Mgawo wa maji watikisa mijini, vijijini

Muktasari:

  •  Licha ya wingi wa rasilimali maji zilizopo nchini, upatikanaji wa maji safi na salama, bado ni changamoto kwa wananchi ambao baadhi hupata maji kwa mgawo, huku wengine hasa vijijini wakitegemea vyanzo asili visivyo salama.

  


Mikoani. Licha ya wingi wa rasilimali maji zilizopo nchini, upatikanaji wa maji safi na salama, bado ni changamoto kwa wananchi ambao baadhi hupata maji kwa mgawo, huku wengine hasa vijijini wakitegemea vyanzo asili visivyo salama.

Uchunguzi wa Mwananchi katika mikoa ya Mara, Mwanza, Geita, Kilimanjaro, Morogoro, Dodoma na Dar es Salaam, umebaini hali si shwari licha ya mikakati mingi ya Serikali ya kuhakikisha huduma hiyo inasambaa nchini kote.

Katika mikoa hiyo, huduma ya maji safi na salama, hasa katika wilaya za vijijini ni asilimia 47, huku wastani wa kitaifa ikiwa ni wastani wa asilimia 74.5 hadi kufikia Aprili, mwaka huu, hali inayosababisha mgawo wa maji mara moja hadi mbili kwa wiki.

Kiwango hicho ni ongezeko la zaidi ya asilimia mbili kulinganisha na wastani wa asilimia 72.3 ya mwaka 2021, hali inayoashiria kuna uwezekano wa kufikia lengo la maji kupatikana kwa asilimia 85 vijijini ifikapo mwaka 2025.

Kwa mujibu wa hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara ya maji kwa mwaka wa fedha 2022/23, hadi kufikia Aprili, 2022 hali ya upatikanaji wa huduma ya maji mijini ilikuwa ni wastani wa asilimia 86.5 ikilinganishwa na asilimia 86 ya mwezi Machi 2021 huku lengo ikiwa ni kufikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2025.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam walisema kutopatikana kwa huduma ya uhakika ya maji, siyo tu unasababisha watu kutumia muda mwingi kusaka maji badala ya uzalishaji, bali pia ni tishio la kiafya kutokana na baadhi ya watu kutumia maji yasiyo salama.

“Maji yanatoka kwa mgawo asubuhi au jioni mara mbili kwa wiki; na yakitoka tunaacha kila kitu ili tukinge na kuhifadhi maji ya kutosha kwa siku mbili hadi tatu,” alisema Latifa Khalfan, mkazi wa Tabata Magenge.

Kwa mujibu wa tovuti ya mkoa wa Dar es Salaam, mahitaji ya maji kwa wakazi wa mkoa huo ni wastani wa lita milioni 544 kwa siku huku uwezo uliopo kwa sasa ni kuzalisha lita milioni 504 yanayokidhi mahitaji kwa asilimia 72 kwa wastani wa saa 16 kwa siku.

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Jamii wa Dawasa, Nelly Msuya alisema hakuna mgawo wa maji kwani kwa sasa mitambo inazalisha maji kama kawaida.

“Hapo nyuma tulikuwa na changamoto ya umeme, unajua sisi tunazalisha maji kwa kutumia umeme, kwa hiyo kipindi kile kweli kulikuwa na changamoto ya umeme, lakini kwa sasa hivi hakuna shida,” alisema.

Kero ya mita, bili kubwa

Mkazi wa Tabata Mawezi, Cecilia James alisema yeye na wapangaji wenzake wanne wanatumia uniti saba za maji kwa mwezi huduma ya maji ikipatikana kila siku, lakini inapofika mwisho wa mwezi wanapokea ankara kubwa kulinganisha na matumizi yao hata kipindi ambacho kuna mgawo wa maji.

Kilimanjaro nako si shwari

Upatikanaji wa maji katika wilaya za mkoa wa Kilimanjaro pia siyo wa kuridhisha ambapo kwa mujibu wa takwimu maeneo ya vijiji vya mkoa huo, upatikanaji wa huduma unafikia wastani wa asilimia 84.

Kwa mfano, wakazi wa Wilaya ya Same wanapata huduma ya maji kwa asilimia 42 wakati wenzao wa Wilaya ya Mwanga wakihudumiwa kwa asilimia 56 huku Wilaya ya Rombo upatikanaji wa huduma ya maji ni asilimia 57 pekee.

Rahel Moiso, mkazi wa Holili Wilaya ya Rombo alisema, huduma ya maji eneo la mpakani mwa Tanzani na Kenya hupatikana kwa mgawo wa mara moja au mbili kwa wiki.

“Tunapofuatilia kwa mamlaka husika tunajibiwa kuwa kuna upungufu wa maji kwenye vyanzo vilivyopo; ni vema Serikali ivalie njuga suala la maji kutuondolea adha hii,” alisema Rahel.

Meneja Wakala wa Maji safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Mkoa wa Kilimanjaro, Weransari Munisi aliiambia Mwananchi Serikali inaendelea kutekeleza miradi kadhaa mkoani humo kukabiliana na tatizo la maji.

Maeneo mengine ya nchi

Wakazi wa Jiji la Mwanza, hasa maeneo ya pembezoni ikiwemo mitaa ya Mahina, Buhongwa, Pasiansi, Nyasaka, Buswelu, Nyakato National na maeneo mengi ya Wilaya za Ilemela na Nyamagana, kwao huduma ya maji hupatikana kwa mgawo wa mara moja au mbili kwa wiki.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa), Leonard Msenyete alisema Serikali inatekeleza miradi kadhaa ikiwemo ya upanuzi wa chanzo cha maji na tiba eneo la Butimba unaogharimu zaidi ya Sh69 bilioni.

Changamoto kama hizo pia ziko katika mikoa ya Morogoro na Geita, ambako viongozi wa Serikali wameeleza mikakati wanaoifanya kutatua changamoto hiyo.

Mikakati ya Serikali

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi amekubali kuwepo kwa tatizo la upatikanaji wa maji, akitaja ukame kuwa chanzo cha changamoto hiyo katika baadhi ya maeneo nchini.

Hali hiyo ya ukame, alisema inatokana na msimu wa kiangazi uliopo.

“Sasa hivi ukame wa kuuliza kweli” kwani hujui tupo kwenye kipindi gani, hiki si kiangazi? Sijajua hilo tatizo (changamoto ya maji) kwa kiasi hicho,” alisema.

Agosti 6 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan alisema anatambua matatizo yanayowakabili kina mama kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya maji, hivyo Serikali itahahakikisha mpaka kufikia mwaka 2025 tatizo la maji nchini linakuwa limekwisha.

Alitoa kauli hiyo wakati akizindua mradi wa maji katika kata ya Makongorosi Wilaya ya Chunya wenye thamani ya Sh2.5 bilioni utakaozalisha maji lita milioni mbili kwa siku.

Naye Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema Serikali inatekeleza malengo ya kuhakikisha huduma ya maji yanapatikana kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo 2025.
“Maji hayana mbadala, ni lazima maji yapatikane popote yalipo bila kujali gharama...’’ alisema.