Mstaafu mfichwa maradhi anapoumbuliwa Kinondoni

Muktasari:
- Mstaafu wetu siku zote amekuwa akiamini maneno ya wahenga wetu kuwa, mficha maradhi kifo kitamuumbua, lakini sasa kwa jibu la mheshimiwa wa siri-kali, yanapaswa kuwa, hata anayefichwa maradhi yake kama wazee walioahidiwa matibabu ya dezo, sasa Kinondoni itawahusu punde!
Siku chache zilizopita, mstaafu wetu wa Taifa, amemsikia waziri wetu mmoja wa siri-kali akijibu swali lililoulizwa bungeni kuhusu wazee na likamfanya kuamini kweli sasa matibabu ya bure kwa wazee wa miaka 60 na zaidi, yameishia kuwa maneno kwenye kanga tu.
Mstaafu wetu siku zote amekuwa akiamini maneno ya wahenga wetu kuwa, mficha maradhi kifo kitamuumbua, lakini sasa kwa jibu la mheshimiwa wa siri-kali, yanapaswa kuwa, hata anayefichwa maradhi yake kama wazee walioahidiwa matibabu ya dezo, sasa Kinondoni itawahusu punde!
Anayesemekana kuwa ni mwakilishi wa wapigakura bungeni aliuliza swali jema kiasi cha kumfanya mstaafu wetu kuamini swali lile lilipaswa kuulizwa wakati Bunge jipya likianza kazi miaka mitano iliyopita na sio wakati huu wa dakika za majeruhi wawakilishi wakijiandaa kuchapa yebo kurudi majimboni kutafuta kura, huku kila mmoja akijitahidi kuuliza maswali yatakayowagusa wananchi ili aweze kujitwalia kura ili ale milioni 14 kwa mwezi!
Asemekanaye ni mwakilishi wa wananchi aliuliza swali jema, lakini lililochelewa, kwamba siri- kali ilikuwa na mpango gani kuhakikisha wazee wanapata matibabu nafuu kwa maradhi yao ya kiutu uzima ikiwamo kisukari ambao sijui kwa nini tuliuita ugonjwa wa kisukari wakati ni uchungu mtupu!
Lilikuwa ni swali nzuri, mbali ya kwamba kuiuliza siri-kali swali kama hili wakati tayari ilikuwa imefanya matibabu ya bure kwa wazee wa Taifa wa zaidi ya miaka 60 kuishia kuwa maneno ya kanga, tena kanga ambayo maneno hayaonekani!
Ndio ilivyokuwa, jibu la mheshimiwa mhusika wa siri- kali halikuwa na jipya, sana sana likawa limekwenda mbele zaidi na kuwafanya wazee wa zaidi ya miaka 60 na wastaafu wenzao kuwa wafichwa maradhi, sio waficha maradhi, ambao Kinondoni itawaumbua!
Badala ya mheshimiwa mhusika kutaja nafuu ya matibabu ya wazee kuhusu maradhi yao, yeye akatoa maelezo maelfu ya jinsi siri-kali ilivyokuwa imeweka utaratibu mpya wa kuwa na vifurushi kadhaa tofauti tofauti anavyoweza kununua mzee wa Taifa wa miaka 60 na zaidi, kwa mujibu wa maradhi yake.
Sio unafuu wa bei wala urahisi wa gharama za kutibu maradhi yake maana matibabu ya bure kwa wazee w Taifa hili yameishia kuwa kitambaa cha deki!
Vifurushi hivyo vilivyowekwa na siri-kali kumsaidia mzee wa Taifa hili wa miaka 60 na zaidi, havijatoa nafuu yoyote kwa mstaafu wa kima cha chini anayepokea pensheni ya Sh110,000 kwa mwezi ambaye ili kutibiwa maradhi yake mengi ya kiutu uzima, dawa za bei mbaya sasa anapaswa kununua mwenyewe kwa pensheni yake njiwa au akamatane na watoto wake ambao bado wanaitafuta ajira kwa tochi wamnunulie!
Narudia tena, hakuna nafuu yoyote kwenye vifurushi vilivyotajwa na siri-kali, maana bei ya dawa ni ile ile, uamue kununua kifurushi kilichopangwa na siri-kali au uinunue kwenye duka la dawa uliolekezwa kwa kidole na daktari wa hospitali ya siri- kali.
Kweli mficha maradhi kifo kitamuumbua, lakini inasikitisha zaidi kuwa mzee mfichwa maradhi na vifurushi vya bima ya afya, Kinondoni itamhusu punde!
Inashangaza unapoambiwa binadamu wote ni sawa wakati wewe mzee unapambana na pensheni yako ya Sh110,000 kununua kifurushi cha matibabu yanayostahili maradhi yako lakini kuna mstaafu mwenzako ambaye anapoumwa mafua au kikohozi tu, siri- kali inamsafirisha yeye na mwenza wake hadi Ujerumani au Uingereza ama India kutibiwa mafua! Hata hospitali zetu ni kayumba sasa.
Kweli binadamu wote ni sawa lakini kuna binadamu wengine wako sawa zaidi kuliko sisi walala hoi! Hakika kwa hali hii, mabadiliko yanakuhusu.
0754 340606 / 0784 340606