Friday, July 21, 2017

Busara ingetumika kushughulikia vituo vya kuuza mafuta

Kituo cha mafuta cha GBP kilichopo Barabara ya

Kituo cha mafuta cha GBP kilichopo Barabara ya Azikiwe jijini Dar es Salaam kikiwa kimesitisha kutoa huduma juzi Picha na Anthony Siame 

By Mwananchi

Jana na juzi, maeneo mbalimbali nchini yalikumbwa na kero kubwa ya upatikanaji wa mafuta aina ya dizeli na petroli, baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuanza kufunga vituo vilivyokuwa vinauza nishati hiyo bila kutumia mashine za kielektroniki za risiti zilizounganishwa na pampu.

Operesheni hiyo ilifanyika karibu nchi nzima na kusababisha baadhi ya wilaya, kama Igunga mkoani Tabora kukosa kituo hata kimoja kilichokuwa na mashine hizo na wakazi kulazimika kuyafuata wilaya jirani ya Nzega.

Katika miji mingi, vituo vichache vilivyokuwa na mashine hizo, vilijaa misururu ya magari, pikipiki na watu waliobeba vidumu kwa ajili ya kununua mafuta kutokana na maeneo mengi kutokuwa na huduma hiyo.

Ni wazi kwamba shughuli nyingi za kiuchumi juzi ziliathirika kutokana na kero hiyo. Wale waliotakiwa kuwahi ofisini kwa ajili ya kuendelea na shughuli za ujenzi wa Taifa, walilazimika kuchelewa na hivyo kuathiri utendaji katika maeneo yao ya kazi.

Wale waliotakiwa kusafirisha abiria, hawakuweza kufanya hivyo au walifanya kwa kiwango ambacho ni chini ya uwezo wao wa kawaida na hivyo kutopata kipato kinachostahili na hivyo hata mapato ya Serikali kuathirika.

Inawezekana kabisa kwamba hata shughuli ambazo mashine zake zinategemea nishati ya mafuta kufanya kazi, zililazimika kusimama kwa muda kutokana na ukosefu wa nishati hiyo.

Taarifa ya TRA kuhusu tatizo hilo ilisema kuwa mamlaka hiyo itaendelea kufunga vituo vyote visivyo na mashine hizo kwa kuwa wamiliki walishaambiwa tangu Agosti mwaka jana kuhusu kuweka vifaa hivyo vya kielektroniki vitakavyoiwezesha Serikali kudhibiti makusanyo ya kodi, tofauti na mashine za awali za EFD’s ambazo inadai zilikuwa zinaweza kutumika vibaya.

Ni dhahiri kuwa TRA iko sahihi kuwa muda iliyoutoa kwa wamiliki wa vituo vya mafuta unatosha kabisa, ingawa kunaonekana kuwapo mawasiliano mabovu kati ya wizara na wadau.

Wadau, hasa Chama cha Wamiliki na Wauza Mafuta kwa Rejareja (Tapsoa), kinasema kulikuwa na matatizo ya bei za mashine hizo awali kwa kuwa kampuni iliyopewa zabuni ya kuzileta iliweka bei ya juu tofauti na ile iliyoko sokoni.

Hoja yetu si malalamiko ya Tapsoa ambayo jana ilisema inahitaji angalau miezi mitatu kufunga mashine hizo, bali ni jinsi suala hilo lilivyotekelezwa.

Pamoja na ukweli kwamba kuuza mafuta ni kufanya biashara, hakuna ubishi kwamba shughuli hiyo pia ni huduma iliyo muhimu sana kwa jamii. Kutokana na umuhimu wa mafuta katika maisha ya kila siku ya mwananchi, TRA ilitakiwa itumie utaratibu ambao ni rafiki kwa mwananchi ambaye hauzi mafuta lakini anayategemea katika kuendesha maisha yake.

Serikali ilitoa agizo la kuweka mashine hizo takriban mwaka mmoja uliopita, lakini kutokana na mafuta kuwa huduma inayotegemewa na wengi, kulikuwa na umuhimu wa kutoa ilani angalau miezi mitatu kabla ya kueleza kuwa ifikapo tarehe fulani, vituo ambavyo vingekuwa havijafunga mashine hizo vingefungiwa.

Hii pia ingesaidia wananchi kujiandaa kwa hali hiyo badala ya kukutana nayo asubuhi wakati watu wakielekea kazini.

Pia, kutokana na ukweli kuwa bei za mashine hizo ni kubwa, kulikuwa na umuhimu wa Wizara kukaa pamoja na wadau kukubaliana njia za utekelezaji badala ya kutumia nguvu kila sehemu ambayo TRA inaona inalindwa na sheria. Ni muhimu kutanguliza busara katika masuala yanayoathiri wananchi.

-->