SAIKOLOJIA : Fahamu jinsi ya kuishinda tabia ya woga

Muktasari:

  • Wakati wowote jamaa au rafiki yake alipomweleza kuwa ana tatizo lakini anaogopa kufanya jambo litakalolitatua, yeye alisema “ondoa wasiwasi hayo ni mawazo yako tu”. Kila mara alimalizia kwa kusema, “Hakuna sababu ya kuogopa”.

Kila ninapoandika kuhusu madhara ya woga huwa naikumbuka tabia ya jamaa mmoja ambaye hata watu walimwita “Ondoa wasiwasi”.

Wakati wowote jamaa au rafiki yake alipomweleza kuwa ana tatizo lakini anaogopa kufanya jambo litakalolitatua, yeye alisema “ondoa wasiwasi hayo ni mawazo yako tu”. Kila mara alimalizia kwa kusema, “Hakuna sababu ya kuogopa”.

Wakati mmoja nilikabiliwa na changamoto iliyonifanya hata nikaingiwa na woga. Nilipomsimulia aliniambia maneno yake yaleyale. Nilipofuata ushauri wake nilipata nafuu, lakini kumbe ilikuwa ya muda. Baada ya muda mfupi ile hali ya woga ilinirudia.

Kadri nilivyotulia huku nikiamini kuwa hakuna sababu ya kuogopa, sikuona dalili yoyote ya kupungua makali ya changamoto iliyonikabili. “Kuondoa wasiwasi” ilikuwa hatua ya mwanzo muhimu katika kuishinda tabia ya woga.

Je, woga hutokana na nini?

Woga ni hulka ambayo kila binadamu anayo. Hata hivyo, kwa baadhi ya watu, tabia hii hupindukia ikawa kama kilema.

Humfanya mtu aogope hata kufuatilia mambo muhimu sana kwa maisha yake. Mtu mwoga hukosa uthabiti katika kutenda mambo mbalimbali yenye manufaa katika maisha. Kama ulivyo wasiwasi na hofu, woga ni athari ya kisaikolojia ambayo hutokana na hisia au mawazo hasi.

Mwoga anapofikiria kusimama mbele ya halaiki na kuongea huwaza fikra hasi kama vile je, nikiteleza na kuanguka mbele ya watu itakuwaje? Je kama nikishindwa kujieleza kwa lugha fasaha itakuwaje? Au mtu kama mie naweza kusimama mbele ya watu nikasema jambo watakaloliona la maana?

Matokeo yake ni kuogopa kabisa kusimama mbele ya watu na akijaribu atatetemeka na wala asiweze kueleza jambo linaloeleweka. Hizi ni fikra hasi ambazo husababisha woga. Kuna fikira hasi mbaya zaidi. Siku moja nilimsikia kijana mmoja akiwaambia wenzake “Mimi kuwa na nyumba yangu na gari yangu ni ndoto, wala haitatokea” Fikira kama hizi zimeshamtia woga wa kufanya jambo lolote litakalomwezesha kujenga nyumba au kupata gari.

Je woga unaweza kutibika?

Aina zote za woga ni maambukizo ya kisaikolojia ambayo huweza kutibiwa kama maradhi mengine ya aina hii. Mtu mwoga atakuwa amepata matibabu sahihi iwapo yatambadili kutoka kwenye tabia ya kujenga hisia hasi zinazoleta woga hadi kwenye tabia ya kujenga hisia chanya.

Hakuna mtu anayezaliwa akiwa na ujasiri na ushupavu. Watu wenye ujasiri na wanaoonekana hawana woga huwa wameipata tabia hiyo kutokana na mazoea yaliyojengeka kidogokidogo katika maisha yao. Hivyo ni dhahiri kuwa kila mmoja wetu mwenye tatizo la woga anaweza kujifunza jasiri. Kuna mwaka fulani niliwahi kuona mazoezi ya mabaharia. Niliambiwa kuwa moja katik sifa muhimu za baharia ni kuweza kuogelea na kupiga mbizi.

Siku hiyo niliwakuta vijana wakifanya mazoezi hayo. Walikuwa wakipanda kwenye ubao mrefu mwembamba uliokuwa umewekwa juu ya usawa wa bwawa la kuogelea. Kutoka kwenye ubao hadi kwenye bwawa ilikuwa meta 4. Walitakiwa waruke kutoka kwenye ubao na kujitupia bwawani. Walipotumbukia walipiga kwa kasi mbizi hatua chache kutoka pale walipoingilia majini kisha wakaibuka na kuogelea hadi ukingoni. Walipoanza zoezi karibuni vijana wote walikuwa wakiogopa kuruka na kujitupa majini. Hata ilibidi mwalimu wengine awasukume kwa kuwastukiza ndipo walipoweza kuruka. Kilichokuwa kikiwafanya wasiruke bwawani ni woga. Baada ya muda vijana wote waliweza kuruka bila woga wowote. Tena wakaona ni mchezo unawavutia.

Kutokana na mfano huu inabidi tujiulize ni kitu gani kilichowafanya vijana waogope na hatimaye waweze kuruka bila hofu yoyote. Ni dhahiri kuwa zoezi hili ililiwawezesha kujenga uwezo wa kudhibiti woga. Kilichowawezesha zaidi ni kujituma kufanya kitendo. Kila unapokabiliwa na woga tumia dhana ya kitendo.

Jiulize ninaweza kufanya kitendo gani ili kuushinda woga unaonifanya nihofu kutenda jambo hili lenye manufaa kwangu. Kumbuka kila woga anaoupata binadamu kuwa kitendo anachoweza kufanya ili kuondoa woga.

Kwa mfano mwanafunzi anayeogopa mtihani kwa kuhofia kuwa atafeli, ataweza kuondoa hofu hiyo kwa kuubadili muda anaoutumia kujisomea zaidi.

Aidha, kadri mtu anavyochelewa kufanya kitendo ndivyo jinsi wasiwasi na woga unavyozidi kuongezeka. Lakini kuna swali “Mtu atawezaje kubuni kitendo cha kufanya kwa kila aina ya woga? Wanafalsafa husema ubongo wa binadamu ni kama benki. Kila siku ubongo unahifadhi mawazo na fikira mpya.

Mawazo na fikira hukomaa yakawa kumbukumbu za kudumu katika akili ya binadamu. Wakati mtu anapotulia akawaza au anapokabiliwa na tatizo akafikiria sana, kwa hakika huwa anauliza benki yake jambo la kufanya.

Mara nyingi watu niliowafundisha kutumia mbinu hii wameniambia kuwa wanapofikiria kitendo cha kufanya kugundua wameamua kufanya bila wasiwasi wowote lile jambo walilokuwa wanaogopa kulifanya.