Majibu ya Serikali kuhusu vazi la Taifa yanachanganya

Muktasari:

  • Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye baada ya kuingia wizarani, miongoni mwa mambo aliyoyakuta mezani na kutarajiwa kuyapa msukumo ni kuendeleza hadi mwisho ajenda ya kuwa na vazi la Taifa

        Mjadala kuhusu umuhimu wa kuwa na vazi la Taifa umedumu miaka kadhaa sasa, huku ukifa na kufufuka kutokana na mgongano wa mawazo kati ya wadau na Serikali wanaotakiwa kusimamia mchakato huo.

Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye baada ya kuingia wizarani, miongoni mwa mambo aliyoyakuta mezani na kutarajiwa kuyapa msukumo ni kuendeleza hadi mwisho ajenda ya kuwa na vazi la Taifa.

Waziri huyo kabla ya nafasi yake kutenguliwa na Rasi John Magufuli, alihitimisha suala hilo kwa kusema kuwa mchakato wa kuwa na vazi la Taifa anawaachia Watanzania wenyewe waamue, kwa kuwa ni suala linaloongozwa zaidi na utashi wa wavaaji.

Kama nchi ikilazimisha kuwa na vazi la Taifa kupitia mchakato utakaoingiza pia masuala ya kisheria, alisema wananchi wanaweza kujikuta wanalazimishwa kuvaa vazi ambalo haliwezi kutofautishwa na sare za wanafunzi.

Alihoji ni nchi gani imewahi kuendesha mchakato wa kupata vazi la Taifa ili akajifunze kwao.

Hata kabla ya kwenda kujifunza nje ya nchi alitaka kupata ushahidi wa mchakato wa kupata vazi la kabila la Wamasai ulivyosimamiwa hadi wakaonekana hivi walivyo sasa.

Alionya si busara kuwa na vazi la Taifa ambalo uvaaji wake umetungiwa sheria na kutaka suala hilo lihitimishwe, na kuwa Serikali inaacha wananchi wenyewe waongozwe na utashi wao kulingana na mila na tamaduni za maeneo yao.

Hata hivyo, msimamo wa Serikali kuhusu vazi la Taifa uliotangazwa na Nape kabla hajatoka wizarani unatofautiana na waziri aliyeteuliwa kushika nafasi yake, Dk Harrison Mwakyembe aliyenukuliwa hivi karibuni akisema kuwa mchakato wa vazi la Taifa ulikwama kwa kuwa kuna waliotaka kutumia fursa hiyo kujitafutia ulaji.

Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe wapo watu wanaotaka kutumia jambo hilo kujitengenezea ulaji, kwa kutaka kwenda kushona vazi hilo nchini China kazi aliyosema ingeweza kufanyika kwa ufanisi hapa nchini.

Wakati akijibu hoja ya Katibu Mkuu wa Shirikisho la Filamu nchini, Mathew Bicco, Waziri Mwakyembe alisisitiza kuwa kazi hiyo ingeweza kufanywa hata na wabunifu wa mitindo wa hapa nchini na hivyo Serikali kudhibiti ulaji huo kwa kusitisha suala hilo.

Katibu huyo awali alimwambia waziri kuwa Serikali inapaswa kulaumiwa, kwa kuwa hadi sasa imeshindwa kutangaza vazi rasmi la Taifa, alilosema lingepunguza uvaaji usio na maadili kwa baadhi ya wasanii.

Kikao hicho cha waziri na viongozi wa vyama na mashirikisho ya wasanii lililokuwa linajadili maadili ya mavazi katika tasnia hiyo, halikuweka wazi maazimio waliyofikia kuhusu ajenda ya vazi la Taifa.

Kama mchakato wa kupata vazi la Taifa ulisitishwa na Serikali ili kudhibiti ulaji ambao ungefanyika kwa kuwatumia wabunifu wa Kichina, ni wazi sasa wananchi wanatakiwa kufahamu ni lini mchakato huo utaanza upya baada ya kudhibiti watu hao.

Kutokana na kauli ya Waziri Mwakyembe, ni wazi kuwa nia ya Serikali ilikuwa ni kutaka kuwanufaisha wabunifu wa nyumbani kuliko kutumia gharama kubwa kunufaisha wabunifu wa Kichina na ndiyo msingi wa kukwama kwa mchakato huo.

Kimsingi, wabunifu wa hapa nyumbani bado wanahitaji fursa hiyo ili kuonyesha ujuzi wao, kwa kuwa hakuna sababu nyingine kubwa zaidi iliyotajwa na waziri wa sasa zaidi ya jambo hilo kusitishwa kwa sababu ya waliotaka kujinufaisha.

Hata hivyo, kauli ya Waziri Mwakyembe kuhusu mchakato wa kulipata vazi la Taifa inatofautiana na mtangulizi wake na hivyo kuwachanganya wananchi na wadau wa sekta ya sanaa kuhusu suala hilo.

Kauli mbili tofauti za mawaziri katika jambo moja, ni ushahidi kuwa kuna mambo ya msingi hatujakubaliana au ni jambo lisilopewa uzito na hivyo kujikuta linatolewa majibu ya kisiasa.

Badala ya kuendeleza mjadala wa vazi la Taifa ambalo kimsingi utekelezaji wake ni mgumu, ni muhimu tukaelekeza nguvu katika kulinda mila na tamaduni zetu ambazo ni chanzo cha kuporomoka kwa maadili.

Kwa mfano, hakuna juhudi za wazi kati ya Serikali na wadau zinazolenga kufanya kila mkoa nchini kuwa na kituo mahususi cha kuhifadhi na kulinda tamaduni za eneo husika kwa ajili ya urithi wa vizazi vijavyo na kutunza historia.

Hili ni miongoni mwa mambo mazuri yanayoweza kutekelezwa kulinda mila zetu, lakini hakuna anayelizungumzia.

Serikali iwe na kauli moja kuhusu vazi la Taifa, wakati hivyo hivvyo tuwajibike kuhifadhi na kulinda utajiri wa lugha za makabila yetu na tamaduni zinazolinda maadili mema katika jamii.

Phinias Bashaya ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Kagera 0767489094