71 wafutiwa matokeo kidato cha sita, ualimu, 244 yazuiliwa

Muktasari:
- Katika matokeo ya kidato cha sita, ufaulu wa jumla ni asiliamia 99.95 kwa watahiniwa 126,135 waliofanya mtihani sawa na ongezeko la asilimia 0.03.
Unguja. Baraza la Mitihani la Tanzania limefuta matokeo ya watahiniwa 71, wakiwemo 70 wa mtihani wa kidato cha sita na mmoja wa ualimu daraja A (GATCE).
Akitangaza matokeo hayo leo Julai 5, 2025 katika ofisi za baraza hilo Zanzibar, Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Profesa Said Mohamed amesema matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa kifungu cha 5(2) (i) na (j) cha shera ya baraza la mtihani sura ya 107.
“Kifungu hiki kinasomwa pamoja na kifungu cha 30 (2) (b) cha kanuni za mitihani za mwaka 2016,” amesema.
Kwa mujibu wa Profesa Mohamed, baadhi yao waliingia na simu, saa janja kwenye vyumba vya mtihani na kusaidiana kwenye mtihani.
“Ni udanganyifu umefanywa na watahiniwa wenyewe, baadhi yao wamesaidiana kwenye chumba cha mtihani, kuna walioingia na simu, smart watch, baadhi yao wameingia na karatasi zenye majibu kinyume cha sheria,” amesema.
Ameongeza: “Baadhi yao tumewakuta katika karatasi za kujibia wana miandiko inayofanana na kuona mfanano ambao sio wa kawaida, hivyo huo nao ni udanganyifu kinyume cha sheria.”
Amesema mbali na adhabu ya kufutiwa matokeo, pia watatoa elimu kuacha udanganyifu huo.
Pia Baraza hilo limezuia matokeo ya watahiniwa 244 wakiwemo 235 wa mtihani wa kidato cha sita na wanne wa mtihani wa ualimu Daraja A (GATCE) na watano mtihani wa stashahada ya ualimu wa sekondari (DSEE).
Sababu za kuzuia matokeo hayo, amesema kuwa baadhi walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani kwa masomo yote au idadi kubwa ya masomo.
“Watahiniwa husika wamepewa fursa ya kufanya mtihani kwa masomo ambayo hawakuyafanya kwa sababu ya ugonjwa mwaka 2026 kwa mujibu wa kifungu cha 32 (1) cha kanuni za mitihani,” amesema.