Breaking News

Dk Magufuli akabidhiwa cheti cha ushindi

Friday October 30 2015Rais mteule wa Tanzania, Dk John Magufuli

Rais mteule wa Tanzania, Dk John Magufuli 

By Matern Kayera, Mwananchi Digital

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva amemkabidhi cheti cha ushindi wa urais Dk John Magufuli wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Sherehe hizo ambazo zimefanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam leo, zimehudhuriwa na Rais Jakaya Kikwete, viongozi mbalimbali wa kitaifa pamoja na marais wastaafu wa Msumbiji na Nigeria. Jaji Lubuva kabla ya kumkabidhi Dk Magufuli cheti hicho, alianza kwa kurudia kuyasoma matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Dk Magufuli na wagombea wengine walioshiriki kwenye uchaguzi huo ngazi ya urais. Akizungumza kwa niaba ya vyama vingine vya upinzani, mgombea urais wa chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira amekubali matokeo yaliyompa ushindi Dk Magugufuli na kumtaka asimamie hoja ya mabadiliko ambayo vyama vyote iliitumia wakati wa kampeni. “Namuomba Rais Mteule, Dk Magufuli asimamie mabadiliko ambayo ni matamanio ya Watanzania wote. Jambo la kwanza ambalo ni msingi wa mabadiliko yote ni kuhakikisha tunapata Katiba mpya itakayotokana na maoni ya wananchi na mambo mengine yatafuata,” alisema Mghwira. Aliongeza kuwa Magufuli anawajibu wa kusimamia umoja wa kitaifa, usawa wa kijinsia kati ya wanawake na wanaume, kusimamia serikali na mfumo wa uchumi ili kuondoa umaskini nchini kwa kuwa Tanzania na watanzania siyo maskini. Wagombea urais wa vyama vya Chadema Edwar Lowassa, Hashim Rungwe wa Chauma na Maximilian Lyimo wa TLP hawakuhudhuria sherehe hizo.