Karibu Dk Mahenge, Dodoma inahitaji maendeleo

Dk Binilith Mahenge

Muktasari:

Huyu anakuwa mkuu wa mkoa wa pili katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano tangu ulipoingia madarakani Novemba 2015 baada ya Jordan Rugimbana ( sasa amepumzishwa) aliyefungua milango kwa Serikali hii na ndiye aliyepokea agizo la Serikali kuhamia Dodoma

        Hivi karibuni, Rais John Magufuli alifanya mabadiliko ya wakuu wa mikoa ambayo yalimhamisha aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dk Binilith Mahenge kuja Dodoma.

Huyu anakuwa mkuu wa mkoa wa pili katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano tangu ulipoingia madarakani Novemba 2015 baada ya Jordan Rugimbana ( sasa amepumzishwa) aliyefungua milango kwa Serikali hii na ndiye aliyepokea agizo la Serikali kuhamia Dodoma.

Hata hivyo, wawili hao si kwamba ndiyo wanaanza kuwa viongozi ndani ya mkoa huu. Wapo waliotangulia na kufanya kazi kubwa iliyotukuka ambayo wengi nyayo zao hazijafutika.

Kiuchumi Dodoma iko nyuma ukilinganisha na mikoa mingi nchini. Kielimu pia bado iko nyuma kwani hata mwamko kwa baadhi ya maeneo ni mdogo.

Dk Mahenge amekuja katika kipindi ambacho mkoa huu unashika nafasi ya 24 kati ya 26 kwa matokeo ya darasa la saba 2017, huku matokeo ya kidato cha nne yakiiweka Dodoma katika nafasi ya 19 nchini.

Katika masuala ya kilimo, bado wananchi wengi wanalazimisha kulima mazao ambayo yanahitaji maji mengi yakiwamo mahindi ilihali mkoa huu ni miongoni mwa mikoa inayopata mvua za wastani.

Kutokana na hali hiyo, kila mwaka maeneo mengi ya mkoa huu wakulima hawavuni na matokeo yake kuwafanya wanasiasa kuwa na mtaji wa kisiasa kwa kuzungumzia suala la njaa na kila mara. Wanaiomba Serikali kuwapeleka wapigakura wao chakula cha bei ndogo na bure.

Unaweza kusema Dk Mahenge ameletwa katika mkoa wenye matatizo kuliko alikotoka na hivyo anatakiwa kuwa mbunifu na makini katika kuwasaidia wananchi wake.

Niliwahi kuhoji siku za nyuma nilipoandika; mfupa uliowashinda wengi, Rugimbana atauweza? Na bila shaka hali ilikuwa hivyo kutokana na ukweli kuwa mkuu huyo hadi anapumzishwa, hakuwa amefanya jambo jipya kiasi cha kukumbukwa kama alifanya kazi kwa zaidi mwaka mmoja.

Siku chache zimepita tangu Dk Mahenge alipotua hapa lakini hata akiondoka leo anaweza kuwa ameacha kitu cha kukumbukwa hata na watu katika maeneo machache ya vijiji alivyopita. Hapa ndipo viatu vilivyokosa mtumiaji sasa vimempata anayeweza kuvitumia huenda vikachakaaa na kulazimika kununua vingine atakavyoacha ili vije kutumiwa na mwingine.

Dk Mahenge amekuja na mambo mawili ambayo kweli yanaonekana kuwa na mwitikio ambao utaipeleka Dodoma katika mikoa yenye viwanda.

Anasisitizia suala la elimu na kilimo chanye tija. Anasema hivyo ndivyo vipaumbele vyake ukiacha ajenda ya kitaifa ya viwanda ambayo anasema itazungumzwa zaidi na wakuu wa wilaya katika maeneo yao.

Msomi huyu anawakutanisha wakulima na wanakaa naye na kuzungumza kama ndugu na marafiki, jambo linalosababisha maeneo yote anayopita watu kumuona kama mfalme waliyekuwa wanamngoja.

Mbinu anayoitumia inampa nafasi ya kukubalika na kusikilizwa, kwani kuna mahali anawauliza wakulima wanapenda kulima nini, na baada hapo anaanza kuzungumza nao kwa kuwapa faida na hasara kuhusu mazao wanayolima.

Bila shaka nguvu hii ikiendelea, Dodoma itakuwa ile ambayo wengi waliitarajia na uwezekano wa wananchi wake kuyapokea makao makuu, utakuwa kwa asilimia kubwa.

Hata hivyo, kinachotakiwa ni kwa watumishi wote kumuunga mkono na kumsaidia ili waweze kuifikia ndoto hiyo.

Habel Chidawali ni mwandishi wa Mwananchi, Dodoma