Mfumuko wa bei una faida na hasara kwa uchumi wa Taifa

Muktasari:

  • Kuna viwango tofauti vya mfumuko wa bei ambavyo humaanisha mwenendo wa uchumi wa Taifa husika.

Kuna namna mbalimbali za kuelezea maana ya mfumuko wa bei. Kwa tafsiri ya kawaida mfumuko wa bei hupimwa kwa kutathmini ongezeko la bei ya bidhaa na huduma kwa kipindi fulani.

Kuna viwango tofauti vya mfumuko wa bei ambavyo humaanisha mwenendo wa uchumi wa Taifa husika.

Mfumuko wa bei unapokuwa asilimia sifuri au hasi humaanisha kushuka kwa bei. Ule wa asilimia sifuri mpaka asilimia 2.5 huonyesha bei ni imara sokoni.

Mfumuko wa kati ya asilimia 2.5 hadi asilimia 5.0 huonyesha kupanda kwa wastani kwa bei za huduma na bidhaa na unapokuwa kati ya asilimia 5.0 mpaka asilimia 8.0 huonyesha ongezeko kubwa la bei.

Aidha, mfumuko unapokuwa kati ya asilimia 8.0 na asilimia 12 humaanisha bei za huduma na bidhaa hujiongeza zenyewe wakati ule wa asilimia 12.0 hadi 20 haudhibitiki na zaidi ya asilimia 20 ni mfumuko uliokithiri.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), mfumuko wa bei nchini kwa Machi, ulikuwa asilimia 3.9 kutoka asilimia 4.1 wa Februari. Taarifa za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonesha lengo ni kuubakisha chini ya asilimia 5.0 ambao ni wa wastani.

Mfumuko wa bei hutajwa kuwa na faida pale unapokuwa mdogo, usioyumba na unabashirika. Zipo faida kadhaa za mfumuko wa bei ikiwemo kuwawezesha wanunuzi na wazalishaji kupanga mipango ya muda mrefu bila bei kubadilika.

Mnunuzi huwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa akiwa na nguvu ya kuzinunua wakati mzalishajii huwa na uhakika wa soko la bidhaa zake.

Pili, mfumuko mdogo wa bei hupunguza kiwango cha riba kinachotozwa na benki na taasisi za fedha. Kiuchumi kiwango cha riba hakiwezi kuwa chini ya mfumuko wa bei hivyo kumaanisha kiwango cha mfumuko wa bei hubainisha riba ya taasisi hizo.

Kiwango cha riba kinapokuwa kidogo huhamasisha watu wengi kukopa hivyo kuongeza uzalishaji, kutengeneza ajira zaidi na kusukuma maendeleo ya nchi kwa kulipa kodi.

Vilevile, mfumo mdogo wa bei, ulio imara na unaotabirika husaidia ukuaji wa uchumi kwa kuongeza kiwango cha uzalishaji wa bidhaa na huduma. Kinyume cha mfumuko wa bei ni kushuka kwa bei.

Bei ya bidhaa na huduma inaposhuka, uzalishaji hupungua hali inayopoteza ajira hivyo kupunguza kiwango cha mapato yatokanayo na kodi.

Hali hii ikiendelea kwa muda mrefu husababisha taasisi kusitisha uzalishaji hivyo kupunguza mapato ya nchi, ajira hatimaye huduma muhimu kukosekana.

Pamoja na faida za mfumuko wa bei zilizopo, kuna hasara zake pia ambazo ni pamoja na kupunguza faida kwa wenye utaratibu wa kuhifadhi fedha kwenye taasisi za fedha kama kiwango cha riba hakibadiliki.

Aliyehifadhi Shilingi milioni moja tangu mwaka 1990, kwa mfano, akiitoa mwaka 2018 thamani yake itashuka kutokana na mfumuko huo wa bei.

Mamlaka zinazofanya maamuzi ya kiuchumi hutatizika mfumuko wa bei unapokuwa hautabiriki na hauko imara. Ili maamuzi sahihi ya kiuchumi yaweze kufanyika ni lazima mfumuko wa bei uwe una kutabirika na kuvumilika.

Hali hiyo pia hupunguza uzalishaji, idadi ya wafanyakazi kisha mapato ya mtu mmoja na Taifa kwa ujumla. Kadiri mfumuko wa bei unayopanda ndivyo hali ya uchumi inayozidi kuwa mbaya.

Mfumuko ukiendelea kuwa hivyo husababisha mtisikisiko wa uchumi hasa kwa wenye vipato visivyobadilika kutokana na mazingira wakiwemo watumishi wa taasisi na wastaafu.

Mwajiri halazimiki kuongeza mshahara pale inapotokea mfumuko wa bei hivyo mwajiriwa hupata kipato ambacho hakikidhi mahitaji kutokana na hali hiyo.

Wakati mwingine Serikali inaweza kutengeneza mfumuko wa bei endapo inaendesha nchi kwa kutumia bajeti isiyotosheleza (nakisi). Hii hutokea pale Serikali inapokuwa imeshindwa kukusanya kodi au misaada na mikopo kama ilivyotarajia.

Hutengeneza mfumuko wa bei mkubwa ili taasisi za fedha ziongeze riba ya mikopo, kumbuka kiwango cha riba hakiwezi kuwa chini ya mfumuko wa bei, hali hii husababisha watu kushindwa kukopa, kushindwa kuzalisha hivyo kushindwa kutokuwa na fedha.

Mwisho wa siku fedha hubaki mikononi mwa Serikali na kuiwezesha kupanga kadiri inavyokusanya mapato kutoka kwenye vyanzo mbalimbali.

Ili kupunguza thamani halisi ya deni la Taifa, mfumuko wa bei unapokuwa mkubwa hupunguza thamani ya fedha ya ndani ukilinganisha na sarafu za kimataifa.

Ni kazi ya Serikali kupitia Benki Kuu kuhakikisha nchi inakuwa na mfumuko mdogo wa bei, ulioimara na unatabirika kwa maendeleo ya mwananchi na Taifa kwa ujumla.

Hakuna mtu au taasisi yoyote ya sekta binafsi yenye uwezo wa kufanya hivyo kwani yenyewe ni sehemu ya tu ya soko kubwa la hduma na bidhaa muhimu zinazouzwa na kununuliwa kwa matumizi ya kila siku.

Mwandishi ni mtakwimu na ofisa mipango.