Room to Read Tanzania inalinda ustawi na haki za mtoto wa kike kupitia elimu

Muktasari:

Desemba 19, 2011, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio na kutangaza Oktoba 11 kuwa siku ya kimataifa ya Mtoto wa Kike duniani kote, dhamira ikiwa ni kutambua haki za mtoto wa kike na changamoto za kipekee anazokutana nazo.

Mnamo Desemba 19, 2011, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio na kutangaza Oktoba 11 kuwa siku ya kimataifa ya Mtoto wa Kike duniani kote, dhamira ikiwa ni kutambua haki za mtoto wa kike na changamoto za kipekee anazokutana nazo.

Kila mwaka wadau mbalimbali wanaadhimisha siku hii ya mtoto wa kike, na katika Taifa letu siku hii huadhimishwa kitaifa kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Moja kati ya wadau hao ni Shirika la Room to Read (RtR) Tanzania ambalo limejikita katika kusambaza elimu kwa jamii ili kuweza kusaidia kuboresha ustawi wa watoto nchini ambao wamekuwa wahanga wa matatizo mbalimbali.

Meneja Mradi Mwandamizi wa Mradi wa Usawa wa Kijinsia na Elimu kwa Msichana, Zamaradi Islahi Said katika mahojiano na gazeti la Mwananchi, ameelezea namna shirika hilo linavyosimamia ustawi wa watoto wa kike nchini.

Vitendo vya ukatili kwa watoto wa kike hufanywa na watu ambao wana ufahamu na elimu kuhusiana na haki za msingi za watoto wa kike. Shirika lenu inafanya jitihada gani kuondoa kadhia hii?

Ni kweli, kwa asilimia kubwa ukatili wa watoto wa kike na makundi mengine yaliyotengwa kama vile wanawake, maalbino, walemavu na wazee hufanywa na watu wenye ufahamu na wakati mwingine watu wa karibu zaidi au wa ndani ya familia zao.Room to Read ni shirika linaloamini juu ya kutendewa kwa usawa kwa jinsia zote, kupitia Mradi wake wa Usawa wa Kijinsia na Elimu kwa Msichana, shirika linafanya jitihada za kusimamia usawa kwa mtoto wa kike kwa kutambua changamoto za kipekee anazokutana nazo.

Pia, Shirika linamjengea msichana stadi za maisha zitakazomwezesha kujisimamia, kujiamini, kupaza sauti na kupinga unyanyasaji na ukatili wowote wa kijinsia kwake binafsi na kwa jamii inayomzunguka. Kupitia mradi huu, wasichana wanapatiwa ushauri wa namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika maisha yao ya kila siku; na kujengewa stadi za kupima na kufanya maamuzi sahihi wao wenyewe.

Wasichana pia wanapatiwa stadi za uwekaji akiba na ujasiriamali ambazo zitawasidia kutambua thamani ya kile wanachopokea na kile watakachopata baada ya kukamilisha malengo yao wanapokuwa shuleni.

Hii huwasaidia kupinga ukatili kwa kujitosheleza wao wenyewe wawapo shuleni na baada ya kumaliza shule wanakuwa na uwezo wa kujiajiri wao wenyewe. Katika kuhakikisha wanapata malezi bora, wasichana wanajengewa stadi za maisha na kupewa ushauri. Shirika limeajiri wahamasishaji jamii wa kike wa mradi wa usawa wa kijinsia na elimu kwa msichana ambao ni mfano wa kuigwa kwa wasichana wadogo.

Shirika linashirikisha jamii zinazozunguka shule za mradi juu ya haki ya elimu kwa mtoto wa kike kwa kuandaa na kuendesha mafunzo, vikao na mijadala. Shirika letu linafuata sera ya ndani inayolinda haki za mtoto (Child Protection Policy) ambapo ukatili kwa mtoto ni suala lisilovumilika. Shirika lina utaratibu wa kutoa taarifa katika Dawati la Jinsia, Ofisi ya Maendeleo ya Jamii n.k. pale inapotokea vitendo vya kikatili.

Wapi mnafikiri kama taifa tunakwama linapokuja suala la mifumo sahihi ya uelimishaji watoto kuhusiana na haki zao za msingi? Na nini kinatakiwa kufanyika?

Room to Read inatambua jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Tanzania, licha ya kuwepo kwa vikwazo mbalimbali vinavyozuia watoto wa kike kupatiwa elimu juu ya haki zao. Mfano mzuri ni utekelezaji hafifu wa haki ya mtoto Katika ngazi ya familia na jamii ambapo sheria ya mtoto Kifungu 95 (1)-(5) inamuwajibisha kila mwanajumuiya kutoa taarifa serikali ya mtaa iwapo haki za mtoto zinavunjwa.

Wavunjaji wa haki hii ni wanafamilia na wanajamii ambao hufanya hivyo kwa maslahi ya muda mfupi, lakini hatua za kisheria zimekwama kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya kukosa ushirikiano wa jamii husika kutokana na kulindana ndani ya familia kwa kuficha aibu bila kujali athari kubwa inayompata mtoto wa kike katika maisha yake yote. Utekelezaji hafifu katika ngazi ya serikali za mitaa.

Tukirejea sheria ya mtoto kifungu cha 94, (1)-(7), inaipa majukumu serikali ya mtaa kulinda na kukuza ustawi wa mtoto katika eneo lake. Hii inajumuisha mamlaka ya vitongoji, mitaa na vijiji. Hata hivyo, bado sheria hii haijafikishwa kikamilifu na utekelezaji wake bado una changamoto kadha wa kadha.Mfumo wa Elimu: Elimu juu ya haki za mtoto haijatolewa kikamilifu hasa katika shule zetu, hata pale inapotolewa inakinzana na vitendo vinavyofanywa katika maisha ya shule, mfano bado zipo adhabu zilizopitiliza kiwango zinazotolewa kwa watoto wa kike.

Mara kadhaa imetokea msichana anapopewa ujauzito na mwalimu, msichana hufukuzwa shule lakini mwalimu uhamishiwa shule nyingine au hupewa adhabu isiyo-lingana na athari aliyosababisha.

Taarifa hizi huishia ndani kwa ndani bila kufikishwa sehemu ambayo haki ya mtoto inaweza kupatikana. Hivyo, Serikali yetu inapaswa kuweka mfumo wa kufundisha stadi za maisha kiukamilifu katika shule zote za msingi na sekondari ambazo zitawajengea wasichana uwezo wa kujitambua, kujithamini, kujidhibiti, kukataa shinikizo, kustahmili, kujiamini na kufanya maamuzi sahihi ya maisha yao ya sasa na baadaye.

Pia, Serikali iwachukulie hatua kali waharibifu wanaowakatili wasichana hawa ikiwa ni pamoja na kuwapa adhabu inayolingana na kuharibu maisha ya mtoto wa kike kama vile kuwafunga kifungo cha maisha.

Nini kinasimama kama alama ya mafanikio yenu mkiangalia wapi mlipotoka mpaka sasa?

Alama kubwa ya mafanikio tuliyoweza kupata tangu mwaka 2012 hadi sasa ni kuweza kubadilisha maisha ya wasichana wengi wasiopungua 3800 katika kupata haki ya kujiunga na shule, kubaki shuleni na kuhitimu elimu ya sekondari ikiwa ndiyo lengo la Mradi wa Usawa wa Kijinsia na Elimu kwa Msichana.

Mafanikio yetu yameonekana zaidi katika maeneo yafuatayo:-

• Kupunguza tatizo kubwa la mdondoko (kuacha shule) kwa wasichana walio kwenye mradi wetu kutoka asilimia 18 mwaka 2012 hadi asilimia 1 mwaka 2016, na asilimia 3.26 mwaka 2019.

• Kupungua kwa idadi ya wasichana wanaopata ujauzito wakiwa shuleni ambapo mwaka 2014 kulikuwa na mimba 13, wakati mwaka 2019 kulikuwa na mimba 3 katikashule zote tunazofanya mradi zenye wasichana zaidi ya 3800. Tatizo la mdondoko kutoka shule kwa wasichana hapa nchini ni kubwa ambapo taarifa zinaonyesha kuwa Tanzania inaongoza katika mdondoko unaosababishwa na mimba peke yake kwa asilimia 27.

• Kupungua kwa tatizo la utoro wa rejareja na utoro sugu: Shirika letu limeandaa utara-tibu wa ufuatiliaji wa karibu kwa wanafunzi watoro kwa kutumia wahamasishaji, serikali za mtaa na kamati za wazazi ambapo tatizo la utoro wa rejareja na wa kudumu limepungua kwa kiasi kubwa katika shule za mradi.

• Ongezeko la kiwango cha ufaulu kitaaluma na kushika nafasi za juu kwa wasichana walio katika shule za mradi: Wakati tunaanza mradi wetu mkoani Pwani mwaka 2014, wasichana walikua hawaingii katika nafasi kumi bora, lakini taarifa za ufaulu kuanzia mwaka 2016 hadi 2019 zinaonyesha wasichana wakishika nafasi katika kumi bora kwa asilimia 70 hadi 80. Kiwango cha ufaulu kwa madarasa ya mitihani hasa kidato cha pili ambapo wasichana walikuwa wakirudia madarasa kime-ongezeka kutoka asilimia 87 mwaka 2017 hadi asilimi 92.07 mwaka 2019.

• Kumekuwa na ongezeko la idadi ya wasichana waliohitimu elimu ya sekondari na kujiunga na elimu ya juu na vyuo mbalimbali kutoka asilimia 16 mwaka 2017 hadi asilimia 52 mwaka 2019.

• Shirika la Room to Read limeweza kuanzisha mfumo maalumu wa ukusanyaji taarifa unaoweza kugundua viashiria vya mwanzo vya wasichana kuacha shule na kubuni mbinu za ufuatiliaji ili kudhibiti tatizo hili. Mfumo huu ni wa kipekee ambao umeleta mafanikio makubwa ya kupunguza tatizo la utoro na kuacha shule kama ilivyoelezwa hapo mwanzo.

• Shirika letu pia limeweza kuandaa vitini vya kufundishia na kujifunzia stadi za maisha kuanzia darasa la tano hadi kidato cha nne ambavyo vimeleta mafanikio makubwa kwa wasichana walio katika mradi kupata uelewa mpana wa kukabiliana na kutatua changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika ukuaji ikiwa ni pamoja na mabadiliko chanya ya tabia.

• Zaidi ya wasichana 3800 wamefadhiliwa na shirika letu kwa kupata msaada wa vifaa kulingana na mahitaji kama vile ada za bweni, baiskeli, sare za shule, madaftari, vitabu vya kiada, vitabu vya ziada, vifaa vya maabara; na elimu na vifaa vya kutengeneza taulo za kike.

• Jamii katika maeneo ya mradi imehamasika na kusaidia jitihada za elimu kwa msichana, hii ni pamoja na kuanzishwa kwa kamati za wazazi ambazo zinashughulikia ajenda ya umuhimu wa elimu kwa msichana katika ngazi ya kata na pia kuhamasisha wazazi wenzao katika maeneo yao.

• Kuimarika kwa ushirikiano kati ya shirika la Room to Read na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa kuendelezwa kwa shughuli za mradi wa Room to Read chini ya utaratibu wa kawaida katika Shule ambazo shirika limemaliza kutekeleza miradi yake mwaka 2019. Shughuli hizi ni pamoja na walimu kuendelea kufundisha Elimu ya Stadi za Maisha na Ushauri baada ya mradi kumalizika katika shule za Kingani, Chalinze, Lugoba, Zinga, Kiromo na matimbwa katika wilaya za Chalinze na Bagamoyo.

• Kuongezeka kwa cha-chu ya utekelezaji wa mradi wa Elimu kwa Msichana mkoani Pwani, ambapo mwaka 2019, Ofisi ya Elimu mkoani Pwani iliazimia kutafuta rasilimali ili kuongeza idadi ya shule zaidi ya 70 ambazo bado hazijanufaika na mradi wa Elimu kwa Msichana.

• Room to Read imeendelea kufanya tafiti zinazolenga kutambua zaidi namna bora ya kutatua changamoto zinazomkabili mtoto wa kike kwa sasa na baadaye. Hii ni kuto-kana na utafiti uliofanywa mwaka 2018 na kubaini kwamba Elimu ya Ujasiriamali huanza kutolewa vyuoni jambo ambalo si sahihi. Hivyo, shirika lilianzisha mradi wa Elimu ya Fedha na Ujasiriamali kwa shule za mradi na tathmini inaonyesha kwamba, elimu hii imewanufaisha wanafunzi na familia zao kuelewa umuhimu wa akiba na kubuni miradi mbalimbali kama vile ufugaji wa kuku kitaalamu, kufanya biashara kitaalamu na kupata mafanikio katika ngazi ya familia hasa katika kuongeza kipato.

Jarida la “My Voice” la Room to Read linajumuisha shuhuda mbalimbali za mafanikio waliyoyapata wasichana na familia zao.

Mnashirikiana na taasisi gani katika utekelezaji wa majukumu yenu?

Room to Read inaamini juu ya nguvu ya pamoja na uwezo tofauti unaoweza kujenga taifa moja. Kwa kuamini hivyo, tunashirikiana na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Taasisi ya Elimu Tanzania pamoja na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kama vile Aflatoun International, Plan International, Kasole Secrets, Girls on Fire n.k.

Mnakabiliana na changamoto gani katika masuala yanayohusu watoto wa kike?

Changamoto za mtoto wa kike ni nyingi ambazo zinahitaji uwekezaji wa muda na rasilimali fedha ili kuweza kupata mafanikio. Moja ya changamoto kubwa ni ushikiliaji wa mila na desturi zilizopitwa na wakati katika baadhi ya jamii.Ushirikiano mdogo kutoka kwa baadhi ya wazazi: Katika jamii tunazofanya kazi, si jambo la ajabu mzazi au mlezi kumkataza binti yake kujibu maswali ya mtihani vizuri ili afeli na akose sababu ya kuendelea na masomo. Umaskini: Wasichana wengi wanatoka katika familia zenye kipato duni ambazo haziwezi kumudu gharama za kununua vifaa vya shule kama vile sare pamoja na kwamba elimu ni bure hapa Tanzania.

Wapi ambapo kama taasisi mnatarajia kufika na kwa kiwango gani mnatamani kufanikiwa?

Room to Read kama shirika limedhamiria kuona watoto walioelimika na taifa lenye usawa wa kijinsia lin-alompa kipaumbele mtoto wa kike ambaye kwa miaka mingi ameachwa nyuma. Kwa maono haya, Room to Read itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau mbalimbali katika mikakati tofauti tofauti ili kuweza kuunga mkono jitihada za serikali za kuboresha elimu hapa Tanzania.

Tungependa kupaza sauti kwa Watanzania wote kwamba Mabadiliko Chanya ya Ulimwengu Yanaanza na Mtoto Aliyeelimika bila kujali jinsia, tabaka au rangi.

Kuhusu Room to Read

Shirika la Room to Read ni shirika lisilokuwa la kiserikali na lisilotengeneza faida, liloanzishwa miaka 20 iliyopita na lenye makao makuu yake huko San Francisco, California nchini Marekani. Room to Read inalenga katika kubadilisha maisha ya mamilioni ya watoto katika jamii zenye kipato cha chini kwa kuzingatia kusoma na kuandika na usawa wa kijinsia katika elimu. Shirika linafanya kazi kwa kushirikiana na jamii, mashirika mbalimbali pamoja na serikali katika kuendeleza ujuzi wa kusoma na kuandika na tabia ya kusoma kati ya watoto wa shule ya msingi. Shirika pia linalenga kusaidia watoto wa kike kumaliza shule ya sekondari wakiwa na stadi za maisha zinazostahili ili kufaulu shuleni na kwingineko katika maisha ya baadaye. Mpaka sasa shirika lipo katika nchi 13 duniani kote ikiwemo Tanzania.

Room to Read Tanzania

Shirika la Room to Read Tanzania (RtR) kama sehemu ya Room to Read limeanza kufanya kazi nchini Tanzania mnamo mwaka 2012 katika mkoa wa Morogoro wilaya ya Mvomero na baadae kuenea katika mikoa ya Pwani na Tanga. Shirika kupitia sekta ya elimu linalenga kuboresha stadi za usomaji na usawa wa kijinsia katika sekta ya elimu, ikiwemo upatikanaji wa fursa sawa za kielimu kwa kila mtoto bila kujali jinsia yake.

Room to Read inaamini kwamba mabadiliko ya ulimwengu yanaanza na mtoto aliyeelimika. Room to Read Tanzania inafanya kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu katika kuboresha elimu katika mikoa ya Pwani na Tanga kwa kujenga na kuimarisha stadi za usomaji na tabia ya usomaji kwa wanafunzi katika ngazi ya elimu ya msingi yaani darasa la kwanza na la pili.

Aidha, shirika linajishughulisha na uboreshaji wa fursa za elimu kwa watoto wa kike katika shule za msingi na sekondari katika wilaya za Kibaha, Chalinze na Bagamoyo kupitia mradi wake wa Usawa wa Kijinsia na Elimu kwa Msichana wenye lengo la kuwasaidia wasichana kumaliza elimu yao ya sekondari na kupata stadi muhimu zitakazowawezesha kufanya maamuzi sahihi ya kimaisha kwa wakati sahihi. Mpaka sasa kwa Tanzania pekee, mradi wa Usawa wa Kijinsia na Elimu kwa Msichana umefikia jumla ya wanufaika zaidi ya 3800 kwa shule za msingi na sekondari.