Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watia nia, wajumbe CCM waonywa

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  Mkoa wa Mwanza, Omary Mtuwa akizungumza na waandishi wa habari, leo ofisini kwake jijini Mwanza. Picha na Damian Masyenene

Muktasari:

  • Mchakato wa uchukuaji fomu ulihitimishwa jana Julai 2, 2025, kesho Julai 4 hadi 29, 2025 vikao vya kuchuja watia nia vitaanza rasmi ili kupata wateule katika nafasi hizo.

Mwanza. Baada ya kukamilika kwa mchakato wa uchukuaji fomu za kuomba ridhaa ya kugombea nafasi mbalimbali ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, watia nia wametakiwa kuwa watulivu, huku wanachama, wakihimizwa kusubiri maelekezo ya chama.

Mchakato wa kuchukua fomu ulifungwa rasmi jana Julai 2, 2025. Kuanzia Julai 4 hadi 29, 2025, vikao vya kuchuja majina ya watia nia vitaanza ili kupata wagombea watakaoteuliwa kupeperusha bendera ya chama kwenye nafasi hizo.

Mkoa wa Mwanza una majimbo tisa ya uchaguzi, tarafa 24, kata 191, matawi 918, vijiji 545, mitaa 346, vitongoji 3,445 na mashina 13,829.

Wito huo umetolewa leo Alhamis Julai 3, 2025 jijini Mwanza na Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Omary Mtuwa wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu mchakato huo.

Amewataka wanachama waliokamilisha hatua ya kuchukua fomu kuheshimu Katiba, kanuni na miongozo ya chama na kuonya dhidi ya vitendo vya rushwa kwa kuwa chama kitachukua hatua kali kwa watakaobainika kufanya makosa hayo.

“Mpaka sasa kuna amani, hakuna tatizo lolote linalohatarisha uhai wa chama chetu. Lakini katika kipindi hiki tunasisitiza waliochukua fomu watulie na wale ambao ni wapiga kura wasubiri maelekezo ya chama kuhusu kinachofuata,” amesema Mtuwa.

Amesema mpaka kazi hiyo inahitimishwa jana, wanachama wengi walijitokeza kuomba ridhaa ya kugombea, jambo linaloashiria chama kinaungwa mkono kwa kiwango kikubwa.

“Hamasa ilikuwa kubwa. Mkoa wetu wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa yenye mwitikio mkubwa. Tuna makundi mengi yaliyoshiriki kwa ari kubwa. Bila shaka wakati ukifika, chama kitaamua nani anafaa kupeperusha bendera katika nafasi hizo,” amesema na kuongeza;

Kwa upande mwingine, Steven Joseph, mmoja wa vijana waliyojitosa kwenye mchakato huo katika Jimbo la Nyamagana, amesema mchakato ulikuwa wa haki na umewezesha wanachama wa rika zote kuonyesha dhamira yao ya kukitumikia chama na wananchi.

Hata hivyo, ameunga mkono kauli ya chama Mkoa wa Mwanza kuwa hatua inayofuata nayo iwe ya haki kwa makada wote.

“Tuachane na vita vya kisiasa vya maslahi binafsi ndani ya chama. Hii inaturudisha nyuma. Nchi nyingi za Afrika zimeshindwa kusonga mbele kwa sababu ya migogoro ya wenyewe kwa wenyewe. Tuungane kama mnyororo na tujenge Tanzania moja,” amesema Joseph.

Naye kada mwingine wa CCM, Dk Hamidu Ibrahim amepongeza utaratibu mzuri na wa haki uliowekwa na chama chao kwa wanaotaka kuwatumikia Watanzania na ametoa wito kwa chama kuongeza umakini zaidi kwenye hatua za uchujaji wa wagombea.

“Nashukuru kwa utaratibu ulivyowekwa na Chama, ni mzuri sana; tulipokelewa vizuri, tukachukua fomu, tukajaza na kurudisha. Sasa kinachofuata ni vikao vya uteuzi, naomba nao uwe wa haki na sawa kama tulivyoanza,” amesema Dk Ibrahim.