Tuesday, September 12, 2017

Karibu Jaji Mkuu uiboreshe Mahakama Jaji Mkuu wa Tanzania,Profesa Ibrahim Hamis

 Jaji Mkuu wa Tanzania,Profesa Ibrahim Hamis 

By Mwananchi

Rais John Magufuli amemteua Profesa Ibrahim Hamis kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania baada ya kukaimu nafasi hiyo kwa miezi minane kabla ya jana kumwapisha katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Tunakupongeza. Hatua ya Rais kukukabidhi jukumu hilo baada ya kukaimu nafasi hiyo tangu Januari, ina maana amekutathmini na kuona unastahili kusimamia mhimili huo.

Katika kipindi cha miezi minane ambacho umekuwa ukikaimu utakuwa umeshuhudia kwa macho yako changamoto mbalimbali za kiutendaji, ukosefu wa nidhamu, uhaba wa fedha na majengo ya mahakama, ucheleweshaji kesi na mgongano wa mihimili.

Tunaamini utakuwa umejiwekea mpango mkakati wa kushughulikia changamoto hizo ili kuifanya mahakama iaminike na kiwe chombo pekee kimbilio kwa kila mtu na haki itolewe kwa wakati.

Inafahamika kuwa dola ni moja lakini ina mihimili mitatu ambayo imegawana majukumu; Serikali Kuu, Bunge na Mahakama. Serikali huandaa miswada, Bunge hutunga sheria ambazo hutafsiriwa na mahakama.

Lakini katika miaka ya hivi karibuni mhimili wa Serikali umekuwa ukigubika Mahakama. Tunafahamu kwamba Serikali ni mdau mkubwa katika shughuli za mahakama kwa kuwa mwanasheria mkuu ana kesi nyingi mahakamani.

Mbali ya mwanasheria mkuu kuwa na kesi nyingi, kiuhalisia Serikali ndiyo inatafuta fedha za kuendesha shughuli za mahakama na ndiyo kiini cha mhimili huo kusema una mizizi mirefu inayofika hadi kwenye mihimili mingine.

Hata hivyo, katika suala la utoaji haki tunaomba mahakama isimame kwa miguu yake isishurutishwe na isiingiliwe; majaji wazingatie sheria wakati wa kutoa hukumu. Haiingii akilini kwamba mahakama inatoa amri fulani lakini watendaji walioko chini ya Serikali wakapuuza na wakaendelea na shughuli zao kana kwamba hakuna amri yoyote.

Mfano halisi ni ubomoaji wa nyumba unaoendelea katika baadhi ya maeneo nchini hasa jiji la Dar es Salaam ambazo inadaiwa zimejengwa katika hifadhi ya barabara. Katika eneo moja nyumba za wananchi ambazo mahakama ilitoa amri ubomoaji usitishwe maofisa waliokuwa wakisimamia kazi hiyo waliendelea kubomoa na mahakama ikakaa kimya.

Jambo jingine tunadhani Jaji Mkuu utalisimamia vyema ni umalizaji wa kesi. Baadhi ya kesi zimekaa muda mrefu mahakamani kwa madai mbalimbali. Kuna kesi zinaahirishwa mara kwa mara kwa madai upelelezi haujakamilika na nyingine kwa maelezo hakimu amesafiri au ana udhuru na sababu mbalimbali.

Tunaomba masuala yote mawili, na hasa la ucheleweshaji kesi kwa visingizo vya upelelezi bado haujakamilika au faili la kesi kutoonekana yakomeshwe ili haki isicheleweshwe.

Vilevile tunaomba juhudi zifanyike kuboresha mahakama ili kuwafikia zaidi Watanzania kwa kuwasogezea karibu huduma za kisheria au mahakama wasitembee umbali mrefu kufuata haki.

Mfano, katika miaka ya hivi karibuni kulikuwa na mpango wa kusogeza huduma ya elimu na afya, kuwa na zahanati katika kila kijiji na kuwa na kituo cha afya katika kila kata. Mkakati huu unaweza kutumiwa hata na idara ya mahakama ili kuwa na mahakama za mwanzo walau katika kila kata.

Mafanikio ya ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na polisi yalitokana na serikali kuhamasisha na kuwashirikisha wananchi, tunadhani mbinu hizo zinaweza kutumiwa hata upande wa ujenzi wa mahakama ili kupunguza gharama za kutafuta haki. Vilevile, mahakama zitumie Tehama na kuona uwezekano wa kesi kubwa kuamriwa kwa uwazi.

-->