Fahamu haki zako kumiliki ardhi, uboreshe kipato na makazi yako

Muktasari:

  • Huwezi kuzungumzia makazi au nyumba bora kabla ya kujua zinajengwa wapi. Ukigusia madini utakuta bado ardhi inayobeba hayo madini inahitajika kabla ya kuchimbwa. Maji safi na salama hayawezi kupatikana mahali pengine popote isipokuwa ardhini.

Mwenye ardhi ndiye anayetunga sheria. Ardhi ni utajiri. Ni dhamana. Ni mali, urithi na moja kati ya rasirimali muhimu katika uchumi. Hii ni kwa sababu kabla hujaanza kuzungumzia kilimo, lazima uihusishe ardhi ambayo itakifanikisha hicho kilimo.

Huwezi kuzungumzia makazi au nyumba bora kabla ya kujua zinajengwa wapi. Ukigusia madini utakuta bado ardhi inayobeba hayo madini inahitajika kabla ya kuchimbwa. Maji safi na salama hayawezi kupatikana mahali pengine popote isipokuwa ardhini.

Huwezi kuzungumzia uchumi wa viwanda bila kwanza kuweka kipaumbele katika rasirimali adimu ya ardhi. Viwanda haviwezi kujengwa hewani ni lazima vijengwe ardhini, malighafi za kutumika viwandani zinategemea ardhi na, maendeleo na mafanikio ya ardhi yatategemea kwa sehemu kubwa namna wadau wanavyoitumia vizuri.

Utajiri wa mahali popote unategemea sana, pamoja na mambo mengine, namna watu wa eneo husika wanavyoweza kutumia ipasavyo rasirimali hii muhimu.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya mwaka 2002; ardhi inajumuisha nafasi ya juu ya ardhi pamoja na ile iliyopo chini yake na vitu vyote vilivyomo ndani yake isipokuwa madini au mafuta yaliyopo katika ardhi hiyo. Hii inajumuisha pia vitu vya asili vinavyoota au kuoteshwa katika ardhi hiyo, majengo pamoja na ardhi iliyofunikwa na maji.

Sheria hii inaeleza juu ya kanuni za msingi za sera ya ardhi ambazo ni pamoja na kutambua ardhi yote ya Tanzania ni mali ya umma ikiwa chini ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano kama mdhamini kwa niaba ya wananchi na kuhakikisha kuwa haki zilizopo au umiliki ambao umekuwepo tangu awali unatambuliwa na kulindwa.

Kuzingatia thamani iliopo kwa kila ardhi inayomilikiwa na mtu yeyote, kulipa malipo sahihi na halali kwa yeyote ambaye ardhi yake imechukuliwa na serikali kwa matumizi maalumu. Kuhakikisha uwapo wa mfumo makini, ulio wazi wa usimamizi wa ardhi na kuwawezesha wananchi wote kushiriki kufanya maamuzi katika mambo yahusuyo ardhi.

Kuna sheria nyingine zinazozungumzia ardhi kwa namna moja au nyingine lakini bado Katiba ndiyo mama na inatoa haki ya msingi ya mtu kumiliki mali ikiwa ni pamoja na ardhi. Jambo la kuzingatia ni kwamba, kila sheria inaeleza juu ya haki na wajibu ulionao ambao unapaswa kupata au kutimiza ili kupata haki zako. Kwa ujumla, kila sheria ipo kwa ajili ya kutetea na kulinda haki zako.

Unachopaswa kufahamu ni kwamba sheria hizi zipo na ujue jinsi ya kuitumia kila moja mahali ili kufanikiwa kupata na kuisimamia na kuifuatilia haki yako kwa mujibu wa sheria hizi. Ufahamu utakaokuwa nao utakufanya uchukue hatua thabiti zenye mwelekeo sahihi.

Kwa mujibu wa sheria za ardhi, kila raia wa Tanzania ana haki ya kumiliki ardhi. Ukimilikishwa ardhi si hisani bali ni haki yako ya kisheria na kikatiba. Hivyo kila mwananchi anapaswa kuamka na kuona ni jinsi gani ataweza kumiliki ardhi.

Mwenyezi Mungu ameipendelea sana Tanzania na kuipa ardhi tele ambayo kila raia wa kizazi cha sasa na kijacho anao uwezo wa kumiliki ardhi pasipo tatizo lolote. Tofauti na nchi zingine ambazo ardhi imeshaisha na hakuna fursa ya kuipata zaidi ya kutoka kwa mwingine anayeimiliki.

Sheria imeigawa ardhi katika makundi matatu ambayo ni ardhi ya akiba, ya kijiji na ya jumla. Ardhi ya akiba mara nyingi hutumika kwa shughuli za umma ikiwemo mbuga za wanyama, mapori ya akiba na maeneo yaliyotengwa kwa shughuli za kiserikali au kijamii. Ardhi ya kijiji ipo chini ya Serikali ya Kijiji na ardhi ya jumla ni ile iliyo chini ya halmashauri.

Kwa upande mwingine sheria ya ardhi imeweka bayana mtu hapewi haki ya kudumu ya umiliki wa ardhi bali hati ya haki ya upangaji wa ardhi kwa muda maalum au leseni ya makazi. Ndio maana hati zinazotolewa na serikali si za kudumu bali ni za miaka 33, 66 au 99 ingawa unaweza kuomba tena muda ukiisha.

Pamoja na kupatiwa muda huo wa kuitumia ardhi hiyo bado Rais anayo mamlaka ya kutengua au kufuta hati ya mtu yeyote kwa maslahi ya umma au endapo hutafuata masharti ya umiliki kwa mujibu wa sheria.

Wakati umefika Watanzania kumiliki na kutumia ardhi ipasavyo kwa shughuli za maendeleo, kila mmoja aamke na kumiliki ardhi. Haitakuwa na maana kama wengine watamiliki ardhi yetu wakati sisi tumelala na kubaki watazamaji. Miliki ardhi kwa manufaa yako na kizazi kijacho maana utajiri wote umefichwa huko.

Mwandishi ni wakili wa kujitegemea. Kwa maoni na ushauri anapatikana kwa namba 0755 545 600 au [email protected]