Prime
Hofu yatanda kwa watia nia CCM

Muktasari:
Kuchukua na kurudisha fomu ni jambo moja, lakini kupenya katika mchujo na kuwa kati ya watatu watakaopigiwa kura za maoni na wajumbe, ni jambo lingine.
Dar es Salaam. Kuchukua na kurudisha fomu ni jambo moja, lakini kupenya katika mchujo na kuwa kati ya watatu watakaopigiwa kura za maoni na wajumbe, ni jambo lingine.
Hilo ndilo linalowaweka matumbo joto maelfu ya makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), waliochukua fomu kuomba ridhaa ya chama hicho kuwania nafasi za udiwani, ubunge na uwakilishi kwa Zanzibar.
Kwa mujibu wa watia nia hao, mchakato unaokuja na matokeo ya majina matatu ndiyo unaohofiwa zaidi, kwa kuwa vikao vyake vinahusisha mamlaka za juu za chama hicho, ambazo aghalabu ni vigumu kuzifikia wala kuzichezea kile walichokiita sarakasi, ukilinganisha na wajumbe.
Hofu na wasiwasi zaidi unatokana na kile kilichoelezwa na watia nia hao kuwa makada wengi wenye sifa stahiki wamechukua fomu, na viongozi mbalimbali wa chama wamekuwa wakitoa msisitizo wa miiko, na imekuwa vigumu kuwatabiri iwapo wanamhitaji nani.
Kutokana na hofu hiyo ya kutokurudi majina, baadhi wamefikia hatua ya kuwafuata hadi wakuu wa mikoa kuwashawishi kwa kuwapatia chochote kitu, ili watumie nafasi zao kujaribu kuwashawishi wajumbe wa kamati za siasa.
Mfano hai ni picha mjongeo kwenye mitandao ya kijamii inayomwonyesha Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, akizungumza mbele ya viongozi wa Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na wananchi kuhusu kushawishiwa na watia nia.
Amedai kuna wagombea wa kisiasa wamekuwa wakijaribu kumshawishi kwa fedha ili awawezeshe kushinda katika kura za maoni kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, akiwatolea mfano watu wawili bila kutaja majina yao na nafasi walizotia nia.
“Juzi watu wawili walikuja ofisini kwangu, dada yangu namheshimu mno, anasema anakuja kujitambulisha, anaona anisalimie, nikasema ‘karibu sana’. Lakini nagombea, akanipa na Sh5 milioni... ya nini? Sasa siwezi kuja kukusalimia Mkuu wa Mkoa halafu nikakuacha hivi hivi.
“Nilimjibu, ‘ulikuja vizuri lakini umeharibu.’ Nikamuuliza, ‘hata nikaichukua, nitaifanyia nini?’... Wewe unaongea na mwenyekiti wa mkoa vizuri, katibu wa mkoa, kwa hiyo kwenye kamati ya siasa pale utawashawishi… Nilimuomba atende matendo mema kama mtu wa Mungu,” alisema Paul Chacha.
Hofu za watia nia hao zinakuja katikati ya kipindi ambacho kamati za siasa, Julai 4 mwaka huu, zilianza vikao vya mchujo wa majina ya makada hao kwa ajili ya kupendekeza kwa mamlaka za juu.
Kamati za siasa za wilaya katika maeneo mengi zilihitimisha shughuli ya usaili kwa wagombea ubunge na udiwani. Hatua inayofuata ni ngazi ya mikoa kuanzia Julai 9 na 10 ambapo vikao vya kamati za siasa za mkoa vitafanyika, huku vikiwa na kazi ya kuteua wagombea wa udiwani na udiwani wa viti maalumu wasiozidi watatu, watakaopigiwa kura ya maoni na wajumbe.
Pia, kamati za siasa zitawajadili wagombea wa ubunge na uwakilishi na kutoa mapendekezo kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa Tanzania Bara na Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar, kwa upande wa Zanzibar.
Vikao vya kamati za siasa vitaendelea kwa ngazi na tarehe tofauti, na mwisho Julai 17 na 18, Sekretarieti ya Halmashauri Kuu itaketi, na kuhitimishwa na Kamati Kuu itakayoketi Julai 19 kutoa orodha ya majina hayo matatu katika kila jimbo na nafasi za viti maalumu.
Vikao hivyo kwa ujumla wake, vitakuwa na kibarua cha kujadili majina ya makada 5,475 wanaotaka ubunge na uwakilishi kwa maana ya Bara na Zanzibar. Hofu hiyo pia itawakabili watia nia zaidi ya 15,000 wa udiwani.
Hata hivyo, CCM kupitia Katibu wake wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, kilishazielekeza kamati za siasa kutenda haki na zisionee watu katika vikao vya mchakato wa mchujo kwa watia nia walioomba kugombea udiwani na ubunge, ili kupunguza malalamiko na manung’uniko.
“Kamati za siasa za mkoa, kwa ratiba ya chama, zitaanza kukaa Julai 9, 2025 kuanza kufanya uteuzi wa mwisho kwa wanaoomba nafasi za udiwani, lakini uwakilishi na ubunge, uteuzi wa mwisho utafanywa na Kamati Kuu kuanzia Julai 19, 2025.
“Katika uteuzi huo tutapata wagombea watatu, na kwa namna wanawake walivyotokeza, tutazingatia jinsia,” alisema.
Makalla alisema mchakato wa mwisho kwa waliotaka udiwani utafanywa na ngazi ya mkoa, lakini kwa uwakilishi na ubunge, Kamati Kuu ya chama itafanya uteuzi huo.
“Wakati wa shughuli hii, kamati za siasa zitende haki, mgombea apatikane kwa kuzingatia sifa na uwezo. Wale wenye orodha waziweke kando ili kupunguza minong’ono,” alisema.
Makalla alisema ni muhimu vikao vyote vya mchujo na uteuzi vitende haki kwa makada wote na wasionewe kwa fitina au majungu.
“Tukatende haki, tuteue watu kwa haki na tusionee mtu. Tunapokwenda kwenye uchaguzi tuna mengi ya kusema, ikiwemo ilani, lakini yote yatanogeshwa tukiwa na wagombea wazuri,” alisema.
Wanachosema watia nia
Ingawa ana uzoefu wa kuhudumu kwa vipindi kadhaa bungeni, mmoja wa watia nia aliyeomba hifadhi ya jina lake amesema anashindwa kujiamini, hasa kutokana na idadi kubwa ya makada wenye sifa waliochukua fomu mwaka huu.
“Ukiangalia washindani wako, wapo wengine wana sifa kukuzidi na siyo mmoja, uzoefu ulionao unaishia hapo, unapata hofu kama hujawahi kuwa mbunge. Hiki ni kipindi cha hofu na wasiwasi,” amesema.
Mtia nia mwingine, ambaye pia ameomba hifadhi ya jina kwa sababu za kiitifaki, amesema hofu zaidi inatokana na kutotabirika kwa mazingira ya vikao vinavyopitisha majina matatu.
“Watia nia wengi huwa tunahesabu kupenya kwa wajumbe, lakini awamu hii mambo yanaanza kata, wilaya, Taifa, ndiyo urudi kwa wajumbe. Hivyo vikao vya mwanzo hadi Taifa havitabiriki kabisa, ndiyo maana tunapata hofu kubwa. Taifa hakuna kucheza sarakasi kama kwa wajumbe, unakatwa kama hawakujui,” ameeleza mtia nia huyo.
Kadhalika, amesema hofu nyingine inajengwa na matamko mbalimbali yanayotolewa na viongozi wa chama wakionya, kuzuia na kutoa marufuku kwa watia nia, akisema hiyo inamfanya ajihisi kuna mahali wamekosea.
Mtia nia mwingine wa ubunge amesema, pamoja na kwamba kinachofanyika kinaongeza utoaji haki, kiuhalisia kimeongeza hofu kwa watia nia kuliko wakati mwingine wowote.
“Hakuna kuzichanga karata siku hizi. Hivi navyokwambia haijawahi kupita siku sikwenda (nyumba ya ibada kusali), familia yangu inasali. Hofu imejaa kwa familia nzima,” amesema.
Amekwenda mbali zaidi na kueleza kuwa angalau uwe mtia nia mpya ukikatwa siyo tatizo, tofauti na mkongwe, akisema hatua ya mbunge mzoefu kukatwa inamaanisha chama hakikuridhishwa na kazi yake.
Aprili 24, 2025 akiwa jijini Dodoma katika Wilaya ya Kongwa, Mkoa wa Dodoma, kwenye muendelezo wa kukagua utekelezaji wa Ilani na uhai wa chama hicho, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, pamoja na tambo za wabunge kurudi bungeni, alisema msimamo wa chama hicho ni kuwasikiliza wananchi ili wapate mtu anayekubalika na wote.
“CCM safari hii hatutaki kujichosha, hatutaki kubeba mizigo. Kama umepakia kwenye mkokoteni halafu unasukuma, hatutaki… Mnasema Ndugai mitano tena, Simbachawene mitano tena – je, wanakubalika? Lakini uamuzi wa mwisho ni wa wajumbe,” alisema Wasira.
Alijenga hoja hiyo baada ya mbunge wa Kongwa, Spika mstaafu Job Ndugai, na mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene ambaye pia ni Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, kueleza kuwa watajitosa tena kutetea ubunge. Wawili hao wamechukua fomu.
Wasira alisema chama hicho kinahitaji kushinda uchaguzi kwa kishindo, na ili kifanikiwe, ni lazima kipate makada wanaokubalika kwa wananchi hata akisimama, wote wanasema “mwenzao.”
Wakili Leonard Manyama, aliyetia nia kugombea ubunge wa Kawe, amesema pamoja na kwamba watia nia wanaohitaji nafasi hiyo wapo 38, lakini hana hofu.
“Nimeshajijenga kisaikolojia, watia nia tuko wengi kama 38 na najua anayetakiwa ni mmoja kati yetu. Chochote kitakachofanyika tutaheshimu utaratibu na uamuzi wa kikao,” amesema.
Kwa mujibu wa Manyama kwa kuwa anaomba ridhaa ya kuwatumikia wananchi hawezi kuwa na hofu yoyote. “Siwezi kuwa na hofu kwa sababu si biashara.”
Wakili Manyama amesema kwenye vikao hivyo wapo watu wanaotoa uamuzi wa kina nani wanapaswa kurudi, na jina lake likirudi atashukuru Mungu.
“Lisiporudi jina langu, nitashukuru Mungu. Nitakuwa tayari kuunga mkono jina litakalokuwa limepenya, kwa sababu katika wote waliojitokeza, anapaswa kupatikana mmoja ili chama kishinde,” amesema.
Mmoja wa watia nia mara ya pili katika Mkoa wa Kagera amesema: “Jana (Jumapili) tulifanyiwa usaili. Alikuwa anaingia mmoja mmoja na tulimaliza salama. Sasa sijajua huko juu wakirudisha majina, langu kama litarudi, ingawa najiona nikirudi.”
Aidha, amesema amezungumza na wenzake kwenye majimbo mengine na ameelewa baadhi ya watia nia wameitwa kwenye vikao vya mkoa. “Nafikiri kuna kitu wanakihitaji zaidi kwa hao wagombea.”
Hofu kwa viongozi wa kamati
Pamoja na kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ndiye Mwenyekiti wa CCM na mwenye uamuzi wa juu zaidi kuhusu kumpitisha au kutompitisha mgombea, hofu ipo kwa baadhi ya viongozi wa kamati za maadili na Kamati Kuu ambao wanawajua mienendo yao.
Wamesema baadhi ya viongozi hao, licha ya uungwana wao, ni wafuatiliaji, wanawajua makada wa CCM kuanzia udhaifu wao hadi turufu walizonazo, na ni wazoefu ndani ya chama hicho.
Wamesema viongozi hao, kwa misimamo yao, hawawezi kuruhusu wapitishwe wagombea kwa huruma mbele ya mwenye vigezo na msafi.
“Sasa kwenye maisha yetu ya siasa haya, kuna wakati pengine uliteleza, kwa hiyo unashindwa kujua kama kosa ulilowahi kufanya litakuhukumu au vipi. Ni hofu tupu,” ameeleza.
Mtia nia mwingine amesema hofu yake inatokana na uzoefu walionao viongozi hao wa Kamati ya Maadili na Kamati Kuu, na uadilifu wao utakaofanya wadhibiti kila mwenye kasoro na kusimamia haki ili mwenye haki apate na asionewe.
“…ni kama fagio la chuma. Ukweli wananipa hofu, na wenzangu wengi wanamtaja taja yeye (wanamtaja mmoja wa viongozi hao). Kama unavyomuona anaongea huku anatabasamu, ndivyo hivyo hivyo atakavyokukata huku akitabasamu. Hapendi makandokando na ana mtandao mpana wa kujua mambo na wanachama,” ameeleza.
Tukubaliane na matokeo
Mtia nia mwingine amesema CCM ni chama kikubwa, ndiyo maana watu wengi wamejitokeza, hivyo amewataka wagombea wenzake katika mchakato kuwa tayari kupokea matokeo ya aina yoyote.
“Mngombea watu watatu na katika mchakato mnakuta wote mna sifa za kuwa wabunge, lakini vile kanuni zinataka mapendekezo ya watu watatu, inabidi mkubaliane na matokeo.
“Usipokuwamo kwenye watu watatu, inabidi mkubaliane na matokeo maana huu mchakato si wa kufa na kupona,” amesema mmoja wa watia nia wa ubunge.
Imeandikwa na Juma Issihaka, Bakari Kiango na Tuzo Mapunda