Bei za huduma ya afya zidhibitiwe, ni chanzo cha umaskini nchini

Muktasari:

  • Watafiti wa maswala ya afya wanatahadharisha hali hii itazidi kuwaongezea watanzania umaskini endapo hatua za makusudi hazitachukuliwa haraka iwezekanavyo.

Kukosekana kwa udhibiti dhidi ya gharama za matibabu na dawa kumeongeza mianya ya utoaji tiba kiholela katika vituo vya huduma za afya nchini.

Watafiti wa maswala ya afya wanatahadharisha hali hii itazidi kuwaongezea watanzania umaskini endapo hatua za makusudi hazitachukuliwa haraka iwezekanavyo.

Kwa miaka kadhaa sasa, watafiti pia wameendelea kuonya mwenendo wa utoaji huduma za afya katika vituo vya afya; hususani vya binafsi, umekuwa ukiongezeka kwa kasi zaidi lakini pia umezidi kugubikwa na utata.

Katika utafiti uliochapishwa na jarida na sera na mifumo ya afya (Journal of Health Policy and Systems Research), wataalamu wanasema kuna haja ya kubuni mbinu za kuwalinda wagonjwa dhidi ya bei ghali za matibabu; hususani zile zinazopangwa kiholela.

“Katika mazingira ambayo kuna ukuaji mkubwa wa sekta binafsi, ni muhimu sana kuweka mifumo ya udhibiti ili kuhakikisha kuwa sekta binafsi haikiuki misingi na haki za kijamii na pia kuilinda jamii dhidi ya gharama zinazoumiza,’’ inasema ripoti ya utafiti ya mwaka 2015.

Hadi kufikia leo hii, hali hii haijabadilika miaka kadhaa baada ya kuchapishwa utafiti huo.

Utafiti huo ulibaini changamoto mbalimbali ambazo huzikumba wizara za afya za nchi za ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika, hasa katika kudhibiti na kufanya ufuatiliaji wa gharama, huduma na mienendo ya hospitali na vituo binafsi vya afya.

Kuhusu gharama, ripoti hiyo ilibaini pia kuwa upatikanaji wa taarifa kutoka katika vituo vya binafsi ni mgumu.

Mmoja kati ya waliohojiwa katika utafiti huo alikaririwa akisema;

“Tatizo kubwa katika kudhibiti gharama za tiba na dawa hapa Tanzania ni upatikanaji wa taarifa kutoka kwa wamiliki wa vituo vya kutolea huduma za afya; vya binafsi. Mara nyingi hawatoi taarifa hizi.”

Ripoti hiyo pia ilibaini kuwapo na udhaifu katika kuwalinda walaji, wagonjwa au watumiaji wa huduma za afya.

Kwa mfano, hakuna taasisi maalumu na sheria madhubuti za kuwalinda wagonjwa na kudhibiti kabisa ulaghai au ukiukwaji wa utaratibu katika kutoa huduma.

Afrika Kusini ilitajwa kuwa nchi ya mfano wa kuigwa katika ripoti hiyo.

Ni nchi pekee kati ya zilizofanyiwa utafiti iliyokutwa na chombo mahususi na huru cha kudhibiti utoaji huduma za afya kwa njia ya bima.

Biashara katika magonjwa(disease-mongering) ya shamiri

Bishara katika magonjwa (disease mongering) ni swala lililo vuta hisia za mwandishi wa maswala ya sayansi Lynn Payer, katika kitabu chake kilicho baini jinsi madaktari, makampuni ya madawa na bima yanavyoweza kumshawishi mtu kutibiwa ugonjwa fulani, hata kama hapakuwepo na haja ya kumtibu.

Kwa lugha ya kiingereza, “Disease-Mongers: How Doctors, Drug Companies, and Insurers Are Making You Feel Sick.”

Yaani, unakuta mtu siyo mgonjwa, ila kwa sababu moja au nyingine, daktari au hospitali fulani wanafanya uamuzi wa kumtibu mtu huyo ili mradi wapate fedha.

Kumekuwapo na taarifa kutoka katika vituo mbali mbali vya afya hapa nchini zinaelezea ni jinsi gani watoa huduma za afya wanadiriki kutia chumvi taarifa zinazo elezea ugonjwa wa mtu fulani ili mradi wapate sababu ya kuongeza mapato au faida katika vituo vyao vya afya.

Uzoefu unaonyesha kuwa kadiri tasnia ya tiba inavozidi kukua, kuna msukumo pingamizi unaochagizwa na makampuni ya dawa na makampuni ya bima za afya katika kuwashawishi madaktari wanapokuwa wanafanya maamuzi juu ya tiba ipi apewe mgonjwa yupi na wakati gani.

Makampuni ya dawa yanazidi kujenga himaya zao katika kusambaza na kuuza bidhaa zao kwa mtindo huu.

Ili kuepukana na tatizo hili, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Faustine Ndugulile anasema Tanzania imeamua kuzindua mwongonzo mpya wa dawa na kuwataka wataalamu wote nchini kuufuata. Hii ikiwa ni suluhisho la muda mrefu(long-term solution).

‘Ninatambua kuwa kuna msukumo wa namna hii kwa madaktari wetu. Na mara nyingi, hawa wataalamu wetu hujikuta katika huu mtego. Sisi kama serikali tulichofanya ni kuzindua mwongozo mpya wa matibabu na kuhakikisha kuwa kila tabibu au daktari anaufuata kwa kutoa dawa zilizowekwa na mwongozo. Si vinginevyo,’’ anasema Dkt Ndugulile.

“Sisi kama serikali huwa tunafanya ukaguzi wa kushtukiza katika vituo mbalimabli vya afya katika kupambana na vitendo vya baadhi ya vutuo vya afya kutoa huduma zisizo endana na miongozo na mienendo ya taaluma. Kwa bahati mbaya kuna ma hospitali bado yanaendelea kukiuka maadili,’’ aliongeza katika mazungumzo na mwandishi wa habari hii.

Katika uzinduzi wa mwongozo mpya wa matibabu jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alitoa onyo kwa wataalamu wa afya kuhakikisha wanawapatia dawa wagomjwa kwa kuzingatia miongozo iloiyowekwa na serikali.

Lakini je, hili ndiyo suluhisho?

Hili laweza kutatuliwa kwa ufasaha pale wataalamu wa afya watakapo kuwa tayari kufuata miiko ya taaluma. Lakini pia, wale wanaopatiwa huduma ni lazima wawe na uelewa juu ya haki zao wanapokuwa katika vituo vya kutolea huduma.

Kadiri muda unavyokwenda, inazidi kubainika kwamba asasi za kiraia au vyombo vingine ambavyo vinaweza kuingilia ili kulinda haki za walaji/wagonjwa zinahitajika nchini.

Mfumo wa bima za afya kuhujumiwa

Takribani miezi mitano iliyopita, shirika la taifa la bima ya afya (NHIF) lilitoa tahadhari juu uwepo wa wamiliki wa vituo vya huduma za afya wanaoghushi madai yao katika shirika hilo na hivo kuongeza gharama za matibabu kinyume na utaratibu.

Mkurugenzi Mtendaji wa NHIF Benard Kongwa alikaririwa na vyombo vya habari akisema, “Tunajua kuwa kuna baadhi ya vituo vya afya vinayotoa huduma duni lakini inapofika muda wa kudai malipo yao katika shirika letu la bima, wanaleta madai ya huduma za gharama kubwa. Hili halikubaliki kabisa,’’ alisema bwana Kongwa.

“Vitendo hivi vinaipotezea serikali mapato na pia kuhujumu hatua za serikali katika kupanua wigo wa kutoa huduma za bima ya afya nchini. Tumedhamiria kupambana nao,’’ alisema alipohojiwa na Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

Bima za afya zinadhibitika?

Kutokana na utata au ugumu(complexity) uliopo katika biashara za maswala ya tiba. Kumekuwapo na changamoto ya kudhibiti bei za madawa na gharama za matibabu nchini.

Kuna baadhi ya wadau wanaosema haiwezekani kudhibiti gharama hizi katika mazingira ambapo hakuna ulinganifu wa kibishara baina ya kampuni au taasisi za afya au makampuni ya bima mbalimbali.

Lakini, kamishna wa Mamlaka ya taifa ya Bima (Tira), Dkt Baghayo Saqware anaamini kunahitajika taasisi au mamlaka huru itakayoweza kudhibiti gharama zinazopangwa va vituo vya afya na pia kufanya ufuatiliaji wa huduma zinazotolewa na bima za afya nchini.

Si jukumu la Kamisha wa Tira kufuatilia maswala ya bima za afya lakini ni mdau wa bima kwa ujumla. Ushauri wake ni kwamba, kuwepo na udhibiti ili kuwalinda wanaopatiwa matibabu haya au huduma hizi dhidi ya gharama kubwa.

“Nakaa nikisali ili siku moja kuwepo na chombo kama hiki. Hii itatokana na mshikamano baina ya wadau na taasisi za serikali husika. Ikiwezekana hii, basi tutakuwa na mwelekeo mzuri katika kutimiza malengo wa upatikanaji huduma za afya kwa wote, yaani Universal Health Coverage (UHC).”