Elimu ya kujitegemea, ufundi ni muhimu kuliokoa Taifa

Muktasari:

  • Pamoja na mambo mengine, taarifa ilieleza kwamba watu wasioweza kujitegemea ni wengi zaidi nchini.

Hivi karibuni, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alizindua taarifa ya makisio ya idadi ya watu nchini iliyoandaliwa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS).

Pamoja na mambo mengine, taarifa ilieleza kwamba watu wasioweza kujitegemea ni wengi zaidi nchini.

Taarifa aidha, ilionyesha kuwa Tanzania inakadiriwa kuwa na watu 54.2 milioni, huku ongezeko la kila mwaka likiwa ni wastani wa watu 1.6 milioni.

Katika uzinduzi huo, Dk Mpango alinukuu taarifa ya sensa na makazi ya mwaka 2012 akisema kiwango cha utegemezi kilionyesha kwamba Watanzania kati ya Watanzania 100 wenye umri wa miaka 15 hadi 64, wanategemewa na watu 92 wenye umri wa chini ya miaka 15 na wale wa zaidi ya miaka 65.

Kwa lugha nyepesi ni kwamba asilimi 92 ya Watanzania 100 hawana uwezo wa kujitegemea.

Hali hiyo ni tofauti na nchi zilizoendelea ambazo zinatajwa kwamba ni asilimia 40 tu ya watu wanaoishi bila kujitegemea katika kundi la watu 100.

Bila shaka Taarifa ya NBS na Waziri ina ukweli mtupu kwani wengi tumejionea hali ilivyo kwa maisha ya mijini na vijijini.

Wapo vijana wengi na wengine wenye afya nzuri na akili timamu, lakini ni tegemezi kwa wazazi.

Miongoni mwa vijana hao ni wasomi wa ngazi mbalimbali kuanzia za msingi hadi vyuo vikuu, lakini wanashindwa kupata mahali pa kuanzia kujitegemea kwa sababu ya mfumo wa maisha waliyoishi nao katika Serikali na nyumbani kwao.

Maisha ya miaka ya 1970 hadi 1990 katika elimu ya msingi hadi vyuo ni tofauti sana na maisha ya sasa kwenye sekta hiyo.

Kwa mfano, enzi za miaka ya 1970, shule zote za msingi zilikuwa na vipindi vya ufundi na kujitegemea kwa vitendo. Wanafunzi enzi hizo walijifunza hata jinsi ya kuchonga mipini, kutengeneza mikeka, ususi, kufuma vitambaa na pia walijifunza kilimo cha kisasa kwa vitendo.

Mimi kwa mara ya kwanza nilijifunza kilimo cha mahindi kupanda kwa sentiment 30 kati ya mhindi na mhindi na mstari mmoja hadi wa pili ni sentimita 90 nikiwa shule ya msingi.

Hali kadhalika, shule za sekondari nyingi enzi hizo zilikuwa na mashamba ya kujitegemea, kwani nikiwa sekondari, nilijifunza jinsi ya kulima bustani za mbogamboga na shamba la matunda mbalimbali.

Pia nakumbuka nikiwa kidato cha tano na sita ilikuwapo miradi midogomidogo ya kujitegemea ambayo ilichangia kutoa elimu ya jinsi ya kuishi.

Enzi hizo, licha ya kuwapo kwa shule za mfumo wa kilimo na biashara, pia palikuwa na shule za ufundi kama vile Ifunda, Iyunga, na Tanga ambazo zilisaidia kuwapata mafundi vijana katika maeneo mbalimbali nchini.

Bila shaka mfumo ule bado upo, lakini hauonekani matunda yake kwa sababu ya changamoto nyingi na tofauti ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi.

Ni kipindi mwafaka kwa Serikali ya Awamu ya Tano yenye kujenga taifa la viwanda kuamua shule zote za msingi vijijini zipatiwe walimu waliosomea kilimo.

Pia ipo haja kwa Serikali kutenga shule nyingi za sekondari ziwe za kilimo na ufundi ili kuwapata vijana wanaoweza kuanzisha miradi midogo

Pia ipo haja kwa Serikali kuanzisha vituo maalumu vya ufundi katika kila kata ili kuwapata vijana watakaosaida kuendeleza viwanda na watakaokarabati majengo ya umma yakiwamo ya shule na zahanati katika maeneo husika.