Akaunti benki ni suluhisho kutopotea fedha za vicoba

Muktasari:

  • Jambo hili hutokea kwa sababu wengi hukaa nazo nyumbani jambo ambalo huleta sintofahamu pindi zinapopotea.

Hivi karibuni kumekuwa na matukio mengi ya watunza hazina na viongozi wa vikundi vya vicoba kutumia fedha za wanachama wenzao jambo linalowarudisha nyuma na kuwakatisha tamaa.

Jambo hili hutokea kwa sababu wengi hukaa nazo nyumbani jambo ambalo huleta sintofahamu pindi zinapopotea.

Kwa kutambua mchango wa vicoba kwa wananchi wenye kipato cha chini kuna kila sababu ya taasisi za fedha kuangalia namna ya kuokoa jahazi. Elimu zaidi itolewe kwa wananchi kuepuka kukaa na fedha nyingi nyumbani.

Wengi hatujazoea kutunza kiasi kikubwa cha fedha na kutopata tamaa ya kukitumia. Kumpa mtu atunze fedha za kikundi bila kutilia shaka matatizo anayoweza kukutana nayo yatakayoshawishi kuzitumia fedha hizo ni kosa.

Baadhi ya taasisi, licha ya kuwa na huduma inayoweza kupunguza tatizo hili linaloisababishia jamii maumivu ya kiuchumi, hazijafika kwa wananchi wa chini kabisa na kuwashawishi kuzitumia.

Benki nyingi zina huduma nzuri kwa vikundi zinazotumia mawasiliano ya simu, lakini watu wengi hawazijui ingawa zikitumiwa vyema huenda ni suluhisho la upotevu wa fedha hivyo kuwahakikishia wanachama wa vicoba usalama wa fedha zao.

Takwimu zinaonyesha ni asilimia 17 tu ya Watanzania wote wana akaunti benki. Licha ya ukweli huu, utunzaji wa fedha za kikundi unapaswa kuwa ni kwa kutumia akaunti maalumu.

Hivyo, kupitia huduma inayowaruhusu wanachama kutumia namba zao za simu kupata taarifa, itasaidia kupunguza kama si kumaliza kabisa changamoto hii.

Tangu kuanzishwa kwa huduma hizo za kielektroniki mpaka sasa kuna idadi ndogo ya wateja ingawa inatia matumaini. Vicoba vikiongezeka na mchango wa sekta ya benki utakua.

Kuwa na akaunti ya kikundi kupitia huduma hizo inaelezwa ni lazima wanachama wote wawe wamesajiliwa kabla ya kufanya uamuzi wowote hasa wa kutoa fedha iliyotunzwa.

Kiongozi wa kikundi anatakiwa kuingiza jina la chama mathalan katika akaunti ya simu ya CRDB kwenye grupu la sim account na kuwaalika wanachama waweze kuliona na watapata namba maalumu ambayo wataitumia ama kujiunga na grupu hilo au la.

Ili akaunti hiyo ya kikundi iweze kutengenezwa ni lazima iwe na wanachama kuanzia watatu hadi 3,000 huku kiwango cha mwisho cha fedha inayoweza kuhifadhiwa kulingana na kanuni za Benki Kuu ya Tanzania kikiwa ni Sh50 milioni.

Ili kuepuka mgongano wa matumizi ya fedha za kikundi, kila mwanachama hupata taarifa kila anapotaka ikiwamo kujua salio lililomo katika akaunti na makusanyo yaliyofanyika kwa mwezi.

Wanachama pia wana uwezo wa kulipa ada na michango mingine waliyokubaliana moja kwa moja kutoka akaunti binafsi kwenda katika akaunti ya kikundi badala ya kuzipeleka kwa mtunza hazina.

Hata kwenye kukopeshana kama ilivyo kawaida ya vikundi hivi, utaratibu huwa tofauti na ilivyozoeleka kwani huku mikopo hutolewa kwa kupigiwa kura za ndiyo kulingana na idadi ya wanachama waliomo na makubaliano waliyojiwekea, vigezo na masharti ya mtu kupata mkopo.

Vipo baadhi ya vikundi huhitaji mkopaji apigiwe kura angalau na robo tatu au nusu ya wanachama ili apatiwe mkopo huo hivyo kupitia sim account wanaweza kufanya hivyo.

Faida nyingine ni kwamba wanachama wanaweza kufungua akaunti ya akiba ndani ya akaunti yao ya kikundi wakiweka muda maalumu kuhakikisha wanatimiza malengo waliyojiwekea.

Kadri teknolojia inavyokua mambo mengi yanakuwa rahisi, hakuna haja tena ya kukusanya fedha kwa mwenyekiti au kumkabidhi mtunza hazina badala yake zinawekwa moja kwa moja katika akaunti ya benki.

Benki zinapaswa kuwaelimisha wananchi kuhusu huduma walizonazo ili kupunguza uhalifu.

Aurea anapatikana kwa namba 0785 541 710.