Wachezaji Stars, mapambano bado yanaendelea

Muktasari:

  • Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kesho itakuwa kwenye Uwanja wa Taifa kwa mchezo wa marudiano dhidi ya Cape Verde kuwania kufuzu fainali za Afrika ‘Afcon 2019’ ikiongozwa na kocha Emmanuel Amunike

Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kesho itakuwa kwenye Uwanja wa Taifa kwa mchezo wa marudiano dhidi ya Cape Verde kuwania kufuzu fainali za Afrika ‘Afcon 2019’ zitakazofanyika nchini Cameroon. Itakumbukwa kwamba Ijumaa iliyopita, Stars ilikuwa ugenini kucheza na timu hiyo na kufungwa mabao 3-0.

Tunaamini kuwa kocha Emmanuel Amunike amefanyia kazi maeneo yote yaliyosababisha kupoteza mchezo huo na kinachosababisha safu yake ya ushambuliaji isipate hata goli moja katika mechi mbili alizoiongoza timu hiyo.

Matokeo ya Ijumaa yameiweka Taifa Stars mahali pabaya. Inashika mkia katika Kundi L baada ya kutoka sare mbili na kupoteza mchezo moja. Uganda ina nafasi kubwa ya kufuzu kwani ina pointi saba ikifuatiwa na Cape Verde (nne) na Lesotho ambayo haina tofauti na Stars kwani zinazidiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Kwa maana hiyo, kinachotakiwa katika mechi ya kesho ni ushindi ili kufufua matumaini ya kwenda Cameroon mwakani na kinyume chake itakuwa imepoteza tena nafasi hiyo ambayo iliipata mara moja katika historia ya nchi mwaka 1980 wakati zilipofanyika huko Lagos, Nigeria. Tunaamini kwamba wachezaji wetu wataingia katika mchezo huo wakiwa na uelewa mzuri wa mambo mawili makubwa yanayohusiana na mechi hiyo.

Jambo la kwanza ni uwezo wa adui. Kama tulivyodokeza awali, tunaamini kwamba Amunike na benchi lake la ufundi wameziona kasoro za kifundi zilizojitokeza na kuzifanyia marekebisho. Wahenga walisema kutenda kosa si kosa, bali kurudia kosa. Tunaamini kwamba makosa yaliyosababisha kupoteza mchezo yatakuwa yamefanyiwa kazi.

Jambo la pili tunaamini kwamba wachezaji wataingia uwanjani wakifahamu fika kwamba kupoteza mchezo huo si tu kutawatoa katika mbio za kucheza fainali, bali tutaipoteza fursa adhimu ya kuitangaza nchi na wachezaji wenyewe katika anga la kimataifa.

Tofauti na miaka ya 1980 wakati Stars iliposhiriki katika fainali hizo, mchezo wa mpira wa miguu hivi sasa ni fursa kubwa kiuchumi na kidiplomasia kwani ukitumika vyema, unaweza kuifanya kazi ya kulitangaza Taifa kwa kiwango kikubwa. Mfano mzuri ni nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta ambaye anaichezea KRC Genk inayoshiriki Ligi ya Daraja la Kwanza ya Ubelgiji. Amekuwa katika kiwango bora na sasa amekuwa akihusishwa na timu mbalimbali kubwa za Ulaya.

Hiyo ina maana kwamba wadau wa mpira wa miguu ambao ni wengi zaidi duniani wataifahamu Tanzania kupitia kwake hivyo kuwa rahisi kwa sekta nyingine kama za utalii na uwekezaji kufanya kazi yao kwa ufanisi zaidi.

Njia mojawapo ya kufika ngazi hiyo ya kutambuliwa kimataifa ni kushiriki katika michezo mikubwa kama fainali hizo za Afcon. Hakuna shaka kwamba Tanzania ikifanikiwa kwenda Cameroon, kuna uwezekano mkubwa wa kupata kina Samatta, Simon Msuva na wengine wanaocheza nje ya nchi na wingi wao utawezesha kazi hiyo ya kulitangaza Taifa kuwa na ufanisi zaidi. Lakini si hayo tu, kuna manufaa makubwa ya kiuchumi kutoka kwa wachezaji hao ambayo yanakwenda katika familia zao na hata jamii kwa ujumla.

Kwa kuzingatia hayo, tunaamini wachezaji wetu watapambana kufa au kupona kuhakikisha kwamba Tanzania haipotezi fursa hii.