Faini kwa uzembe yamaliza tatizo la utapiamlo, maambukizi ya VVU

Muktasari:

  • Kijiji hicho cha Ikuna, hakina mtoto hata mmoja aliye chini ya umri wa miaka mitano mwenye tatizo la udumavu wala maambukizi ya VVU, japo wapo wazazi walio na maambukizi hayo.

Katikati ya Mkoa wa Njombe wenye changamoto ya udumavu na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), kuna kijiji kilichoweka rekodi ya aina yake kwa kufanikiwa kuwalinda watoto dhidi ya maradhi hayo.

Kijiji hicho cha Ikuna, hakina mtoto hata mmoja aliye chini ya umri wa miaka mitano mwenye tatizo la udumavu wala maambukizi ya VVU, japo wapo wazazi walio na maambukizi hayo.

Utafiti wa Tanzania Demographic Health Survey (TDHS), unaonyesha mkoa huo unashikilia nafasi ya pili kwa kuwa na asilimia 49.4 ya udumavu.

Lakini pia, Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika utafiti wake wa mwaka jana, unautaja Mkoa huo kuongoza kwa asilimia 11.4 ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.

Wakati karibu kila kijiji tulichobahatika kutembelea kikiwa na kati ya watoto wawili hadi wanne wenye utapiamlo, Ikuna hakukuwa na mtoto hata mmoja.

Kijiji cha jirani cha Nyombo, chenye mazingira sawa na Ikuna wapo watoto chini ya umri wa miaka mitano wenye utapiamlo na maambukizi ya VVU.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikuna, Ahazi Kihombo anasema si kwamba maambukizi ya VVU na utapiamlo kwa watoto hayakuwapo, laa. Yalikuwapo.

Anasema hayo yote yamewezekana kwa sababu ya umoja, ushirikiano na adhabu mbalimbali kwa familia zinazokiuka masharti ya malezi na lishe kwa watoto.

Muuguzi Mkunga wa Zahanati ya Ikuna, Anitha Mtitu anasema kati ya watoto zaidi ya 40 wa kijiji hicho waliofikishwa kliniki Desemba 22, 2017 hakuna aliyepatikana na utapiamlo.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) lilisema mkakati wake ni kuhakikisha watoto hao wanapatiwa nafasi ya kuishi na kuziomba nchi hizo ikiwamo Tanzania, kuwekewa mazingira ya kuokoa vifo vya watoto hao kutokana na ukweli kwamba wengi hufariki dunia ndani ya saa 24 baada ya kuzaliwa. Kwa mujibu wa Unicef, Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 duniani zenye viwango vya juu vya idadi ya vifo vya watoto wachanga duniani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ya Level & Trends in Child Mortality 2017, mwaka huo 2016, watoto wachanga 46,000 walifariki dunia nchini na kuifanya Tanzania kushika nafasi ya tisa kwa vifo hivyo.

Wakati Ikuna ikikosa mtoto mwenye utapiamlo, vijiji vya jirani kikiwamo cha Nyombo, wapo baadhi ya watoto wanaokabiliwa na hali hiyo licha ya kuwapo kwa chakula cha kutosha. “Watoto wote walikuwa kwenye rangi ya kijani kuonyesha afya zao ni nzuri, zamani hali haikuwa hivi. Ilikuwa mbaya sana,”anasema.

Waliwezaje kumaliza utapiamlo?

Hali mbaya ya utapiamlo na maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto iliwafanya viongozi wa kijiji hicho kutafuta suluhu ya nini wafanye kuokoa maisha ya watoto hao.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Kihombo anasema njia rahisi ilikuwa kutengeneza ushirikiano wa karibu baina ya Serikali ya kijiji, wahudumu wa afya wa zahanati, wahudumu wa afya ya msingi na wananchi.

“Tulikubaliana kushirikiana, muuguzi akigundua mtoto ana utapiamlo, anatoa taarifa kwa mhudumu wa afya ya msingi, inakuja kijijini na sisi tunaenda kuitembelea hiyo familia,”anasema Kihombo.

Anasema Serikali ya kijiji ikipata taarifa ya kuwapo kwa familia yenye tatizo la lishe kwa mtoto, wanaenda kuitembelea kujiridhisha n akubaini sababu zinazowafanya wazazi washindwe kumpatia lishe bora mtoto wao

Anasema kama wakibaini sababu ni hali ngumu ya uchumi ndani ya familia, kijiji kinakubaliana kuchanga fedha au chakula kwa ajili ya kuisaidia.

“Kwa hiyo hapo mwenye chochote anatoa, tunakusanya na kuwapelekea walezi wa mtoto husika tukiwasisitiza kuhakikisha mtoto huyo anarejeshewa afya yake,” anasema.

Ikiwa watabaini sababu ni uzembe, familia husika inatozwa faini ya Sh20,000 na inapewa masharti ya kuhakikisha mtoto aliyepatwa na utapiamlo anarejea kwenye afya yake.

Kihombo anasema faini hiyo ilisaidia kila mzazi mwenye mtoto aliye chini ya umri wa miaka mitano kuona wajibu wa kusimamia na kuhakikisha anampa mwanawe lishe bora badala ya kuendekeza shughuli za kilimo na kuwasahau watoto.

Mhudumu wa fya ya msingi wa kijiji hicho, Jafeth Ngimbudzi anasema kihalisia hali ilikuwa mbaya na kama kijiji kisingesimama kidete, mambo yangekuwa mabaya zaidi.

“Kwa hiyo, kazi yangu kubwa ni kuwatembelea nyumbani watoto wenye shida, kuwashauri wazazi na kuhakikisha wanawapatia watoto wao chakula bora,” anasema.

Muuguzi Mtitu anasema kila watoto wanapoletwa kliniki, jukumu lake kubwa ni kutoa elimu ya lishe bora kwa wazazi.

Anasema wengi hawajui makundi bora ya chakula ndiyo maana ilikuwa rahisi kwa mtoto kupata utapiamlo.

“Mzazi anamlisha mtoto uji asubuhi, ugali mchana na jioni kila siku, hapo anakuwa anamlisha chakula cha aina moja tu wakati uhakika wa kupata aina nyingine upo,” anasema.

Mratibu wa Lishe Mkoani Njombe, Ester Kibona anasema wanaendelea na hatua ya kuwahamasisha wazazi na walezi kufuga mifugo midogo kama bata, kuku na simbilisi kwa ajili ya kupata nyama na mayai kwa ajili ya lishe ya familia.

Hata hivyo, Unicef kupitia baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi chini ya Serikali, yamekuwa yakisaidiana na zahanati kuimarisha afya za watoto.

“Tunatamani kuiona Njombe isiyo na utapiamlo, hili litawezekana kama jamii yenyewe itakubali na kuona umuhimu wa kuwatunza watoto,” anasema.

Simulizi za udumavu kijijini

Baadhi ya wazazi na walezi waliowahi kupigwa faini au kusaidiwa wanasema bila sheria kijijini hapo pengine wangewapoteza watoto wao kwa uzembe.

Emiliana Lucheza mkazi wa Kijiji cha Ikunza anasema mtoto wake alizaliwa akiwa na kilo 3.5, lakini baadaye alipungua hadi kilo 1.5 kutokana na lishe duni jambo lililoufanya uongozi wa kijiji kuingilia kati.

“Mimi uchumi wangu ulikuwa tatizo, kwa hiyo nilichangiwa, nikapelekwa hospitali ambako mtoto alilazwa na kupewa dawa lishe. Hivi sasa nakazana kufanya kazi nipate chakula cha mtoto, sina tatizo tena,” anasema.

Naye Tumpe Ngimbudzi anasema mjukuu wake aliyekuwa na tatizo la utapiamlo anaendelea vizuri baada ya kupata lishe bora kutokana na jitihada za wauguzi na viongozi wa serikali ya kijiji.

Tulahega Magula anasema faini aliyotozwa kwa ajili ya uzembe wa kuwapa lishe bora wanawe ilimfanya ajitahidi kuwasimamia na kuhakikisha hawapati tena tatizo hilo.

Kuhusu maambukizi ya VVU

Mtitu anasema mkakati pekee waliojiwekea kuhakikisha hakuna maambukizi yanayowapata watoto ni kwa mama zao kuhudhuria kliniki na kujifungulia zahanati.

“Mama anapopata huduma za afya tangu wakati wa ujauzito anapata nafasi ya kuijua afya yake, kama atakuwa ameambukizwa anaweza kumlinda mtoto wake aliye tumboni kabla na baada ya kuzaliwa,”anasema.

Anasema kutokana na ukweli huo, wahudumu wa afya ya msingi wanasimamia kuhakikisha wajawazito wote kijijini hapo wanapima afya zao na kuwa makini kujilinda ili kuwalinda watoto wao tumboni.

“Hili pia tulifanikiwa. Hakuna mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano aliye na maambukizi japo wapo wazazi wenye watoto wadogo ambao wanayo maambukizi,” anasema.

Mwenyekiti huyo wa kijiji, Kihombo anasema sheria ya kwanza kwa wajawazito kijijini hapo ni kuhudhuria kliniki.

“Kujifungulia hospitali ni lazima, hii imetusaidia sana na tunamuomba Mungu tuendelee kuwasaidia watoto wetu,” anasema.

Mmoja wa akina mama ambaye mwanawe hana maambukizi anasema aliijua afya yake kuwa anamaambukizi ya VVU wakati wa ujauzito.

Anasema awali alishtuka, lakini baadaye aliiona ni hali ya kawaida kutokana na huduma aliyoipata kutoka kwa wahudumu wa zahanati.

“Kwa hiyo nilijifungua salama, nilimnyonyesha mwanangu miezi sita bila kumpa chochote na sasa nimemuachisha. Ana afya nzuri na ninamshukuru Mungu atakua salama,”anasema.

Mratibu wa Ukimwi mkoani Njombe, Dk Braine Burure anasema mkakati wa mkoa huo ni kupunguza au kumaliza kabisa maambukizi ya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Hata hivyo, anasema japo kukosekana kwa mashine ya kupima wingi wa virusi kwa maendeleo ya mtumiaji wa dawa za kufubaza VVU ni changamoto inayowafanya wengi kutofuatiliwa maendeleo ya tiba ipasavyo na huduma ya mama na mtoto inasimamiwa kwa umakini.

Anaitaja changamoto nyingine ni umbali kutoka makazi ya wananchi na vituo vya kutolea huduma za upimaji VVU na Ukimwi.

Lakini anasema tatizo hilo bado halijawa kikwazo kikubwa kwao, wanaendeleo kutoa elimu kwa jamii kuhusu suala hilo ili kuona umuhimu wa kuwalinda watoto wao dhidi ya maambukizi ya VVU.

Mkakati wa Serikali

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka anasema msingi wa afya bora kwa jamii ni pamoja na kuzilinda zile za watoto na wajawazito.

Anasema ili kupunguza maambukizi ya VVU mkoani humo, mbali na kutoa elimu, lazima watoto wafanyiwe tohara ili kuua mila ya kutotahiriwa kwa baadhi ya jamii mkoani humo kwa madai inachangia kusambaza maambukizi.

Mratibu wa Shirika lisilo la Kiserikali la Cocoda, Alatanga Nyagawa anasema Kijiji cha Ikuna ni cha mfano kwenye ulinzi wa mama na mtoto kwa sababu wametambua umuhimu wa kundi hilo.

“Ni kweli kijiji hiki ni waelewa hata sisi wakati tunakwenda kutekeleza miradi yetu wanatuelewa na kuitekeleza kwa makini hasa ile inayowahusu watoto,”anasema.

Nyagawa anasema kuzalisha chakula kwa wingi si sababu pekee ya jamii kuwa na afya bora.

“Kikubwa hapa ni usimamizi wa nini anachokula mtoto na kwa wakati gani,” anasema.