaji wa huduma za umma kikanda na
  4. (iv) Kuimarisha sauti ya Afrika katika majadiliano ya kiposta ya kimataifa. TCRA inaipongeza PAPU kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya kwa bara letu la Afrika hususani katika kuboresha na kuimarisha usambazaji wa barua, vifurushi pamoja na vipeto huku wakizingatia usalama, kutoa elimu kwa ajili ya ufanisi zaidi pamoja na kuende-lea kuboresha huduma za msingi za Posta barani Afrika. Kutokana na mafanikio haya, Tanzania inajivunia Makao Makuu ya Umoja wa Posta barani Afrika kuwepo Tanzania katika Jiji la Arusha.
  5. Tanzania kupitia TCRA imekuwa mwanachama wa PAPU kwa muda mrefu. imesaidiaje kukamilisha malengo ya kuanzishwa kwa umoja huo?

Tanzania ni mjumbe wa kudumu wa Baraza la Uongozi la PAPU tangu kuanzishwa kwa Umoja huu kwa sababu ya kuwa mwenyeji wake. Kwa nafasi hii Tanzania imepata fursa ya kushiriki mafunzo, semina na mikutano mbalimbali ambayo imeijengea uwezo kuleta maboresho ya sekta ya posta katika bara la Afrika na nchini.

Tanzania imekuwa na hatua ya mbele katika mab-adiliko ya sekta hasa katika matumizi ya TEHAMA na utoaji wa huduma bora za posta. Kwa maana hiyo nchi yetu imekuwa chachu kwa maendeleo ya sekta ya Posta Afrika. Tanzania imepata fursa ya kutetea maslahi yake katika vikao vya uamuzi wa Umoja.

Ni mambo gani ambayo nchi inanufaika nayo kutokana na kuwa mwanachama wa PAPU?

PAPU ndicho chombo cha Umoja wa Afrika katika kue-ndeleza sekta ya posta. Kwa hiyo imekuwa ikisaidia nchi wanachama ikiwa ni pamoja na Tanzania kuhakikisha kwamba wanaboresha huduma kwa wananchi.

Nchi zote zinanufaika kwa kupitia PAPU kwa sababu ili sekta ya posta ifanikiwe lazima kusiwe na mipaka ya upelekaji na upokeaji wa huduma kati ya nchi na nchi (single postal territory).

Ni ipi nafasi ya PAPU katika kuboresha huduma za posta nchini na Afrika kwa ujumla?

Posta zote Afrika zinayo fursa kubwa ya kufanikisha wanunuzi na wauzaji kufikia malengo yao kupitia uratibu wa PAPU. Inawezesha kukamilisha mzunguko wa mnyororo wa thamani wa biashara mtandao kati yao.

Biashara mtandao inatoa fursa kwa posta kuhusu ufikishaji bidhaa na usambazaji ikiwa ni pamoja na urejeshaji wa bidhaa, malipo ikijumuisha malipomtandao, hawala za fedha na malipo ya posta, maendeleo ya madukamtandao na masoko mtandao.
Matumizi ya huduma za posta kwa sasa yakoje hapa nchini?

Matumizi ya Posta yanaendelea vema hasa katika maeneo ya biashara mtandao yaani e-commerce na usafirishaji wa mizigo (parcels and Cargo). Kumekuwa na changamoto kidogo katika usambazaji wa barua za kawaida kwa sababu ya ukuaji wa matumizi ya TEHAMA. Aidha, Huduma za fedha jumuishi za posta zimekuwa zikiongezeka.

Elimu ya matumizi ya huduma za posta inatolewa kwa kiasi gani na je kuna haja ya elimu hii kuingizwa katika mitaala ya shule za msingi na sekondari?

Elimu inatolewa kwa njia mbalimbali lakini bado inahitaji kutolewa zaidi. Elimu ya Posta na matumizi yake ilikuwa inatolewa katika shule miaka ya nyuma. Inashauriwa elimu ya masu-ala ya mawasiliano irudi tena shuleni na vyuoni ili kuimarisha uelewa wa sekta hii.

Kwa sasa dunia inashuhudia mapinduzi makubwa ya teknolojia hususani katika huduma za mawasiliano.

Kwa namna gani mapinduzi haya yameathiri huduma za posta?

Teknolojia ni changamoto lakini pia ni fursa kwa mashirika ya posta. TEHAMA imesaidia sana kuboresha shughuli za posta kuanzia uchakataji wa barua na mizigo hadi kufikisha kwa walengwa na kujenga imani ya ubora na usalama wa bidhaa. Aidha, teknolojia imesaidia Posta kuanzisha biashara na huduma mpya ambazo zinahitajika na wateja.

Mfano mzuri ni kwamba kampuni inaweza kutaka kuwasiliana na wateja wake wengi kwa mpigo. Kwa kutumia masanduku ya barua Posta inaweza kusambaza habari hizo kwa wingi kwa wakati mmoja.

Kuongezeka kwa imani ya wateja kunaongeza kuaminika kwa posta na kuleta wateja wengi zaidi. Mfano mwingine ni katika kuwezesha biashara mtandao (E-commerce). Mnunuzi anaweza kuagiza au kununua bidhaa kwa TEHAMA lakini atapokea mzigo halisi kwa kupitia Posta. Kwa sasa biashara mtandao ndiyo inaleta biashara kubwa kwa mashirika ya Posta.

Je Mamlaka kama TCRA ina nafasi gani kuhakikisha huduma za posta zinaendelea kutumika ipasavyo katika kipindi hiki ambacho teknolojia imeshika hatamu ulimwenguni kote?

TCRA inayo nafasi nzuri ya kuhakikisha uendelezaji wa huduma za posta nchini. Hii ni kwa kutumia nafasi yake ya kuweka mfumo mzuri na endelevu wa utoaji wa leseni za posta, Kanuni na kuishauri Serikali.

Mfumo wa leseni ukimpatia mtoa huduma za posta uhuru wa kutumia teknolojia inatoa uwezo wa kutoa huduma nyingi.

Kwa namna gani ushirikiano kati ya PAPU na TCRA umesaidia kuboresha sekta ya huduma za posta nchini?

PAPU imekuwa inashirikiana na mashirika mengine ya kimataifa kutoa mafunzo, kuandaa semina na makongamano ya kujenga uwezo wa kutoa huduma zinazohitajiwa na watumiaji wa huduma za posta.

TCRA inaizungumziaje sekta ya huduma za posta nchini wakati tukiadhimisha miaka 40 ya kuanzishwa kwa PAPU?

PAPU imepiga hatua nzuri katika kuiunganisha Afrika kuwezesha ubadilishanaji wa bidhaa za posta kati ya nchi wanachama na nchi zote nje ya bara la Afrika. Kifupi malengo yake yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

MAELEZO YA MKURUGENZI MKUU WA MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA MHANDISI JAMES M. KILABA KUHUSU MRADI WA UJENZI WA JENGO LA MAKAO MAKUU YA UMOJA WA POSTA AFRIKA (PAPU) ALIYOYATOA KWENYE HAFLA YA KUWEKA JIWE LA MSINGI TAREHE 18 JANUARI, 2020

Habari za Mchana!

Awali ya yote nianze kwa kumpa Sifa Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai hadi sasa; Lakini pia nikushukuru wewe Mheshimiwa Mhandisi Isack Aloyce Kamwelwe (Mb.), Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kufika katika uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika, ukiwa mgeni rasmi. Kusema ukweli hatua ya leo ni jambo kubwa kwa nchi yetu nzuri ya Tanzania na Bara zima la Afrika kwa sababu imekuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Kama ambavyo tumeendelea kusikia, Umoja wa Posta wa Afrika au Pan African Postal Union (PAPU) ulianzishwa mwaka 1980 ikiwa ni chombo au Taasisi maalum (Specialized Agency) ya Umoja wa Afrika (AU) yenye jukumu la kuendeleza sekta ya huduma za Posta Barani Afrika na Makao yake Makuu yakawa Jijini Arusha. Serikali yetu ya awamu ya kwanza chini ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na kukubali kuwa mwenyeji wa taasisi hii ya kimataifa pia ilitoa kiwan-ja kwa ajili ya kujengwa Makao Makuu yake.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Tangu PAPU ianzishwe Jijini Arusha haijawahi kuwa na ofisi yake ya kudumu na kwa hiyo imekuwa inatumia Makao Makuu ya muda. Mwanzoni ilihifadhiwa katika Ofisi za Shirika la Posta na Simu (mkoani Arusha) pale Telephone House, baadaye ilihamia Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) na kisha jengo la muda lililopo mahali hapa ambalo lilijengwa mwaka 2003.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Jengo hili lilijengwa baada ya juhudi za kujenga Makao Makuu ya kudumu na yenye hadhi ya kimataifa kuchelewa kukamilika. Mwaka 2013 Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilikubaliana na Umoja wa Posta Afrika (PAPU) kuingia ubia katika kujenga Makao Makuu haya kwa uwiano wa umiliki kwamba PAPU iwe na 60% na TCRA 40%. Ubia huu utaifanya Ofisi ya TCRA Kanda ya Kaskazini kuwa katika Jengo hili sambamba na PAPU. Katika jengo hili la PAPU kutakuwemo pia mgahawa, kumbi za mikutano na maeneo ya biashara.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Kufuatia makubaliano ya ubia, tarehe 6 Septemba, 2016 TCRA na PAPU walisaini Mkataba na M/S J.B Amuli Architects na Washirika wake kuwa Mshauri Mwelekezi wa ujenzi wa jengo hili la PAPU. Mkandarasi aliyechaguliwa kujenga Jengo ambalo jiwe la msingi utaliweka leo, ni Beijing Construction Engineering Group Co. Ltd. Mkataba wa Ujenzi wa Jengo hili la Makao Makuu ya PAPU ulisainiwa na pande zote za ubia Desemba 23, 2019 na utagharimu Shilingi za kitanzania 33,578,225,631.36.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Jengo hili litakuwa na urefu wa ghorofa kumi na sita (16) za juu na ujenzi wake utachukua muda wa miezi thelathini (30). Aidha, tarehe 8 Januari 2020, Mkandarasi alikabidhiwa kiwanja (site) hii kwa ajili ya kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Ninaomba kumalizia maelezo yangu kwa kukushukuru tena Mheshimiwa Waziri kwa kutenga muda wako kuifanya kazi hii leo. Ninaomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mgeni rasmi, kwamba TCRA, PAPU na timu yote ya kutekeleza kazi ya ujenzi wa Jengo hili la PAPU jijini Arusha tutafanya kila lililo ndani ya uwezo wetu kumaliza ujenzi katika muda uliopangwa na kwa ubora unaokusudiwa.

Naomba kuwasilisha