Bodi ya Mfuko wa Barabara inavyosimamia matengenezo ya barabara kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini


Bodi ya Mfuko wa Barabara inavyosimamia matengenezo ya barabara kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini

Usafiri wa barabara ndio usafiri unaotumiwa na watu wengi zaidi kuliko aina nyingine za usafiri kama vile usafiri wa ndege na reli. Inakadiriwa zaidi ya asilimia 80 ya wasafiri hutumia usafiri wa barabara na asilimia 90 ya mizigo yote husafirishwa kwa njia ya barabara.

Usafiri wa barabara ndio usafiri unaotumiwa na watu wengi zaidi kuliko aina nyingine za usafiri kama vile usafiri wa ndege na reli.Inakadiriwa zaidi ya asilimia 80 ya wasafiri hutumia usafiri wa barabara na asilimia 90 ya mizigo yote husafirishwa kwa njia ya barabara.

Aidha, mtandao wa barabara ndiyo rasilimali ya umma yenye thamani kubwa kuliko zote kwa nchi zote duniani. Kwa Tanzania, thamani ya barabara zilizo rasmi inakadiriwa kufikia takribani Sh 21 trilioni sawa na asilimia 16.4 ya pato la Taifa.

Usafiri wa barabara hutoa mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kuwezesha wananchi kupata huduma za kijamii na kushiriki kikamilifu katika kutekeleza shughuli zao za kiuchumi.

Kuwepo kwa mtandao mzuri wa barabara, wananchi huwa na uhakika wa kusafiri na kusafirisha mizigo yao kwa wakati na kupunguza gharama za usafirishaji na hivyo kupunguza gharama za kufanya biashara.

Matengenezo ya barabara

Tofauti na ujenzi wa barabara ambao hufanyika mara moja, matengenezo ya barabara hufanyika mara kwa mara ili kuzilinda barabara ambazo zimeshajengwa kwa lengo la kuwawezesha watumiaji wake kuzitumia kwa ufanisi na pia kuzifanya zisiharibike haraka.

Matengenezo yanayofanyika ni pamoja na kuziba mashimo, kuzibua mifereji, kukata nyasi kandokando ya barabara, matengenezo ya muda maalumu na matengenezo ya sehemu korofi.

Umuhimu wa matengenezo ya barabara

Ili mtandao wa barabara uweze kutoa mchango wake kwenye maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kuwanufaisha wananchi, ni lazima barabara zifanyiwe matengenezo ya mara kwa mara na kikamilifu.Hii ni kwa sababu baada ya barabara kujengwa huwa zinaharibika kutokana na matumizi yake na wakati mwingine kutokana na mvua.

Barabara isipotunzwa na kufanyiwa matengenezo kwa wakati inaweza kuharibika kabisa kiasi cha kuhitaji kujengwa upya kwa gharama ya zaidi ya mara tatu ya gharama ya matengenezo.

Inakadiriwa kuwa gharama za matengenezo huongezeka mara sita ya gharama kama barabara isipofanyiwa matengenezo kwa miaka mitatu na kama isipofanyiwa matengenezo kwa miaka mitano gharama huongezeka mara 18.

Hivyo matengenezo ya mara kwa mara ni muhimu ili kupunguza gharama. Watumiaji wa barabara hushirikishwa kikamilifu kwenye matengenezo ya barabara kwa kuwa hupata madhara ya moja kwa moja pale barabara zinapokuwa mbovu.

Madhara hayo ni pamoja na gharama kubwa za matengenezo ya magari, kuongezeka kwa gharama na muda wa safari na ongezeko la ajali za barabarani.

Mfuko wa Barabara na Bodi ya Mfuko wa Barabara

Kutokana na umuhimu wa matengenezo ya barabara kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, Serikali ilianzisha Mfuko wa Barabara na Bodi yake kama chombo mahsusi cha kusimamia matengenezo ya barabara nchini.Mfuko wa Barabara na Bodi yake vilianzishwa kupitia Sheria ya Tozo ya Barabara na Mafuta-Kifungu cha 220.

Majukumu ya Bodi ya Mfuko wa Barabara

Kisheria Bodi ya Mfuko wa Barabara ina majukumu makuu matatu, ambayo ni:

• Kukusanya fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara,

• Kugawa fedha hizo kwa ajili ya matengenezo ya barabara na

• Ufuatiliaji wa utekelezaji wa kazi za matengenezo ya barabara ili kuhakikisha zinafanyika kwa viwango vilivyopangwa.

Vyanzo vya mapato

Kwa mujibu wa sheria, Mfuko wa Barabara una vyanzo vikuu vitatu vya mapato ambavyo ni: tozo ya mafuta ya petroli na dizeli (fuel levy), ushuru wa magari ya kigeni mipakani (transit charges) na tozo ya kuzidisha uzito wa magari (overloading fees).

Tozo ya mafuta ni chanzo kikuu cha mapato ya mfuko ambacho huchangia takribani asilimia 97 ya mapato yote ya Mfuko. Kwa kila lita moja ya petroli au dizeli inayonunuliwa hutozwa Sh 263. Aidha, magari ya kigeni hutozwa dola 6 hadi 16 za Kimarekani kulingana na aina ya gari.

Vyanzo vingine ni pamoja na ada ya mae-gesho ya magari na matumizi ya hifadhi ya barabara. Fedha zinazokusanywa kwenye vyanzo hivi hupelekwa moja kwa moja kwenye mfuko kwa ajili ya kugharamia matengenezo ya barabara.

Asilimia 90 ya fedha zote zinazokusanywa hutumika kugharamia matengenezo ya barabara yanayofanywa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).

Aidha, asilimia 10 inayobaki hutumika kugharamia shughuli zinazohusu miradi ya ujenzi mpya wa barabara zinazofanywa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Mtandao wa Barabara

Kwa sasa mtandao wa barabara nchini una urefu wa kilomita 170,471 – ikijumuisha kilomita 34,490 za barabara za kitaifa na kilometa 135,981 za barabara za Wilaya. Matengenezo ya barabara za kitaifa husimamiwa na TANROADS na matengenezo ya barabara za Wilaya husimamiwa na TARURA.

Mafanikio

Kutokana na juhudi za Serikali kupitia Bodi ya Mfuko wa Barabara, kumekuwa na ongezeko la makusanyo ya mapato ya mfuko wa Barabara. Makusanyo ya tozo ya mafuta yaliongezeka kutoka Sh 705,091 milioni mwaka 2015/16 hadi kufikia Sh 747,160.6 milioni mwaka 2017/18 sawa na asilimia 6.

Kutokana na Serikali kuweka mazingira mazuri ya biashara ya usafirishaji, wafanyabiashara wa nchi jirani za ukanda wa maziwa makuu wamevutiwa kutumia barabara na bandari zetu.

Ongezeko la magari yanayotumia barabara zetu ambayo hayajasajiliwa nchini, limesababisha mapato yatokanayo na ushuru wa magari ya kigeni kuongezeka kwa takribani asilimia 60 katika kipindi cha miaka mitatu.

Ongezeko la mapato limeuwezesha mfuko kugharamia shughuli nyingi za matengenezo ya miundombinu ya barabara na hivyo kufanya mtandao wa barabara kuwa katika hali nzuri.

Changamoto

Changamoto kubwa inayoikabili Bodi ya Mfuko wa Barabara ni uwezo mdogo wa kukidhi mahitaji ya matengenezo ya barabara. Kwa sasa, uwezo wa Mfuko unatosheleza asilimia 41 tu ya mahitaji halisi ya matengenezo ya barabara hapa nchini.

Bajeti kwa ajili ya mtandao wa barabara za kitaifa ilikidhi kwa asilimia 44 na mtandao wa barabara za Wilaya asilimia 35 ya mahitaji yote ya fedha.

Hii ni baada ya kuondoa barabara zile zenye hali mbaya zinazohitaji pesa ya maendeleo. Changamoto hii imesababishwa na mtandao mkubwa wa barabara unaogharamiwa na Mfuko ni wa changarawe au udongo ambao uharibika kirahisi kipindi cha mvua na hivyo kuhitaji matengenezo ya mara kwa mara.

Ili kuondokana na tatizo hili, Serikali inaendelea na mpango wa kuzifanya barabara nyingi kuwa za lami au kutumia teknolojia mbadala kama vile kujenga kwa mawe.

Uzidishaji wa mizigo kwenye magari makubwa kinyume na ule unaokubalika kisheria unaosababisha barabara kuharibika kabla ya muda wake.

Ili kudhibiti uharibifu huu, Bodi inafuatilia kwa undani sababu za kutokoma kwa uzidishaji wa uzito wa magari ikiwa ni pamoja na kuangalia kiwango cha faini kama kinatosha kuwaadhibu wanaokiuka sheria.

Pia, kupitia kamera za barabarani ukiukwaji wa taratibu za kwenye mizani umekuwa ukifuatiliwa na wahusika kuchukuliwa hatua. Uharibifu wa samani za barabara ikiwa ni pamoja na alama za usalama barabarani. Uharibifu huu husababishwa na ajali za barabarani pamoja na wananchi ambao huondoa samani za barabara zenye asili ya chuma na kuuza kama chuma chakavu.

Ili kukabiliana na changamoto ya ajali, Bodi imepeleka mapendekezo serikalini ili kurasimisha ukaguzi wa vyombo vya moto vitumiavyo barabara.

Pia, imezishauri taasisi zinazohusika na barabara kutumia teknolojia isiyohusisha chuma ili kutowashawishi wanaohitaji chuma.

Mikakati

Ili kukabiliana na changamoto, Bodi ya Mfuko wa Barabara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inatekeleza mikakati ifuatayo:

Kuelimisha watumiaji wa barabara umuhimu wa kutunza na kulinda miundombinu ya barabara na pia madhara ya kutumia mafuta yaliyochakachuliwa katika vyombo vya moto.

Kuratibu utafiti wa teknolojia mbadala na rahisi ya matengenezo ya barabara ili kupata teknolojia itakayopunguza gharama na kuongeza ufanisi katika matumizi ya fedha za mfuko.

Kuendelea na ufuatiliaji wa ubora wa kazi za matengenezo ya barabara katika mikoa yote.

Bodi pia itaendelea kuishauri Serikali juu ya namna ya kuongeza mapato ya mfuko kulingana na wakati muafaka.

Kutumia teknolojia ya kisasa katika kuimarisha usimamizi wa uendeshaji wa mizani ya kupimia magari ili kupunguza idadi ya magari yanayozidisha uzito na hivyo kuzilinda barabara zetu.

Kurasimisha ukusanyaji na utoaji taarifa juu ya vyanzo vinavyotokana na matumizi ya maeneo ya akiba ya barabara (road reserve user charges).

Wito

Wito unatolewa kwa watumiaji wa barabara kuzingatia na kufuata sheria na taratibu zilizowekwa ili kuzilinda barabara zetu. Jambo kubwa la kuzingatia ni kuepuka kuzidisha uzito uliowekwa kisheria kwa kuwa uzito mkubwa wa magari ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa barabara.

Pia, tunatoa wito kwa watumiaji kulinda miundombinu ya barabara na samani zake ikiwa ni pamoja na vibao vya alama za barabarani na kingo za madaraja. Ni muhimu pia watumiaji kuepuka kutengenezea magari barabarani kwa kuwa husababisha uharibifu wa barabara na inaweza kusababisha ajali.