Mafuriko yameshatufunza mengi, tubadilike

Mafuriko katika baadhi ya maeneo nchini, yanaonekana kuwa ni suala la kawaida.

Waathirika wakubwa ni wakazi wanaoishi maeneo ya mabondeni na karibu na kingo za mito.

Kwa Mkoa wa Dar es Salaam mvua iliyonyesha kwa siku kadhaa mfululizo hivi karibuni, ilisababisha madhara makubwa ya miundombinu na hata vifo vya watu 10.

Awali, Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa (TMA), ilitahadharisha juu ya ujio wa mvua hizo na baadhi ya maeneo ambayo yalitajwa kuwa na mvua zaidi ya wastani, huku ikiwataka wakazi kuchukua tahadhari.

Jambo la kusikitisha ni kuwa mvua hizo zilipoanza kunyesha zikaleta madhara ambayo yalishatabiriwa na TMA.

Madhara haya yangeweza kuepukika kama watu wangechukua tahadhari kama walivyotangaziwa mapema na mamlaka husika.

Ukiachilia mbali jukumu la Serikali kufanya uokoaji katika majanga mbalimbali, wajibu wa kwanza ni watu wenyewe kuchukua tahadhari kwa kujiepusha na madhara hususan vifo.

Maeneo ambayo huathiriwa na mvua kila mara yanafahamika, lakini watu wameendelea kuishi katika maeneo hayo, huku wakiendelea kupoteza mali.

Serikali imekuwa ikihimiza mara kwa mara watu wahame katika maeneo ya mabondeni kuepusha majanga. Lakini masikio ya walio wengi yamewekwa nta.

Niendelee kutoa mfano wa jiji la Dar es Salaam ambalo maeneo yake mengi yako bondeni na aghalabu hukumbwa na baa la mafuriko, lakini wakazi wake ni kama vile hawajali.

Kwa nini mtu usichukue tahadhari mapema kwa kuondoka katika maeneo hayo. Wakati mwingine unakuta mtu ni mpangaji katika nyumba, lakini naye anaona tabu kubadili maeneo ya kukaa.

Watu wengine ambao wanapaswa kujitathmini ni wale ambao huthamini mali zao kuliko uhai.

Wakati wa hatari, hakuna haja ya mtu kuhangaika kuokoa mali bali nafsi pekee.

Lengo langu sio kukebehi waliotangulia mbele ya haki, lakini ni uzembe wa kufikiri mtu kufa akijaribu kuokoa runinga yake au vyombo vyake wakati angeweza kujiokoa kwanza yeye binafsi.

Watu watambue kuwa uhai wao una thamani kuliko mali zote wanazomiliki.

Ukiona maji yanaanza kujaa ndani kwa kasi isiyo ya kawaida, ondoka eneo hilo sio kuhangaika kuokoa vitu. Mali zinaweza kutafutwa, lakini uhai ukitoka haurudi.

Uokoaji wa mali ni vyema ukafanywa mapema kabla hali ya hatari haijaanza kuonekana (maji hayajaanza kujaa) au baada ya kujihakikishia usalama wa eneo husika kama ni ndani ya nyumba au barabarani.

Ni muhimu kurejea matukio yaliyopita ili yawe fundisho kwa wakati ujao, ili mambo kama haya yasiwe ya kila msimu wa mvua.

Tumechoka kusikia ndugu zetu wakipoteza maisha kila ufikapo msimu wa mvua hasa za Masika.

Tubakie na ajali zile ambazo kweli hazina kinga na kutokea kwake hakutabiriki, lakini sio hili la mafuriko ambalo mamlaka husika hutoa taarifa mapema kwa wananchi.

Kila mmoja athamini na ajisikie ana deni la kulinda uhai wake na wa mwenzake. Lakini pia Serikali iendelee kutoa elimu ya uokoaji ili watu waweze kujihami wanapokumbwa na majanga kama mafuriko.

Naamini vifo vitokanavyo na mvua vinaweza kuepukika, lakini jambo hilo linaanza na utashi wa mtu mmoja mmoja.

Tuchukue tahadhari na tuelewe kuwa uhai ni muhimu zaidi kuliko vitu au mali.

Ephrahim Bahemu ni mwandishi wa Mwananchi.

0756939401