Hili alilofanya Makonda lipewe nguvu kisheria

Muktasari:

  • Wanawake hao wamefanya hivyo baada ya mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda kutangaza kampeni ya kuwasikiliza. Umati mkubwa wa wanawake kutoka vitongoji vya jiji hilo ulidhihirisha kuwa tatizo hilo ni kubwa katika jamii.

Ni wiki moja imepita tangu wanawake wenye watoto wanaodai kutelekezwa waanze kuwasilisha malalamiko yao katika ofisi za mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Wanawake hao wamefanya hivyo baada ya mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda kutangaza kampeni ya kuwasikiliza. Umati mkubwa wa wanawake kutoka vitongoji vya jiji hilo ulidhihirisha kuwa tatizo hilo ni kubwa katika jamii.

Wapo wanawake ambao ukiwatazama usoni hutabisha kwamba wanawalea watoto wao katika mazingira magumu baada ya waume zao au watu walio zaa nao kuwatelekeza.

Lakini pia wapo wanawake waliojitokeza na mbwembwe kwa nia ya kuwakomoa wenzi wao kwa madai kuwa fedha wanazopewa kwa ajili ya matunzo ya watoto ni chache.

Tukiachilia mbali siasa zilizojitokeza wakati sakata hilo likiendelea, ni ukweli usiopingika kwamba watoto wengi wanaishi kwenye mazingira hatarishi kwa sababu ya wazazi wao.

Hivi karibuni niliandika makala maalumu ya watoto wa mtaani jijini Dar es Salaam na wengi niliokutana nao wametelekezwa na wazazi wao.

Watoto hao wamejikuta mtaani wakiishi kwa kuomba na kulala kusikojulikana kisa tu eti mama alipopata ujauzito baba alikataa au alikimbia.

Na baba alipokataa mimba hiyo, mama huyo baada ya kujifungua akaona bora amtelekeze mwanaye mtaani kwa kushindwa kumlea.

Ukweli ni kwamba, migogoro mingi ya ndoa au wenza ndiyo inayosababisha watoto wengi kuishi katika mazingira magumu. Hakuna anayebisha kwamba hawa ndio Taifa la kesho.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, idadi ya watoto ni takriban nusu ya watu wote.

Kwa lugha nyingine idadi hiyo ya watoto ni viongozi wa baadaye.

Binafsi alilolifanya Makonda kuwaita wanawake waliotelekezwa wakiwa na watoto wao ofisini kwake nimelipokea kwa mikono miwili.

Hata hivyo, najiuliza maswali mengi, baada ya hapo nini kitafuata? Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009, watoto wana haki ya kulindwa, kutunzwa, kupendwa na kupata mahitaji yote muhimu ikiwamo elimu.

Kwa maana nyingine, ili watoto wa Tanzania waweze kutimiza ndoto zao kimaisha ni lazima wazazi wasiowatunza wawajibishwe. Wazazi hawa hawataweza kuendelea kuwajibishwa kupitia kampeni? Jibu ni hapana.

Kampeni ya Makonda iiamshe jamii na Serikali yenyewe kuona kwamba tatizo hili lipo na ni kubwa.

Umati wa wanawake waliojitokeza umeonyesha kuwa wana migogoro na wenzi wao, vingine wasingeweza kujitokeza hadharani.

Ni jukumu sasa la Serikali kuvipa meno vyombo vyake katika kuhakikisha jambo hilo linasimamiwa kikamilifu.

Pia, madawati ya jinsia yaliyo kwenye vituo vya polisi lazima yawe na uwezo wa kuwasaidia watoto wanaofikishwa huko wakilia kufanyiwa ukatili ikiwamo kutelekezwa.

Ofisi za ustawi wa jamii ambazo ndizo husikiliza kesi zinazohusiana na malezi ya watoto ni lazima ziongezewe nguvu kwa sababu sheria ipo.

Kinacholitesa Taifa letu ni hata kwenye masuala ya msingi kama hili la watoto tuingiza siasa.

Mathalan, niliona picha ya mtoto ikisambazwa huku pembeni yake akiwapo mwanasiasa mmoja jambo lililomfanya yeye mwenyewe akanushe na hivyo kuonyesha namna gani katika kila penye manufaa tunaingiza siasa.

Katika uzinduzi wa Jukwaa la Kimataifa la Haki za Mtoto kwenye Elimu Tanzania kupitia programu mtandaoni, hivi karibuni, wadau wa haki za watoto walisema ni kosa kisheria kusambaza picha ya mtoto bila ridhaa ya wazazi wake na hii ipo duniani kote.

Hata hivyo, inawezekanaje jambo muhimu kama hili kulifanyia mzaha? Au wanaofanya huo mzaha hawajui kwamba wanachezea na kulidhalilisha Taifa la kesho?

Makonda amesaidia kuamsha macho ya wengi waone kwamba watoto waliotelekezwa na wazazi wao ni wengi. Lakini je, wazazi wanaodaiwa kutelekeza watoto wao wapo? Kwa nini waachwe bila kuchukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria ya mtoto?

Lakini pia ni wakati wa wizara husika kuja na mkakati kabambe wa kuielimisha jamii juu ya uzazi wa mpango.

Wanawake na wanaume wengi wamejikuta wakizaa watoto wasiopanga kabla kuwazaa kwa kuwa tu wameshiriki tendo la ngono bila kutumia njia ya uzazi wa mpango.

Idadi kuwa ya wanawake waliobeba watoto hadi kwa Makonda wanaonyesha wazi namna gani bado jamii inahitaji elimu kuhusu uzazi na kumtunza au kumlea mtoto aliyezaliwa.

Narudia tena kusema, Makonda ameonyesha kwamba tatizo lipo na sitarajii kuona kuwa mikoa mingine inafanya kampeni ya aina hiyo, lakini natarajia kuona madawati na vyombo vya Serikali vilivyoanzishwa kwa mujibu wa sheria kuwasaidia watoto vinapewa msukumo.

Tumaini Msowoya ni mwandishi mwandamizi wa Mwananchi na anapatikana kwa baruapepe; [email protected]