Hii ya Rais kuwa mgeni rasmi michezoni iwe endelevu

Muktasari:

  • Wadau wengi hawakutarajia kuyasikia ya TFF kumwalika Rais kuja kuifanya kazi hiyo kwa sababu halikuwa jambo la kawaida baada ya kufanywa hivyo na Rais Ali Hassan Mwinyi takribani miongo mitatu iliyopita.

Baada ya kipindi kirefu cha kutomwona Rais wa nchi akienda uwanjani kukabidhi kombe la mshindi/bingwa wa Ligi Kuu kama ambavyo tumemshuhudia Rais John Magufuli alivyowakabidhi Simba kombe lao la VPL.

Wadau wengi hawakutarajia kuyasikia ya TFF kumwalika Rais kuja kuifanya kazi hiyo kwa sababu halikuwa jambo la kawaida baada ya kufanywa hivyo na Rais Ali Hassan Mwinyi takribani miongo mitatu iliyopita.

Baada ya taarifa ya kwamba Rais ameukubali mwaliko na kwamba atahudhuria, kila mwana michezo alifurahia kwa sababu huyo ni kiongozi wa juu wan chini mwajiri namba moja na ndiye mwenye uamuzi wa mwisho ya kulikubali jambo au kulikataa, hivyo kufika kwake uwanjani ameuonyesha umma wa Watanzania kwamba yeye pia ni mwanamichezo na kudhihirisha yale ambayo amekuwa akiyasema kwa kuyatekeleza au kuyasimamia.

Ni matarajio ya wadau wengi kwamba fursa hiyo itakuwa imetumiwa vyema kwanza kumwelezea kuhusu changamoto ambazo ziko ndani ya uwezo wake kama fursa hiyo ningeipata ningemweleza Rais asaidie yafuatayo kama suluhisho la muda mfupi:

• Kuviboresha viwanja ambavyo vinamilikiwa na CCM.

Ni jambo lililodhahiri kwamba viwanja vingi ambavyo mchezo wa mpira wa miguu unachezwa vinamilikiwa na CCM.

Mathalani, Lake Tanganyika, Ali Hassan Mwinyi, Kambarage, Kirumba, Samora, Majimaji, Sokoine, Jamhuri Dodoma na Jamhuri Morogoro na Mkwakwani.

Kati ya viwanja hivyo, ni viwanja vya Samora na kidogo Kirumba ndivyo vina hali nzuri.

Ikumbukwe kwamba sehemu ya kuchezea ina mchango mkubwa sana katika kumwezesha mchezaji kuonyesha kiwango chake na kuinua kiwango cha wachezaji. Viwanja hivi vinatakiwa vitengenezewe mpango mkakati hasa wa kuviendeleza.

Hili linawezekana baada ya kuona maboresho makubwa yaliyofanyika Uwanja wa Samora ambao sasa unaweza kutumika hata katika mechi za kimataifa na miaka miwili tu iliyopita ulikuwa mmoja wa viwanja vibovu Tanzania.

• Kambi za JKT kutumika kama vituo vya kuendeleza michezo, Jeshi la Kujenga Taifa limekuwa ni kitovu cha umahiri wa wanamichezo na karibu kila kanda ina kambi moja ya JKT.

Wizara na TFF wangeweza kuutumia mwanya huo kumwomba Amiri Jeshi Mkuu kumwomba vikosi vya JKT vitumike kama vituo vya umahiri vya kukuza michezo ukiwemo mpira wa miguu na hata uboreshaji miundombinu yake.

Kuendesha vituo kama hivyo kwa watu binafsi ni gharama kubwa na tumeshuhudia vituo hivyo vikishindwa kufanya vizuri. Rais angeweza kuombwa kutoa maelekezo hayo ili vikosi hivyo vya JKT visaidie kuwaendeleza wachezaji wenye vipaji.

Kwa mpango wa muda mrefu, ningemwomba Rais asaidie katika maeneo yafuatayo

• Kuimarisha vipindi vya michezo na mashindano ya shule za msingi na sekondari

Kwa wale ambao walisoma shule miongo minne iliyopita, watakumbuka kwamba kwenye shule za msingi na sekondari kulikuwepo na vipindi vya michezo ambapo wanafunzi walitoka nje ya madarasa kwa ajili ya michezo na kuendelea na vipindi vya masomo ya kawaida. Hali hiyo iliamsha wanafunzi wenye vipaji kujitokeza na ni katika miaka hiyo, ndipo tulipoona klabu nyingi za mitaani kuwa na wachezaji kutoka kwenye shule na vyuo na hata timu zetu za Taifa za kandanda na netiboli zilikuwa tishio kwenye ukanda huu.

Ni kweli Umisseta na Umitashumta imerudi, lakini si kwa kiwango kile. Kipindi cha PE kikirudishwa, kitaongeza wanamichezo wenye vipaji na mahiri kujitokeza lakini sanjari na Malya kutoa walimu wengi.