Kama Bodi ya Mikopo imeelemewa, wadau wengine wahusishwe

Muktasari:

  • Mkurugenzi wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru alisema idadi hiyo ni ongezeko la wanafunzi 7,000 kulinganisha na mwaka jana na kwamba walioomba walikuwa 33,000.

Hivi karibuni, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB) ilitangaza kutenga Sh427 bilioni kwa mwaka 2018/19 zitakazonufaisha zaidi ya wanafunzi 120,000. Kati yao 40,000 wakiwa ni wa mwaka wa kwanza.

Mkurugenzi wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru alisema idadi hiyo ni ongezeko la wanafunzi 7,000 kulinganisha na mwaka jana na kwamba walioomba walikuwa 33,000.

Hata hivyo, kumekuwa na hofu miongoni mwa wananchi baada ya bodi hiyo kutoa masharti kwa waombaji yanayoonyesha aina fulani ya ubaguzi katika kupata fursa hiyo.

Sifa kumi za msingi zilizotolewa na bodi hiyo ndiyo zilizoanzisha utata huo. Kwa mfano, sifa namba tisa na 10 zinazosema; “Waombaji ambao wazazi wao ni wakurugenzi au mameneja waandamizi katika makampuni binafsi yanayotambuliwa na mamlaka za mapato na usajili, hawatarajiwi kuomba” mkopo.

Kipengele cha 10 kinasema “waombaji ambao wazazi wao ni viongozi wa umma au kisiasa ambao wanatajwa na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, hawatarajiwi kuomba mikopo”.

Masharti mengine japo hayajaorodheshwa kwenye miongozo ya bodi, yamekuwa yakisemwa na viongozi wa Serikali majukwaani. Kwa mfano, tunaambiwa hata mwanafunzi aliyesomea shule binafsi haruhusiwi kuomba mkopo. Nasema japo hayajaorodheshwa, lakini lisemwalo lipo na kama halipo linakuja.

Ingawa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amefafanua kuhusu masharti hayo, bado kuna ukakasi mwingi katika utoaji wa mikopo hiyo.

Kwanza, Katiba ibara ya 11(2) na (3) inatoa haki ya kila raia kupata elimu.

“Kila mtu anayo haki ya kujielimisha, na kila raia atakuwa huru kutafuta elimu katika fani anayopenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wake. Serikali itafanya jitihada kuhakikisha kwamba watu wote wanapata fursa sawa na za kutosha kuwawezesha kupata elimu na mafunzo ya ufundi katika ngazi zote za shule na vyuo vinginevyo vya mafunzo,” inasema.

Ni kweli Serikali imeanzisha Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) ili kukidhi matakwa ya kikatiba ya kuwawezesha Watanzania kupata elimu na mafunzo ya ufundi katika ngazi zote. Lakini bado bodi hii haijajizatiti kikamilifu kukidhi haja hiyo.

Hii inaonekana kwenye masharti kwa waombaji yanayoonyesha kuwapo kwa hisia za ubaguzi na tayari kumekuwapo malalamiko kutoka kwa wananchi.

Angalau sharti la 10 linalokataza watoto wa viongozi wa umma kuomba mikopo, lakini hayo masharti mengine yamepitiliza.

Kwa mfano, huwezi kukataza wanafunzi waliotoka shule binafsi kwa kigezo tu kwamba walikuwa wakijilipia ada tofauti na wa shule za Serikali, wakati hata huko wapo wanaolipa kiasi kidogo.

Hivi Serikali ina uhakika gani kwamba kila aliyesomea shule binafsi wazazi au walezi wake ni matajiri? Kwenye suala la leseni ya bishara, napo pana utata, kwa sababu inaweza isiwe kigezo cha biashara kuwa kubwa.

Ni kweli lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaotokea kwenye kaya masikini wanapata fursa ya elimu, lakini hilo lisiwabague kabisa hata waliotoka kwa wazazi wafanyabiashara kwa hoja ya leseni ya biashara.

Huko kwenye biashara kwenyewe hali ni mbaya; kuna taarifa kuwa biashara zinafungwa kwa sababu ya tozo kubwa za kodi. Kwa mfano, tumesikia baadhi ya wafanyabiashara wameamua kuhamia nchi jirani kama Zambia ili kuepuka bugudha ya tozo kubwa.

Kimsingi, mazingira ya biashara kwa sasa siyo mazuri nchini. Ieleweke pia kwamba kuna asilimia zaidi ya 80 ya wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi wakiwamo wajenzi, wasafirishaji, wafanyabiashara ndogo ndogo ambao licha ya kutokuwa katika mfumo rasmi baadhi yao wanajimudu kifedha.

Kwa hiyo, unahitajika uchambuzi wa hali ya juu ili kubaini nani anamudu kumsomesha mtoto wake chuo kikuu na nani hawezi, kuliko kujumuisha watu bila kujali undani wake.

Masharti haya yanayoibuka kila siku yanaashiria kwamba Bodi haina fedha za kutosha kufadhili wanafunzi wote wanaostahili kwenda vyuo vikuu.

Kama hilo ni kweli, basi bodi hiyo ikiri na iweke mikakati ya kukusanya fedha za kutosha. Serikali nayo iwekeze kwenye bodi hiyo ili kuwapa fursa wanafunzi wote wanaostahili.

Elimu ina gharama kubwa, kama Serikali imeamua kutoa elimu bure kutoka shule za msingi hadi kidato cha nne, basi ijue pia kuna jukumu la kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Aidha, Serikali iruhusu wadau wengine zikiwamo benki zinazotaka kukopesha wanafunzi zifanye hivyo, kuliko kutegemea bodi peke yake ambayo sasa inaonekana kuelemewa na wingi wa wanafunzi.

Elias Msuya ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi.