Kauli ya Rais ichochee mjadala mimba shuleni

Muktasari:

Rais alisema hayo wakati akizindua Barabara ya Bagamoyo-Msata wiki hii alipotoa msimamo wake kuwa chini ya Serikali yake, hakuna mwanafunzi atakayepata mimba ambaye ataruhusiwa kuendelea na masomo.

Rais John Magufuli ameeleza msimamo wake kuhusu tatizo kubwa la wasichana kupata mimba wakati wakiwa shuleni na kusababisha wasiendelea na masomo katika shule za Serikali.

Rais alisema hayo wakati akizindua Barabara ya Bagamoyo-Msata wiki hii alipotoa msimamo wake kuwa chini ya Serikali yake, hakuna mwanafunzi atakayepata mimba ambaye ataruhusiwa kuendelea na masomo.

Alisema shule ziko kwa ajili ya wanafunzi na si wazazi, hivyo mtoto atakayepata mimba atakosa masomo na aliyempa mimba atashtakiwa na kwenda jela kutumikia kifungo cha hadi miaka 30.

Rais ametoa kauli hiyo wakati kukiwa na mijadala na mikakati ya jinsi ya kumsaidia mtoto wa kike apate haki yake ya msingi ya elimu hata baada ya kushika mimba akiwa shuleni.

Harakati nyingi zinalenga kuishawishi Serikali kuridhia na kutengeneza utaratibu ambao utamuwezesha mtoto huyo kuendelea kufuata ndoto yake ya mafanikio kwa kupitia elimu.

Pia, kauli ya Rais imekuja wakati hata Serikali na chama tawala cha CCM wako kwenye mchakato huo wa kuangalia ni jinsi gani wataweza kumsaidia mtoto wa kike aliyekutwa na janga hilo.

Harakati hizo hazimaanishi kuwa watetezi hao wanataka kulea umalaya shuleni, bali wanatambua kuwa si wote wanaopata mimba, wanapata kwa sababu ya “kiherehere” kama alivyowahi kusema Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.

Ukweli ni kwamba idadi kubwa ya wanaopata mimba ni watoto wa maskini, wanaoishi maeneo ya vijijini ambako shule ziko mbali na makazi na hivyo kulazimika kuzifuata umbali mrefu ambako njiani hukutana na vikwazo vingi.

Pia wengine ni wale ambao kazi za nyumbani huwalazimisha kushinda nje ya nyumba kwa muda mrefu kufuata kuni na maji na hivyo kukutana na wanaume wanaojua kutumia mazingira hayo vizuri kukidhi tamaa za mwili.

Lakini katika kundi hilo, pia wako wale ambao wanabakwa kwa nguvu na kujikuta wakipata mimba bila ya kutarajia.

Familia zinazoishi maisha bora hazikumbwi sana na tatizo hili na hata likitokea, wazazi wao huweza kuwapeleka shule za binafsi ambazo pia ni nzuri kuliko za Serikali na kupata elimu bora.

Kwa hiyo, suala hili haliwezi kubebeshwa watoto wa kike wanaopata mimba au wazazi, eti kwa sababu tu hawawaangalii vizuri watoto wao, bali kwa sababu mazingira ya umaskini, ya kielimu na huduma za jamii si rafiki kwa mtoto wa kike.

Kwa hiyo, Rais Magufuli ameeleza msimamo wake kuhusu tatizo la watoto wa kike kupata mimba kabla ya kumaliza shule na hivyo huo ndio mwelekeo wake.

Lakini, Rais Magufuli hajazuia watu wenye mawazo tofauti wasijadili wala kutafuta mbinu mbadala za kusaidia watoto wa kike. Ni vizuri kauli ya Rais ikawa kuchochea mjadala huo wa kusaidia watoto wa kike ili kupata suluhisho la kudumu.

Ni vizuri kwamba moja ya taasisi zinazotetea elimu, HakiElimu imesema itatafuta nafasi ya kuongea na Rais ili kujua msingi wa hoja zake na wao kumweleza. Hili ni jambo zuri na linaloonyesha ukomavu wa jinsi ya kukabiliana na masuala ya kijamii; kwamba badala ya kumshambulia Rais kwa kutofautiana nao, wanataka kukutana naye kwanza.

Kwa kuwa suala hili ni zito na linazungumzia mustakabali wa mtoto wa kike, mjadala huu ni muhimu ukaendelezwa ili kupata suluhisho bora.

Mjadala wa kutafuta suluhisho unaweza kusaidia kupata mbinu za; kwanza kuzuia kwa kiasi kikubwa tatizo hilo lisitokee; na pili kupata njia ya kusaidia watoto wa kike pale litakapotokea kwa bahati mbaya.

Kwa hiyo, kuna faida kubwa kulijadili kuliko kutafuta mbinu za kuwazomea watetezi, wazazi au watoto waliopatwa na tatizo hilo kwa sababu tu wanatofautiana na msimamo wa Rais.