ELIMU NA MALEZI : Elimu bora ilenge kuwawezesha wanafunzi kujitambua

Tuesday November 14 2017Christian Bwaya

Christian Bwaya 

By Christian Bwaya

Bila shaka umewahi kukutana na mtu mwenye kiwango kikubwa cha elimu lakini anafanya mambo yasiyofanana na elimu aliyonayo.

Wakati mwingine kitu kilekile kingefanywa na mtu unayejua hajaenda shule hakishangazi.

Lakini kwa kuwa aliyekifanya ni ‘msomi’ basi swali linakuwa, “Hivi huyu naye amesoma? Kama kusoma kwenyewe ndio huku, kuna haja gani ya kusoma?”

Jamii kwa kawaida ina matarajio makubwa kwa mtu aliyekwenda shule. Kiwango cha elimu anachokuwa nacho, mtu kinaijengea jamii matarajio fulani kwake.

Elimu inachukuliwa kama chombo chenye uwezo wa kubadili maisha ya mtu katika ujumla wake.

Tabia ya mtu aliyesoma inatarajiwa kuwa bora zaidi ya mtu asiyesoma. Hapa tunazungumzia mambo madogo, lakini yenye umuhimu kama vile heshima kwa watu.

Mengine ni uwezo wa kuvumilia mawazo tofauti na namna anavyoweza kuwasilisha mawazo yake.

Jamii inayachukulia mambo haya kama kiashiria cha kupima ‘usomi’ wa mtu.

Ingawa ni kweli ubora wa elimu ya mtu unaweza kupimwa kwa upeo wake wa kuona na kutatua matatizo yanayoikabili jamii, mara nyingi jamii haishii hapo. Jamii huyapa uzito mkubwa mambo ya kawaida yanayogusa utu wa watu.

Watu mathalani, wanataka kuona namna gani elimu aliyonayo mtu imemjengea tunu muhimu za maisha kama uadilifu, uaminifu, kusema kweli na unyenyekevu.

Tunu hizi ndizo zinazochukuliwa kwa uzito mkubwa wakati mwingine kuliko utaalamu alionao mtu.

Inapotokea mtu amesoma na bado akawa mwizi, tapeli, mlaghai, mwenye majigambo, mlevi, mzinzi, kwa kawaida watu huanza kuwa na wasiwasi na elimu yake.

Mara zote mtu anapoonyesha tabia hizi, watu watajiuliza, “Elimu ina faida gani kama mtu anafanya mambo ya kijinga kama haya?”

Katika muktadha huu, mabadiliko ya maisha huchukuliwa kama kipimo muhimu cha ubora wa elimu aliyoipata mtu.

Pia, jamii inaamini mtu aliyesoma lazima aweze kumudu maisha yake. Usomi wake ni lazima uende sambamba na kuboresha mtindo wake wa maisha.

Huwezi kwa mfano, kusema umeelimika na bado ukabaki kuwa masikini.

Katika macho ya jamii, umasikini ni kiashiria cha mtu aliyeshindwa kuelimika.

Elimu inatarajiwa ikusaidie kutumia maarifa yako kujipatia au kujiongezea kipato.

Inapotokea mtu anakuwa na elimu kubwa lakini hana uwezo wa kubadili changamoto zilizopo kwenye jamii kuwa fursa, watu wanakuwa na wasiwasi naye.

Wakati mwingine, hali hiyo huifanya jamii iwabeze wasomi kwamba wamepoteza muda mwingi kujifunza mambo ambayo yameshindwa kuwasaidia wao wenyewe kuboresha maisha yao wenyewe.

Kwa mujibu wa jamii, kushindwa kumudu maisha yako ni kiashiria cha elimu isiyokidhi haja anayoweza kuwa nayo mtu.

Inawezekana mitazamo hii inawakilisha mtazamo hasi wa jamii dhidi ya elimu.

Tunafahamu kwa mfano, lipo wimbi la kujaribu kuifanya fedha iwe ndio kipimo cha heshima ya mtu.

Lakini ni kweli pia kwamba wasomi wenyewe kwa namna wanavyoonekana kupitia mchango walionao kwa jamii, ndio waliochangia kukuza mtazamo hasi uliopo kwa jamii dhidi ya elimu.

Lakini kwa kuwa matokeo ya elimu ni sharti yaiguse jamii ambayo ndiyo mnufaika wake mkuu, ni dhahiri jamii isipoguswa na matokeo hayo, maana yake ni kwamba wasomi wameshindwa kutekeleza wajibu wao kwa jamii.

Zipo sababu nyingi zinazochangia kuifanya elimu ishindwe kuwa na manufaa kwa watu na jamii kwa jumla. Mojawapo ya sababu hizo ni msisitizo wake kwenye eneo moja tu la taaluma.

Tangu mwanafunzi anapoanza darasa la kwanza mpaka chuo kikuu anatarajiwa ‘kuelimika’ kwa kipimo cha kufaulu mitihani.

Mzazi anategemea mtoto arudi nyumbani na cheti chenye alama za juu. Wakuu wa elimu wanapozungumzia kupandisha kiwango cha elimu, wanafikiria ufaulu wa mitihani.

Mtazamo huo wa kutukuza taaluma dhidi ya maeneo mengine ya kimaisha unashushwa kwa mwalimu ambaye naye kwa nafasi yake, anakuwa hana namna nyingi zaidi ya kufanya kazi ya ziada kufikia matarajio hayo kwa kuhakikisha mwanafunzi anafaulu kwa kiwango cha juu.

Mwalimu anakuwa hana muda wa kusikiliza shida za mwanafunzi, kumsaidia mwanafunzi kujenga tabia njema, kwa sababu jitihada zake zote zinalenga kukuza eneo moja tu la maarifa.

Hata hivyo, hili si kosa la mwalimu pekee. Jamii yetu kwa ujumla wake, inaamini elimu ni uwezo wa kiakili unaomfanya mwenye akili aonekane kuwa bora kuliko mwenzake ‘asiye na akili’ za darasani.

Matokeo ya mtazamo huu finyu wa elimu, ni kudumaza maeneo mengine muhimu ya maendeleo ya binadamu. Kwa mfano, siha zinazokuza utu na utimamu wa binadamu kama vile nidhamu, maadili, bidii ya kazi, uaminifu, afya ya akili na mwili, stadi za maisha na ukuaji wa kiroho hazipewi nafasi inayostahili.

Hali iko hivyo kwa sababu mitalaa yetu imebaki kuwa na kazi moja kubwa. Kupanua ufahamu wa mtu na kukuza uwezo wake katika kudadisi mambo wakati mwingine kuliko kujielewa na kuwa binadamu timamu.

Tunatumia muda mwingi kuyaelewa mambo yanayotuzunguka lakini tunasahau kumfanya ‘msomi’ huyu aingie ndani yake na kujitafakari yeye ni nani na nafasi yake ni ipi katika jamii.

Matokeo yake wanafunzi hukazana kupata alama A darasani lakini wanadumaa kwenye maeneo mengine muhimu yatakayowasaidia kufanikiwa kwenye maisha.

Ni vyema tukatambua kwamba ufaulu mzuri usiokwenda sambamba na kujengwa kitabia hauwezi kuwa na manufaa ya maana.

Tunahitaji kuweka msisitizo katika kukuza maeneo yote muhimu kwa maendeleo ya mwanafunzi.

Tujenge mfumo thabiti ulio rasmi utakaosaidia kuwalea vijana kimaadili na kiroho ili maarifa wanayoyapata yawasaidie kuwa binadamu wenye tija kwa jamii.

Sera zetu za elimu hali kadhalika, zisiishie kuelimisha akili za vijana wetu na kuwaacha hawajitambui wao ni nani na nafasi yao katika jamii.

Vinginevyo, elimu itabaki na kazi ya kumwandaa mtu atakayesubiri kuajiriwa ili apate fursa ya kutumia maarifa yake kuiba na kujiletea manufaa yake binafsi.

Blogu: http://bwaya.blogspot.com

Advertisement