Bei ya mafuta yazidi kushuka
Muktasari:
Bei ya mafuta imeendelea kushuka, baada ya Ewura kutangaza bei mpya kuanzia kesho, ambapo lita moja ya petroli itauzwa Sh2, 886, dizeli Sh3083 na mafuta ya taa Sh3, 275 kwa lita.
Dar es Salaam. Vicheko vitaendelea kutawala Oktoba kwa watumiaji wa mafuta kufuatia kushuka kwa bidhaa za mafuta kama mwenendo wa bei ulivyotolewa leo Oktoba 4.
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) inaonyesha kuwa bei za mafuta kuanzia Oktoba 5 zimeshuka hivyo petroli katika jiji la Dar es Salaam itauzwa Sh2,886 kwa lita, dizeli Sh3083 na mafuta ya taa Sh3,275 kwa lita.
Kulingana na taarifa hiyo kushuka kwa bei za mafuta kumetokana na kushuka kwa bei ya bidhaa hizo katika soko la dunia kwa Agosti 2022, ambazo zimetumika katika kukokotoa bei za mafuta za hapa nchini katika mwezi wa Oktoba 2022 zimepungua kwa asilimia 7.4, 3.9 na 1.9 kwa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa, mtawalia, ikilinganishwa na bei hizo kwa mwezi Julai 2022.
“Hata hivyo, ikilinganishwa na gharama za uagizaji zilizotumika katika kukokotoa bei za Septemba 2022, gharama za uagizaji wa mafuta zimeongezeka kwa kati ya asilimia 50 na 163 kwa kutegemea bandari na bidhaa husika ikilinganishwa na gharama za uagizaji zilizotumika katika kukokotoa bei za Septemba 2022, na hivyo kuathiri mwenendo wa bei za mafuta hapa nchini.
“Pamoja na hayo, kufuatia dhamira ya Serikali ya kuendelea kupunguza madhara ya ongezeko la bei za mafuta hapa nchini kwa wananchi na uchumi kwa ujumla, Serikali imetoa ruzuku ya Sh59.58 bilioni kwa ajili ya bei za mafuta ya Oktoba 2022,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Ewura Modestus Lumato.