‘Lulu Diva kuleta homa ya muziki mzuri’

Muktasari:

Akisimulia safari yake ya muziki, Lulu anasema aliachia wimbo wake wa kwanza aliomshirikisha Baranaba mwishoni mwa Novemba mwaka jana, uliotayarishwa katika studio za High Table Sound.

Milele, ndiyo jina la wimbo uliomtambulisha katika ramani ya muziki, licha ya kwamba aliingia katika fani hiyo zaidi ya miaka 10 iliyopita akiwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Green Acres.

Huyu ni Lulu Abasi maarufu Lulu Diva, ambaye ameongeza namba ya wasanii wa kike nchini ambao hata wamekuwa wakipungua siku hadi siku kutokana na changamoto mbalimbali zilizopo kwenye tasnia hiyo kwa sasa.

Akisimulia safari yake ya muziki, Lulu anasema aliachia wimbo wake wa kwanza aliomshirikisha Baranaba mwishoni mwa Novemba mwaka jana, uliotayarishwa katika studio za High Table Sound.

Anasema licha ya wimbo wake kufanya vizuri, hajataka kukaa sana bali kwa sasa yupo katika mchakato wa kuachia wimbo mpya ambao ameupa jina ‘Usimuache’ ambao utaachiwa wiki mbili zijazo.

Wimbo huo umetayarishwa katika studio za MJ Records chini ya Marco Chali na video yake kufanywa na mwongozaji kutoka Afrika Kusini, Nicholaus.

Lulu Diva anasema aliamua kumtumia Nicholaus kwa kuwa alishaona kazi zake nyingi za wasanii wa nje na baada ya kufanya naye akagundua pia alitayarisha video ya wimbo Bado ya Harmonize na Diamond na Kokoro wa Rich Mavoko na Diamond pia.

“Niliona kuna tofauti kubwa kati ya waandaaji wa ndani na nje, wanaangalia wasanii na anapofanya kazi yako anaichukulia kwa uzito na hata kama iweje hakuchukulii kwamba umetoka Bongo, hatosheki na kile ambacho amekifanya haweki chochote kuonyesha kama ni mwenye kazi ,  kazi yake inasambazwa na midomo ya watu, nilielekezwa baada ya kuona video za watu wa nje,” anasema Lulu Diva.

Anasema kazi yake ameianza muda mrefu na ameshaimba nyimbo nyingi  ambazo hajazitoa.

“Nina albamu ya muziki kwa sasa tunajipanga kuitoa, ninapenda sana muziki na maskani yangu ni studio, mwenyewe niliamua kufanya muziki kwani ni kitu ambacho ninakipenda kuna wengine ambao hawakuniona nimetoka rasmi walikuwa wakiuliza sana kwa nini sijatoka na naona kabisa huu ni wakati wangu,” alisema.

Anasema awali alijitengea muda kwa ajili ya muziki kwani siku zote amekuwa akiamini kwamba muziki ni biashara na anaufanya kama kazi iliyo rasmi, kwani ameamua kufanya kibiashara.

Lulu anasema mpaka sasa ameshafanya shoo takribani nne ambazo anakiri kwamba zikilikuwa nzuri kwake ikiwemo After School Bash, Vodacom Party ya Diamond, na Natoka Tarehe 30.

“Ninachoangalia ni jina na nembo yangu ninavyosema kwamba naamua kutengeneza jina langu, ninafanya kitu kwa umakini na kama unategemea muziki ni biashara yako nimeupa kipaumbele, ninajiwekea hazina niwe na kazi nyingi, nimejipanga sijakurupuka kufanya muziki, niliona nini nikifanyie kazi katika muziki wangu,” anasema.

Wakati ujio wa Lulu Diva ukiwakuta baadhi ya wasanii wa kike wakiwa taaban kutokana na matumizi ya mihadarati, msanii huyo anasema amejipanga kuhakikisha kwamba anaepukana na vitendo hivyo huku akielimisha jamii.

Lulu anasema kwa kawaida msanii akishajulikana hupata marafiki wengi ambao huwa chanzo cha kushawishi, lakini kwa upande wake bado hana makundi wala marafiki, alionao hushirikiana kikazi bali kinachoweza kumwongoza ni uongozi wake pekee.

“Ikiwa bize na unachokifanya chochote kinachokuja unaona hakuna maana wapo niliowapenda katika muziki lakini sasa wamechoka na wanadhalilika, kudharaulika, wameshuka kimuziki kutokana na unga, nitaachia wimbo ambao utafundisha na kuhamasisha jamii kuhusu kuacha matumizi ya dawa za kulevya.

“ Nimedhamiria kuonyesha dunia athari za hivi vitu, mtu anaposikia muziki anapata mafunzo, nataka niachie wimbo wangu ambao utapinga matumizi ya dawa za kulevya,” anasema.

Meneja wa Lulu Diva kwa sasa, Mubenga ambaye anamiliki lebo ya Benga’s ENT, anasema mpaka sasa tayari wana wasanii wanne walio chini ya lebo hiyo.

Mubenga anasema wamejipanga na wiki mbili zijazo video mpya itaanza kuonekana, hivyo wengi wataanza kuelewa baada ya kuona kazi zake mpya zinazofuata tangu kuanza kusimamiwa na lebo hiyo.

“Mipango tuliyonayo ni kumtangaza zaidi hapa nyumbani kwa kuwa ni lazima ufanye vizuri kwenu ndipo uweze kujitangaza katika nchi jirani, kwa hiyo tunaimani Mungu akipenda na jinsi tulivyojiandaa watu wataona hata nyimbo zake zitakuwa za levo fulani, nina imani hatatuangusha,” anasema Mubenga.