Elimu itolewe samaki wanaofaa kuuzwa sokoni

Muktasari:

  • Maofisa hao walikamata kilo mbili za samaki ambazo zilikuwa sehemu ya kilo 100 zilizonunuliwa na mfanyabiashara anayetoa huduma ya chakula bungeni hapo.

Juni 19, Watanzania walisikia na wengine kuona tukio la maofisa wa Serikali wanaoshughulikia masuala ya uvuvi wakifika katika mgahawa wa Bunge mjini Dodoma na kupima urefu wa samaki waliodaiwa kuvuliwa Ziwa Victoria.

Maofisa hao walikamata kilo mbili za samaki ambazo zilikuwa sehemu ya kilo 100 zilizonunuliwa na mfanyabiashara anayetoa huduma ya chakula bungeni hapo.

Maofisa wa Serikali waliamua kupima samaki hao kwa madai kwamba wanaofaa kuvuliwa ni wale wanaozidi urefu wa sentimita 25.

Tukio hilo lilivuta hisia za Watanzania wengi hasa baada ya mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Peter Serukamba kuwasilisha hoja akitaka apate maelezo juu ya tukio hilo.

Kwa kifupi suala hilo lilijadiliwa huku Serikali ikitoa maelezo ya ufafanuzi na hatua kadhaa zilizochukuliwa, lakini ukweli ni kwamba Watanzania wakiwamo wa mikoa ya Kigoma, Dar es Salaam na Mbeya bado linawakera na halijaeleweka.

Hali kadhalika hata baadhi ya maofisa uvuvi nao wanafanya kazi zao kwa ubabaishaji kuhusu samaki wa aina gani anayefaa kuvuliwa, kuuzwa pamoja na kuliwa na wananchi.

Nasema hivyo kwa sababu hivi karibuni maofisa uvuvi mkoani Dar es Salaam walizuia kuvuliwa na kuuzwa dagaa katika Soko Kuu la Feri kwa madai kwamba hawaruhusiwi.

Agizo hilo lilizua taharuki kwa wavuvi, wauzaji na walaji wa dagaa jijini hapo.

Vyombo vya habari viliripoti maelezo mbalimbali ya maofisa uvuvi pamoja na hoja za wananchi waliokuwa wakilalamikia kitendo cha kuzuiwa dagaa kuuzwa sokoni hapo.

Tukio hilo lilizusha mjadala katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na jijini Mbeya.

Je ni kweli dagaa wa baharini nao wamezuiwa kuvuliwa? Kama ni hivyo vipi dagaa kutoka Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na Ziwa Victoria?

Wote tunatambua kwa miaka mingi dagaa wako katika masoko mbalimbali na wanavuliwa kwenye maeneo mbalimbali yakiwamo ya baharini.

Pia wengi wanashuhudia kuzagaa kwa samaki wa ukubwa mbalimbali katika masoko karibu yote hapa nchini na namna walivyo na mvuto kwa wananchi. Kwa mfano soko la Soweto jijini Mbeya limejaaa samaki wa ukubwa tofauti kutoka bwawa la Mtera, Ziwa Rukwa na dagaa kutoka maeneo mbalimbali nchini. Je, maofisa uvuvi wametoa elimu gani kuhusu samaki na dagaa hao?

Ni wazi kwamba Serikali kwa miaka mingi imejikita kupambana na wavuvi haramu. Uvuvi haramu ni pamoja na wale wanaovua kwa kutumia baruti, mabomu na wanaomwaga dawa kwenye mito ili kuua samaki.

Wavuvi haramu ni wabaya na bila shaka wananchi wanaungana na Serikali kupambana nao, lakini maofisa uvuvi lazima watoe elimu ya kutosha kuhusu suala la kujua samaki wanaotakiwa kuvuliwa ama kuachwa.

Tabia ya maofisa uvuvi kuvamia kwenye hoteli na kupima urefu wa samaki au kwenda kwenye masoko kuzuia dagaa haina budi kukomeshwa kuanzia sasa.

Maofisa uvuvi ni lazima watambue dagaa ni dagaa kwa aina yake sawa na binadamu waliopo ambao ni wafupi wanaojulikana kama mbilikimo.

Pamoja na kutambua mambo hayo, maofisa uvuvi hawana budi kutoa elimu hiyo wakiwa kwenye maeneo ya uvuvi.

Kwa mfano, maofisa uvuvi wapige kambi kwenye maziwa ya Victoria, Nyasa, Tanganyika na mito mikubwa kutoa elimu ya aina ya samaki wanaotakiwa kuvuliwa.

Iwe ni mwiko kwao kuvamia kwenye hoteli au sokoni kupima samaki ama kuzuia kuuzwa samaki ambao wamevuliwa na kufikishwa kwa walaji.

0767 338897