Wednesday, December 6, 2017

Maadui wa Taifa walewale hadi uzeeniMusa Juma.

Musa Juma. 

Jumamosi wiki hii, Watanzania wataadhimisha miaka 56 ya uhuru wa Tanzania Bara, maadhimisho ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Dodoma.

Kama ni binadamu, miaka 56 ni umri wa mtu mzima ambaye anaelekea uzeeni. Ni umri ambao mtu ameweza kupambana na changamoto nyingi na kuzishinda.

Wakati tunaadhimisha miaka hiyo, bado maadui watatu waliotajwa na hayati baba wa Taifa, umaskini, ujinga na maradhi wanaendelea kuliandamana taifa hadi uzeeni.

Ingawa kasi ya kupambana na maadui hawa ni kubwa lakini taifa halijafikia hatua ya kutangaza ushindi wa kishindo.

Tangu Mwalimu Julius Nyerere akiwa kiongozi wa chama cha Tanu, alitangaza vita dhidi ya maadui hawa, aliingia uwanjani kwa nguvu zake zote kuandaa mikakati na kusimamia utekelezaji wa mapambano.

Pamoja na kuwa wakati wa kutangazwa vita hivi, Mwalimu hakuwa na teknolojia za kisasa kama ilivyo sasa, lakini alijaribu kupambana kwa kiasi chake. Alianzisha vijiji vya ujamaa ili wananchi wakae eneo moja na kufanya kazi ya uzalishaji mali licha ya zoezi hilo kuwa na changamoto.

Katika kipindi hicho, Mwalimu pia alianzisha vyama vya ushirika ili kusaidia wakulima, viwanda vingi vilijengwa ili kuongeza thamani ya mazao ya wakulima.

Katika vita dhidi ya adui ujinga, yalitolewa maazimio mbalimbali ya kuboresha elimu kama lile la Musoma la mwaka 1974 la “Elimu kwa wote” na “Elimu kwa watu wazima” na aliweza kuyasimamia na matunda yake yalionekana.

Kumbukumbu zinaonyesha katika kipindi hicho, Tanzania ilikuwa ni moja ya mataifa ya mfano duniani kwa kupunguza kiwango cha wananchi wasiojua kusoma na kuandika.

Jitihada hizo za kukuza elimu zilisaidia vita dhidi ya maradhi, kwa kuwa walipatikana madaktari wazalendo na wauguzi japo walikuwa wachache.

Uelewa wa wananchi dhidi ya magonjwa uliongezeka lakini pia hospitali za Serikali na vituo vya afya vilitoa huduma bora.

Hata hivyo, wakati huo miaka ya baadaye ya utawala wake walikuwepo wasaliti na watu waliokosa uzalendo ambao walishiriki kuua viwanda vya umma, waliua mashirika na makampuni ya umma na hata vyama vya ushirika.

Wasaliti hawa ambao, hadi sasa wapo kwa viwango tofauti ndio ambao pia walidhoofisha kwa kujali maslahi yao jitihada za kupambana na ujinga na maradhi.

Sasa enzi la Mwalimu zimepita lakini inaonekana maadui aliyowabaini bado wapo na wameongezeka wengine.

Taifa hivi sasa lingepaswa kuwa linakwenda mbio katika kupigana vita dhidi ya maadui wengine baada ya kuwashinda wale watatu wa awali lakini hali sivyo ilivyo.

Hivi sasa pamoja na wale watatu, kumeongeza maadui wa kifisadi na wanaotokana na utandawazi wa kiuchumi na wanaojichukulia sheria mkononi.

Vita ya maadui hao sasa ni kubwa zaidi kuliko miaka 50 iliyopita na kibaya zaidi imejaa usaliti na hivyo kujikuta tukipigana wenyewe kwa wenyewe.

Hivyo, wakati tunaadhimisha Uhuru wa Tanzania Bara ni fursa nzuri kuanisha maadui zaidi wa Taifa letu na kuweka mipango madhubuti ya kukabiliana nao.

Hofu ya kufanya maamuzi haiwezi kuwa silaha ya ushindi. Ushindi wa vita, unajengwa na ujasiri na maridhiano ya Watanzania wote hasa pale mchango wa kila mmoja unapothaminiwa.

Kama Mwalimu na wasaidizi wake waliweza kutangaza vita dhidi ya maadui wa Taifa miaka 50 iliyopita na kufanikiwa kuanzisha vema mapambano, viongozi wa sasa na wananchi hawana kisingizio cha kushindwa kupata ushindi.

Hivyo itoshe kutoa wito, katika maadhimisho ya miaka 56 ya uhuru wa Tanzania tusitumie siku hii kuimba na kucheza tu, bali tuenzi vita takatifu aliyoanzisha Mwalimu kuhubiri umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania ili kuwashinda na maadui zetu.

Mussa Juma ni mwandishi Gazeti la Mwananchi mkoa wa Arusha anapatikana. 0754296503.     

-->