Zitto agusa umasikini wa Watanzania, awapa mbinu

Muktasari:
- Zitto amedai kuwa watu ambao wanaishi chini ya mstari wa umasikini ni wale ambao kwa siku moja mtu anashindwa kupata Sh 1,600 na kuzitumia.
Katavi. Wakati Taifa linaelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025, Chama cha ACT Wazalendo, kimewataka Watanzania kupima watawala kama wametimiza malengo ya kupunguza umasikini wananchi kama ilivyoanishwa kwenye Katiba.
Chama hicho kimefafanua kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ibara ya 9 (i) imeanisha juhudi zote zielekezwe katika kuondoa umasikini ambao kimedai Serikali imeshindwa kutekeleza jukumu la kupunguza umasikini kwa Watanzania.
Hayo yamebainishwa na Kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe leo Alhamisi Julai 3, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Inyonga wilayani Mlele mkoani Katavi katika mwendelezo wa ziara ya iliyopewa jina la 'Operesheni Majimaji Linda Kura Yako.'
Operesheni 'Majimaji Linda Kura' itadumu kwa siku 30 kwa viongozi wakuu wa chama hicho waliojigawa katika makundi mawili.
"Tumefanya uchaguzi mwaka 2020 na mwingine tutafanya mwaka huu, tujiulize katika utekelezaji ibara ya 9 (i) Serikali iliyopo madarakani imefanya nini.Baada ya uchaguzi wa mwaka 2020 idadi ya wananchi masikini Tanzania walikuwa milioni 14.
"Watu ambao wanaishi chini ya mstari wa umasikini ambayo ni wale kwa siku moja mtu anashindwa kupata Sh1,600 na kuzitumia. Mwaka 2024 watu ambao hawawezi kupata Sh1,600 kwa siku wameongezeka hadi milioni 26," amedai Zitto Kabwe ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya uchumi.
Amefafanua kwa nyakati tofauti wabunge na viongozi wa Serikali wa mikoa na wilaya wamekuwa wakisisika katika majukwaa wakisema 'mama ameshusha mabilioni' lakini hakuna siku waliosema kiwango cha umasikini kimepungua.
Zitto amedai sera za CCM bado haziondoi umasikini wa Watanzania, ndio maana ACT Wazalendo kinawaomba wananchi kuwaunga mkono kukiondoa chama hicho tawala.
"Bunge lililoisha limeshindwa kuhoji Serikali kuhusu hili kwa sababu lilikuwa la chama kimoja. Kipindi ambacho umasiki ulipungua ni pale ambapo kulikuwa na wabunge wa upinzani na demokrasia imetamalaki, ambao walikuwa wakihoji Serikali," amedai Zitto.
Kwa mujibu wa Zitto, mikoa kanda ya magharibi ikiwemo ya Tabora, Rukwa, Kigoma na Katavi ndio inayoongoza kwa masikini na kuna tofauti kubwa kati ya walioanacho na wasionacho.
Mwaka 2024 akihojiwa na TBC Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo alisema katika miaka 25 ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo (2000-2025) kiwango cha umasikini kimepunguzwa hadi kufikia asilimia 26, na lengo ni kumaliza katika miaka 25 ijayo.
"Kama tumeweza kupunguza hadi kufikia asilimia 26, tunataka kuona hii asilimia 26 kuelekea mwaka 2050 tuweze kuondoa kabisa," alisema Profesa Mkumbo huku akiongeza kuwa suala la kuondoa umasikini ni la nchi zote duniani kwani hakuna nchi iliyofanikiwa kwa asilimia 100.
Katika hotuba yake Zitto amesema hali ya umasikini iliyopo wananchi watakwenda nayo katika uchaguzi, ndio maana ACT Wazalendo inawaomba Watanzania wakiunge mkono ili kukomesha changamoto hiyo na wasipofanya hivyo Bunge litarudi lilelile la CCM pekee.
"Ndio maana tunawataka msikate tamaa ya kuondoka katika michakato ya uchaguzi ambayo ndio njia pekee ya kufanya mabadiliko.Twendeni kwenye uchaguzi ili tuindoe CCM katika mazingira haya haya yaliyopo," amesema.
"Ukikimbia kuingia katika uchaguzi unarefusha muda wa CCM kuendelea kukaa madarakani na unarudisha Bunge lilelile. Hata tukipata mbunge mmoja tutamtumia huyo huyo kutetea masilahi ya Watanzania ikiwemo changamoto ya migogoro ya ardhi," ameeleza Zitto.
Waziri Kivuli wa Fedha wa ACT Wazalendo, Kiza Mayeye amesema ziara hiyo si maagizo bali kuzungumzia changamoto za Watanzania kwa sababu siasa ndio maisha na wanasiasa wanaohusika kupanga mipango ya maendeleo.
"Hapa Katavi mmebarikiwa ardhi yenye rutuba ya kilimo, lakini bado mkoa huu wananchi wana hali ya umasikini.Licha ya kulima bado kilimo hakijawanufaisha," amesema.
"Siasa ni maisha lazima ifike mahali tuseme tunataka mabadiliko,wakati wa mabadiliko ndio sasa, tuungane tukaitoa CCM madarakani ili kubadilisha maisha ya Watanzania," amesema Mayeye ambaye ni Mwenyekiti ACT Wazalendo Mkoa wa Kigoma.
"Watu wa Katavi tuungane katika safari ya mabadiliko, msiogope twendeni tukapige kura atakayeshinda ndiye atakayetangazwa.Kigoma tutasimama imara atakayeshinda ndiye atakayetangazwa," amesema Mayeye ambaye aliwahi kuwa mbunge wa viti maalumu 2015/ 2020.