Kero usafiri wa mwendo kasi zivaliwe njuga

Muktasari:

  • Si mara ya kwanza kwa usafiri huo ambao kimsingi umekuwa kimbilio la wakazi wengi wa jiji hilo, kudorora na kuzusha sintofahamu kwa watumiaji wake. Lakini tukio la kuzorota kwa huduma hiyo juzi lilichukua sura mpya, kwa baadhi ya abiria kufikia hatua ya kukwea madirishani kwa ajili ya kupata nafasi ya kusafiri.

Jana tuliripoti taarifa ya kutokea kwa mshikemshike baada ya wasafiri wanaotumia mabasi ya mwendo kasi jijini Dar es Salaam kuanzisha vurugu, kufuatia kudorora kwa huduma ya usafiri huo juzi asubuhi.

Si mara ya kwanza kwa usafiri huo ambao kimsingi umekuwa kimbilio la wakazi wengi wa jiji hilo, kudorora na kuzusha sintofahamu kwa watumiaji wake. Lakini tukio la kuzorota kwa huduma hiyo juzi lilichukua sura mpya, kwa baadhi ya abiria kufikia hatua ya kukwea madirishani kwa ajili ya kupata nafasi ya kusafiri.

Vurumai ya wananchi katika vituo vya mabasi hayo, ikawalazimisha baadhi ya viongozi serikalini kuingilia kati. Viongozi hawa ni Waziri Ofisi ya Rais (Tamisemi), Suleiman Jaffo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Kwa tukio hili la juzi na mengineyo yaliyowahi kutokea siku za nyuma, tuna kila sababu ya kusema kwa kinywa kipana kuwa mamlaka husika hazikujipanga kwa mradi huu na ndio maana kila uchwao kuna tatizo linalozuka kuhusu usafiri huo kiasi cha kuwakirihisha watumiaji wake.

Ni lini tutasikia habari njema kuhusu usafiri huu kama vile kuongezwa kwa mabasi, kuwekwa kwa utaratibu wa watu kutorundikana vituoni na mengineyo yanayoweza kuwavutia watu wengi zaidi kutumia usafiri huu?

Kinyume chake kila siku tangu huduma hii ianze, wakazi wanachoshuhudia ni kero juu ya kero. Kama si ukosefu wa tiketi, tatizo litakuwa uhaba wa mabasi. Mabasi yakiwepo, hakuna utaratibu mzuri wa kudhibiti abiria. Lakini ipo pia kero ya mabasi kupita vituoni na kuacha abiria.

Kuanzishwa kwa usafiri huu kuliwakuna watu wengi. Hata nasi tulifikiri kuwa huduma ya usafiri katika jiji hili si tu utaboreshwa, lakini pia utaendeshwa kisasa na kwa kufuata misingi ya ustaarabu.

Ni kwa sababu hii wakazi wengi waliupokea mradi huu kwa mikono miwili wakijua umekuwa mkombozi kwao. Wapo wenye magari walioamua kuyaacha wakiamini nusura ya usafiri jijini hapa imepatikana, lakini sivyo hivyo.

Usafiri wa mabasi ya mwendo kasi nao umeturudisha kulekule kwenye usafiri wetu wa daladala usiojali utu na hata ustaarabu wa kibinadamu.

Kibaya zaidi na kinachowakwaza wasafiri wengi ni kuwa katika baadhi ya maeneo ambayo mabasi ya mwendo kasi yanapita, mabasi ya kawaida ama yaliondolewa au baadhi kupunguzwa, jambo linalozidi kuongeza ukubwa wa tatizo la usafiri kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.

Hatuelewi kipi hasa kinachokwaza uendeshaji na usimamizi mzuri wa huduma hii, ili hatimaye ufikie ile azma ya kuboresha usafiri wa abiria, si kwa kurahisisha usafiri pekee, lakini kuufanya uwe wa kistaarabu kama ilivyo katika majiji mengine yaliyopiga hatua katika usafiri wa abiria.

Usafiri wa mabasi ya mwendo kasi ni mradi muhimu na wa kipekee kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam. Mamlaka husika hazina budi kuweka mifumo thabiti ya kushughulikia kila aina ya kero ili huduma hiyo ifikie lengo lililokusudiwa.